Monday, August 8, 2016

Tumuunge mkono JPM kuamia Dodoma

Picha:en.wikipedia.org
Hakika, uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa serikali yake kuamia Dodoma ni wa kuungwa mkono na kupongezwa. Rais John Pombe Magufuli alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma mara baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti julai mwaka huu.

Blogu hii inaupongeza na kuunga mkono uamuzi huu na inawaomba watanzania wote kuunga mkono ili malengo yaliyowekwa na Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Nyerere miaka ya sabini yaweze kutimia.

Kijiografia, Dodoma ni katikati ya Tanzania na ni rahisi kufikika toka kona mbalimbali za nchi. Pia kiusalama, Dodoma ni mahali salama kwa nchi. Kiuchumi, Dodoma ni kiunganishi cha mikoa mingine nchini.

Blogu hii inaomba vyombo vyote vya serikali kujipanga na kutengeneza mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu (sio zaidi ya miaka mitano) kuhakikisha Dodoma inakuwa makao makuu kwa vitendo kiutawala, kisiasa, kiuchumi na kimiundombinu.

Blogu hii pia inaomba mamlaka za mkoa wa Dodoma na hasa CDA kujiongeza zaidi kwa kutengeneza miundombinu inayolenga mahitaji ya sasa na miaka 100 ijayo. Blogu hii ingependa hata kama uwezo wa kutengeneza barabara za lami zenye njia zaidi ya nane kwa pamoja haupo basi kwa makusudi ni muhimu kuacha sehemu ya barabara kwa ajili hiyo. Pia kubakisha sehemu ya upanuzi wa majengo ya serikali kama viwanja vya ndege, vituo vya reli, vituo vya mabasi, vituo vya maroli, hospitali, shule, vyuo nk ili upanuzi uweze kufanyika bila ya serikali kuingia kwenye ghrama kubwa ya kulipa fidia.

Mwisho, CDA na mamlaka za kiutawala Dodoma ziweke au ziuishe mpango wa mji wa Dodoma kwa kuwa na sehemu maalumu za viwanda vikubwa na vidogo (visiingiliwe), masoko makubwa ya kisasa (yenye kuzingatia usafi na mazingira), makazi bora ya watu yaliyo na mpangilio sawa (kama ni sehemu inatakiwa ghorofa moja mpaka nne basi ziwe hivyo au sehemu ni ghorofa kumi na kuendelea iwe hivyo hivyo).

No comments:

Post a Comment