Sunday, January 10, 2016

Hongera Samata kwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa kulipwa Afrika kwa wachezaji wa ndani 2015

Picha: taarifa.co.tz

Hongera Mbwana Samatta kwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa kulipwa barani Afrika kwa wachezaji wa ndani 2015. Hakika umeitangaza Tanzania kwenye ramani ya dunia. Blogu hii inakupongeza sana na kukutakia mafanikio mema. Blogu hii inawapongeza wadau wote waliofanikisha mafanikio ya Samatta kwa namna moja ama nyingine hasa Mh Ismail Aden Rage akiwa Rais wa Simba kwa wakati huo kwa kumruhusu kijana huyu kwenda TP Mazembe kucheza soka la kulipwa. Pia blogu hii inazishukuru klabu ya Simba Sports na African Lyon ya Mbagara kwa kumtunza na kumwonyesha njia kijana huyu. Aidha blogu hii inaishukuru TFF pamoja na Wizara ya Habari, Michezo na Wasanii na hasa Waziri wake Mh Nape Nnauye kwa jinsi alivyoonyesha ukaribu katika masuala muhimu ya soka na hasa suala la Samatta. 

Aidha blogu hii inawapa changamoto wachezaji wengine wa Tanzania na hasa wenye umri mdogo kufuata nyayo za Mbwana Samatta ili waweze kufikia malengo makubwa na kuwa wachezaji wakubwa wa kulipwa duniani.

Pia blogu hii inawaomba wadau wa soka nchini kuhakikisha wanajenga miundombinu sahihi ya kuibua vijana kama Samatta na hasa TFF kuhakikisha inaratibu uwepo wa "soccer academy" nyingi nchini kwa kushirikiana na serikali kupitia wizara za Michezo, Elimu na Tamisemi. Pia kuna haja ya serikali kuteua shule maalum za michezo na hasa soka na pia kuwa na vyuo vya ualimu vinavyozalisha wakufunzi wa michezo. Pia Wizara ya Elimu iweke somo la michezo na hasa kwa vitendo katika mtaala na katika mashule yote nchini ili kila mwanafunzi wa ngazi ya chini mpaka juu acheze na kujua angalau mchezo mmoja na hii itajenga utamaduni mzuri nchini. Pia serikali inaweza kutoa "incentive" kwa wanafunzi wenye kuonyesha kipaji cha mchezo wowote kwa kuhakikisha mwanafunzi huyo anafikia malengo. Pia ni wakati kwa jamii na serikali kwa ujumla kutambua nafasi ya michezo na usanii kama sehemu ya shughuli inayoweza kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment