Wednesday, April 20, 2016

Hongera Serengeti Boys kwa kuwafunga mafarao wa Misri mara mbili

Picha: tanzaniatoday.com
Licha ya kuwa ilikuwa mechi ya kirafiki ya kimataifa, blogu hii inaipongeza timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 serengeti boys kwa kuifunga timu ya taifa ya Misri mara mbili. Hakika kila mtanzania anajua ubora wa timu za Misri na hivyo kiwango walichoonyesha vijana wetu wa kitanzania kinahitaji pongezi za dhati. Pia blogu hii inawapongeza makocha na benchi zima la ufundi kwa juhudu walizofanya na wanazoendelea kufanya. Pia tunaipongeza TFF kwa kuilea timu hii na kuwa na mafanikio haya. Blogu hii inaomba TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu nchini na hasa wizara ya Elimu, Michezo na TAMISEMI kuunganisha nguvu na kuwa na mpango wa kuhakikisha michezo inachezwa na kushindaniwa kwenye shule zetu kiwilaya, kimkoa, kikanda na kitaifa. Kwa kufanya hivyo taifa litaweza kuwa na vijana wengi wenye vipaji na wanaojitambua maana watakuwa na ujuzi wa michezo na elimu ya darasani pia.

Hongera Dr John Pombe Magufuli kwa kuzindua daraja la kigamboni

Picha: teamtz.com
Hongera Dr John Pombe Magufuli kwa kuzindua daraja la kigamboni jana tarehe 19 Aprili 2016. Blogu hii inakupongeza wewe binafsi kwa kuwa ndiye ulikuwa waziri wa ujenzi wakati mchakato wa ujenzi unaendelea. Hakika daraja hili ambalo umependekeza liitwe daraja la nyerere linakuwa kioo cha taifa na pia litachochea maendeleo eneo la kigamboni na Dar es Salaam kwa ujumla. Pia tunaipongeza shirika la hifadhi ya jamii NSSF chini ya uongozi wa aliyekuwa mtendaji mkuu wake aliyepita Dr Ramadhan Dau kwa kutoa baadhi ya fedha zilizowezesha ujenzi wa daraja hili. Pia blogu hii inaipongeza serikali ya Jakaya Kikwete kwa kutoa uamuzi wa ujenzi wa daraja hili.

Blogu hii inaomba daraja hili litunzwe na watu wote na wasimamizi wawe wakali kwa yeyote atakayehujumu miundombinu ya daraja hili. Blogu hii inasema hivi kutokana na baadhi ya watu wasiowaaminifu kuhujumu miundombinu ya barabara na madaraja kwa sababu mbalimbali kama uuzaji wa vyuma chakavu. 

Aidha blogu hii inaomba serikali kuendelea na juhudu ya ujenzi wa barabara na hasa za juu jijini Dar es Salaam na majiji mengine ili kuondoa kero ya msongamano wa magari.