Hongera Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwa uzinduzi wa treni ya abiria toka Dar es Salaam kwenda Kigoma. Hakika treni hiyo ni nzuri na ya kisasa kwa dunia ya leo. Treni hii ni tofauti na treni za zamani zilizokuwepo nchini. Abiria akipanda treni hii anakuwa kama yuko nyumbani kwake maana anapata huduma za kisasa kama vile uwezekano wa kuendelea kutumia kompyuta, internet, kuchaji simu nk muda wote wa safari. Pia viti vya treni hii havimfanyi abiria kuchoka tofauti na viti vya zamani. Treni hii licha ya kuongeza wigo wa usafari wa abiria nchini pia unaokoa maisha ya watu kwa kuwa usafiri wa mabasi umekabiliwa na ajali ambazo baadhi ni uzembe wa binadamu.
Blogu hii inaomba abiria kuzingatia usafi na pia TRL kuwa wakali kwa yeyote atakayechafua mandhari ya treni hii bila sababu ya msingi. Blogu hii inaomba TRL wajiwekee "standards" za huduma kwa wateja kama vile kufanya ukarabati na marekebisho ya mara kwa mara ili treni hii ifanane kwa viwango na treni nyingine zilizoko Ulaya, Marekani na Asia. Pia TRL kuhakikisha kila abiria anayepanda treni hii anapata kiti ama chumba na kuondoa uwezekano wa kuwa na abiria wengi wasiokuwa na nafasi. Blogu hii inatarajia TRL kuwa na mkakati wa kuwa na treni zinazoenda kwa mwendo wa haraka yaani "Express" inayosimama vituo vichache sambamba na "ordinary" inayosimama vituo vingi zaidi.
Blogu hii inaipongeza sana TRL pamoja na Wizara ya Uchukuzi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasaidia wananchi hasa wa mkoa wa Kigoma ambao walikuwa wakikabiliwa na tatizo sugu la usafiri. Blogu hii inaomba safari hizi ziwe za kila siku toka Dar es Salaam kwenda Kigoma. Pia kuwe na safari za kila siku kwenda mikoa mingine ya Tanzania kuelekea Moshi na Mwanza. Kwa habari zaidi soma mwananchi.

Picha: mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment