Sunday, August 24, 2014

Hongera Rais Kikwete kwa kuahidi kuboresha sekta ya huduma ya afya kwa njia ya mtandao


Image result for kikwete
Picha: en.wikiquote.org     

Picha: ippmedia.com

Hongera Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuahidi kuboresha sekta ya huduma ya afya kwa njia ya mtandao.

Rais alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kisaki, Matombo, Dutumi na Kinole Morogoro vijijini. Aidha alisema huduma itakayotolewa itapunguza vifo vya wagonjwa hasa akina mama wajawazito na watoto.

Huduma ya matibabu kwa njia ya mtandao itafanya mawasiliano ya moja kwa moja kutoka kwa madaktari bingwa wa ndani na nje ya nchi wakati wa kutoa matibabu. Aidha, huduma ya mtandao imeonyesha mafanikio makubwa  kwa madaktari wa ngazi ya chini kuwasiliana na madaktari bingwa popote duniani na kuokoa maisha ya mgonjwa.

Blogu hii inaomba huduma hii itolewe nchi nzima hasa maeneo ya vijijini. Blogu hii inasisitiza kuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia hasa ya simu na internet inawezekana huduma ya namna hii kutolewa bila tatizo lolote. 

Ni rahisi kutoa visingizio kuwa baadhi ya vijiji nchini havina umeme wa kuchajia simu na vifaa vya kielektroniki. Lakini huduma za solar, betri za magari makubwa, pamoja na booster charger za kisasa zinasaidia katika kupatikana kwa nishati. Suala linalotakiwa ni kwa Wizara ya Afya pamoja na halmashauri za miji na mikoa kujipanga katika kufanikisha huduma ya afya kwa njia ya mtandao ili kuokoa maisha ya watanzania hasa wakina mama na watoto. 

Tuesday, August 12, 2014

Hongera Serikali kwa kuahidi kujenga barabara 4 za juu ‘flyover’ jijini Dar es Salaam ndani ya kipindi cha miaka 3

Hongera Serikali ya Jamhuri wa Tanzania, kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kuahidi kujenga barabara nne za juu ‘flyover’ jijini Dar es Salaam ndani ya miaka mitatu ijayo. Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli. Pia Mh Magufuli amesema Daraja la Kigamboni litakamilika ifikapo Juni mwakani.
Aidha Waziri wa Ujenzi amesema Serikali imetenga Sh2 bilioni kwa ajili ya kununua kivuko cha mwendo kasi kitakachokuwa kikitoa huduma kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa barabara za pembezoni ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Mh Magufuli amesema barabara za juu zitakazojengwa ni Tazara, Ubungo, Gerezani na DIT (Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam) na kuwaahidi watanzania kuwa ndani ya miaka mitatu foleni katika jiji la Dar es Salaam itakuwa historia.
 
Blogu hii inaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kuwa na lengo hili zuri ambalo litapunguza foleni jijini Dar es Salaam. Kupungua kwa foleni jijini Dar es Salaam kutaleta manufaa kwa wakazi wa jiji hili pamoja na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na jiji kwa ujumla. Aidha blogu hii inaomba juhudi hizi za Serikali ziende katika miji mingine mikubwa kama Arusha, Mwanza, Dodoma, Mbeya n.k.
 
Aidha, ombi la blogu hii ni kwamba Taifa lisisubiri kuwepo kwa foleni katika miji mikubwa ila ijiandae kabla idadi ya magari haijawa mengi. Kwa habari zaidi soma mwananchi.
 
Picha: mwananchi