Monday, December 16, 2013

Hongera Rais JK kwa kutoa hotuba nzuri sana katika mazishi ya MANDELA kijijini kwake Qunu

Sikiliza hotuba ya JK Qunu katika mazishi ya MANDELA 15/12/2013

Picha:Pool/AFP, Odd Andersen


Jana tarehe 15/12/2013 nikiwa nyumbani kwangu nikiangalia matangazo ya moja kwa moja ya luninga toka Qunu nchini Afrika ya Kusini kupitia chaneli ya MADIBA niliona na kusikiliza mambo mengi lakini mojawapo ni hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh Jakaya Mrisho Kikwete. Hakika katika hotuba hiyo JK alifunika. Kikwete aliwakumbusha wananchi wa Afrika ya Kusini walipotoka katika masuala ya kukomboa nchi yao. Kikwete aliwakumbusha wasauzi kuwa Tanzania iliwapa hifadhi pamoja na baadhi yao hati za kusafiria. Mandela alipewa yote hayo! Wasauzi enzi za ubaguzi wa rangi iliwapa hifadhi katika maeneo kama vile Kongwa, Mgagao, Mazimbu, Dakawa nk. 

Rais JK alisema Tanzania ilitoa ushirikiano wa hali ya juu na kusimamisha maendeleo yake kwa ajii ya Afrika ya Kusini. Wakati Mandela alipokuja Tanzania hakuwa na hati ya kusafiria "passport" ila alipewa "travel documents" toka Tanzania na aliweza kusafiri nchi mbalimbali. Tanzania ilianzisha Radio Freedom iliyokuwa inatangaza toka Tanzania Dar es Salaam kwa ajili ya ukombozi wa wananchi waliokuwa wanabaguliwa wa Afrika ya Kusini. Radio hii ilisaidia kuimarisha juhudi za ukombozi kusini mwa Afrika. Pia JK alisema, MANDELA alipokuwa anakuja Tanzania alikuwa haishi hotelini bali kwa watu binafsi ili kulinda usalama wake.

Hakika JK amewafungua macho na masikio wasauzi juu ya uhusiano uliokuwepo kati ya wananchi wa nchi hizi mbili na hasa wakati wa ukombozi. Hakusau kusema kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipigania sana ukombozi wa wananchi wa Afrika ya Kusini na alikuwa rafiki wa MANDELA. MANDELA alianza kutembelea Tanzania kutoka Afrika ya Kusini akipitia Northern Rhodesia, Tanganyika (Town of Mbeya) mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya kuomba msaada wa ukombozi na kupatiwa mafunzo ya wapigania uhuru na ubaguzi wa rangi.

JK alisema, Mandela alipotolewa gerezani na kutembela Tanzania miaka ya 90 alipokelewa na wananchi wengi waliokuwa na shauku ya kumuona mwanamapinduzi huyo. JK alisema licha ya mvua kubwa wananchi wa Tanzania walizidi kujitokeza kumshangilia. Nakumbuka wakati huo na mimi nilipata fursa ya kumuona akiwa pamoja na Mwalimu Nyerere na Winnie Mandela kwenye gari la wazi wakielekea Ikulu toka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam.

Blogu hii inampongeza sana JK kwa kutoa hotuba nzuri na kuwaeleza jinsi Tanzania ilivyoshiriki kikamilifu katika ukombozi kusini mwa afrika na hasa ukombozi dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Blogu hii inaomba taasisi husika ziweze kutunza kwa umakini na umaridadi mambo yote ili vizazi vijavyo na wageni waweze kujua jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika ukombozi. Maeneo yote ambayo kulikuwa na historia ya ukombozi hasa maeneo ya Morogoro yawe chini ya makumbusho ya Taifa ili pamoja na mambo mengine iwe mojawapo ya pato la taifa kupitia wageni toka nje nchi. Pia kuwe na matangazo kupitia radio, luninga, magazeti, internet juu ya historia, makumbusho na vitu vya kale vilivyopo Tanzania. Wenzetu mambo haya yanaingiza fedha na sisi tuchangamke!

Sikiliza hotuba ya JK Qunu katika mazishi ya MANDELA 15/12/2013

No comments:

Post a Comment