Saturday, July 26, 2014

Hongera DUCE na Wizara ya Elimu kwa ujenzi wa Jengo la Mihadhara timilifu. Wengine waige

Jengo la mihadhara katika  Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu. Unaweza kuona jengo lina 
mihadhara mitatu tofauti, nje kuna vitofali na njia ya lami pamoja na bustani na miti. 
Huu ni ujenzi kamili "timilifu" (Picha: Geofrey Kalumuna) 

Jengo hilo ni ukumbi mkubwa wa mihadhara katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu, DUCE (Dar es Salaam University College of Education), kilichopo jijini Dar es Salaam. Jengo hili lina mihadhara mitatu (3) kwa ajili ya kutoa mihadhara kwa wanafunzi wanaochukua shahada ya kwanza na diploma ya juu ya elimu. Mhadhara mmoja unaweza kuchukuwa wanafunzi na watu wengine waliokaa elfu 1 (1,000) kwa wakati mmoja.

Aidha jengo hili hutumika katika kuendesha mikutano mikubwa ya chuo, wanachuo pamoja na wadau wengine kutoka nje ya chuo kwa ruksa maalum. Blogu hii imeona itoe habari hii ili vyuo vingine nchini Tanzania viige mfano huu mzuri wa kuwa na zaidi ya mihadhara mitatu katika jengo moja ambapo shughuli tatu tofauti kwa watu wengi zinaweza kufanywa bila bughuza yoyote. 

Ndani ya jengo hili kuna huduma mbalimbali za ki-Tehama kwa ajili ya kurahisisha mihadhara. 

Kilicho ifurahisha zaidi blogu hii ni ujenzi "timilifu" unaojali mazingira, nje ya jengo kuna bustani nzuri, vitofali vinavyozuia vumbi na tope, pia pembeni kuna viti na meza za tofali nzuri kwa ajili ya watu kupunzika na wanafunzi kujisomea (vimbweta). Blogu hii kwa kutumia mfano huu wa DUCE, kuwa ni vyema kama kuna majengo ama barabara zinajengwa basi zijengwe "kikamilifu" ili kujali watu wote. Mfano kama tunajenga majengo tuzingatie pia mazingira nje ya jengo ama barabara. Ni vyema kama barabara inajegwa kuwe na njia kwa ajili ya watu, baiskeli na walemavu ambazo zina vitofali ili kuepuka vumbi wakati wa kiangazi ama tope wakati wa mvua. 

"Kwa maneno mengine haifurahishi kujenga jengo zuri lakini nje kuna tope ama vumbi ama kujenga barabara nzuri ambapo watu wanapita pembeni kwenye vumbi ama tope. Watanzania kwa hili tunaweza"

Hongera DUCE na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kujenga jengo la namna hii. Hongera pia kwa ujenzi timilifu. Kasi hii iendelezwe kwa vyuo vingine nchini ili vijana na watoto wetu wapate sehemu ya kupata mafunzo ya elimu ya juu kwa ubora unaostahili.

Saturday, July 19, 2014

Hongera TFF kwa kuanza kuuza tiketi za mechi za soka kwa njia ya kieletroniki kati ya Taifa Stars na Timu ya Taifa ya Msumbiji

Hongera Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa kuanza kuuza tiketi za mechi za soka kwa njia ya kieletroniki. Hakika blogu hii imefurahishwa sana na hatua hii ya maendeleo katika soka la Tanzania. Hivi karibuni TFF imetangaza kuuza tiketi za mchezo kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania "Taifa stars" na Timu ya Taifa ya Msumbiji "Mambas" utakaofanyika jumapili 20 Julai 2014. 

Utaratibu huu licha ya kuboresha mapato yatokanayo na uuzaji tiketi nchini pia unawawezesha wapenzi wa soka kununua tiketi bila taabu. Ni simu yako ya mkononi ndiyo itakuwezesha kununua tiketi yako. 

Blogu hii inaomba utaratibu huu uwe wa kudumu na hasa kwa mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara. Hongera sana TFF, Jamal Malinzi (Rais wa TFF), wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF, watendaji na wafanyakazi wa TFF, Max-Malipo na M-Pesa. Hakika maendeleo ya soka Tanzania yanawezekana!!

Ili kupata tiketi yako tumia M-PESA kwa kupiga *150*00# Kisha Bonyeza 4, Bonyeza tena 4 kisha weka Namba ya Kampuni 173399 Kisha Ingiza 7000 kama Namba ya Kumbukumbu ya Malipo, kisha andika tena 7000 kwenye Weka kiasi, Kisha weka namba ya siri na Baadaye bonyeza  1 Kukubali. Hapo utapokea ujumbe wenye orodha ya vituo vya MaxMalipo vya kuchukua tiketi ukiwa na namba ya uhakiki wa malipo yako.

Picha:tffnews.blogspot.com

Monday, July 7, 2014

Hongera VETA kwa kupata TUZO kwenye maonyesho ya 77 katika kipengele cha utoaji mafunzo na ujuzi

Hongera MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kupata TUZO kwenye maonyesho ya Sabasaba katika kipengele cha kundi la utoaji mafunzo pamoja na ujuzi nchini.
Hakika blogu hii imefurahishwa na juhudi za VETA katika kuwapa wananchi hasa vijana ujuzi ili kukabiliana na changamoto zilizopo nchini. Ujuzi wanaoupata vijana unawasaidia kuinua uchumi wa mtu moja moja na taifa kwa ujumla.
Blogu hii inaomba VETA izidi kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana na hasa walio katika mikoa na wilaya za pembezoni ili faida ya mafunzo iwe kwa taifa zima. Pia blogu hii inawaomba vijana bila ya kujali elimu walionayo kwa sasa kujiunga na vyuo vya VETA ili kupata ujuzi na maarifa ya kutenda kazi kivitendo. Nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea zimetilia mkazo mafunzo ya namna hii "Vocational and Technical Education". Uwepo wa mafunzo ya namna hii huziwezesha nchi zilizoendelea na zinazoendelea kupata Nguvu Kazi yenye ujuzi na maarifa katika nyanja mbalimbali kama vile ufundi mchundo, ufundi makenika, ufundi uashi, ufundi bomba, watengeza vywele, wapaka rangi, mafundi wa kompyuta na magari, madereva wa magari makubwa kama matreka, maroli, waendesha mitambo na mashine kubwa, wahudumu wa hoteli, waongoza watalii nk.
Maendeleo ya taifa lolote yanakuwa shakani bila ya kuwa na watu wa namna hii katika nchi ambao wamepata mafunzo rasmi ya ufundi stadi katika nyanja mbalimbali.Mfano, huwezi jenga barabara zenye uhakika bila ya kuwa na watu waliopitia VETA katika fani ya ujenzi. Nchi yetu ina mafundi wengi sana ambao hawajapitia VETA, na hivyo ubora wa huduma zao kuwa hafifu. Pia taifa linapaswa kupitisha sheria kwa kazi za namna hii zifanywe na wale tu walioudhuria mafunzo ya namna hii na kufaulu. Unataka kujiunga na VETA? Bonyeza hapa.
Picha: veta.go.tz