Saturday, July 26, 2014

Hongera DUCE na Wizara ya Elimu kwa ujenzi wa Jengo la Mihadhara timilifu. Wengine waige

Jengo la mihadhara katika  Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu. Unaweza kuona jengo lina 
mihadhara mitatu tofauti, nje kuna vitofali na njia ya lami pamoja na bustani na miti. 
Huu ni ujenzi kamili "timilifu" (Picha: Geofrey Kalumuna) 

Jengo hilo ni ukumbi mkubwa wa mihadhara katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu, DUCE (Dar es Salaam University College of Education), kilichopo jijini Dar es Salaam. Jengo hili lina mihadhara mitatu (3) kwa ajili ya kutoa mihadhara kwa wanafunzi wanaochukua shahada ya kwanza na diploma ya juu ya elimu. Mhadhara mmoja unaweza kuchukuwa wanafunzi na watu wengine waliokaa elfu 1 (1,000) kwa wakati mmoja.

Aidha jengo hili hutumika katika kuendesha mikutano mikubwa ya chuo, wanachuo pamoja na wadau wengine kutoka nje ya chuo kwa ruksa maalum. Blogu hii imeona itoe habari hii ili vyuo vingine nchini Tanzania viige mfano huu mzuri wa kuwa na zaidi ya mihadhara mitatu katika jengo moja ambapo shughuli tatu tofauti kwa watu wengi zinaweza kufanywa bila bughuza yoyote. 

Ndani ya jengo hili kuna huduma mbalimbali za ki-Tehama kwa ajili ya kurahisisha mihadhara. 

Kilicho ifurahisha zaidi blogu hii ni ujenzi "timilifu" unaojali mazingira, nje ya jengo kuna bustani nzuri, vitofali vinavyozuia vumbi na tope, pia pembeni kuna viti na meza za tofali nzuri kwa ajili ya watu kupunzika na wanafunzi kujisomea (vimbweta). Blogu hii kwa kutumia mfano huu wa DUCE, kuwa ni vyema kama kuna majengo ama barabara zinajengwa basi zijengwe "kikamilifu" ili kujali watu wote. Mfano kama tunajenga majengo tuzingatie pia mazingira nje ya jengo ama barabara. Ni vyema kama barabara inajegwa kuwe na njia kwa ajili ya watu, baiskeli na walemavu ambazo zina vitofali ili kuepuka vumbi wakati wa kiangazi ama tope wakati wa mvua. 

"Kwa maneno mengine haifurahishi kujenga jengo zuri lakini nje kuna tope ama vumbi ama kujenga barabara nzuri ambapo watu wanapita pembeni kwenye vumbi ama tope. Watanzania kwa hili tunaweza"

Hongera DUCE na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kujenga jengo la namna hii. Hongera pia kwa ujenzi timilifu. Kasi hii iendelezwe kwa vyuo vingine nchini ili vijana na watoto wetu wapate sehemu ya kupata mafunzo ya elimu ya juu kwa ubora unaostahili.

No comments:

Post a Comment