Serikali inakusudia kutoa maelfu ya tabuleti za kufundishia masomo mbali mbali nchini kwa walimu na wanafunzi wa shule za sekondari.
Ili kufanikisha mpango huo, Serikali inakusudia kuingia ushirikiano na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya
Opportunity Education Trust ya nchini Marekani ambayo hivi karibuni, ilizindua mpango wa majaribio wa utoaji wa tabuleti hizo kwa walimu na wanafunzi wa shule za sekondari nchini.
Mpango wa Serikali wa kusambaza tabuleti kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari ulitangazwa majuzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokutana na kuzungumza na Bwana Joe Ricketts, mmiliki wa taasisi ya Opportunity Education Trust na mmoja wapo wa matajiri wa Marekani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete amemweleza kwa undani Bwana Ricketts hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania kupania na kuboresha elimu tokea mwaka 2006, hatua ambazo zimechangia kupanua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa wigo wa utoaji elimu nchini.
Hakika blogu hii inaipongeza serikali ya Tanzania kwa jitihada inazofanya za kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufundisha na kujifunza. Mojawapo ya teknolojia hii ni matumizi ya tabuleti (tablets) ambapo mara nyingi iPad ndio inatumika sana.
Pia, blogu hii inampongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Kikwete kwa jitihada anazofanya katika kuboresha sekta ya elimu kupitia teknolojia. Blogu hii inapenda kutoa changamoto kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuandaa sera mbalimbali zitakazofanikisha suala hili katika sekta ya elimu nchini. Mojawapo ya sera ambayo itasaidia matumizi ya tabuleti kwenye mashule yetu ni sera ya matumizi ya mitandao ya kijamii katika elimu "social media in education". Bila ya kuwa na sera madhubuti itakuwa vigumu kutambua na kutumia na kupata faida ya mpango huu wa serikali. Sera ya matumizi ya mitandao ya kijamii itasaidia sana utumiaji wa vifaa hivi (tabuleti) kwa sababu "applications" nyingi sasa zinatumika kupitia mitandao ya kijamii. Na walimu na wanafunzi kwa njia moja ama nyingine watatumia vifaa hivi kupitia kwenye mitandao ya kijamii ili kuongeza kasi ya ufundishaji. Mara nyingi matumizi ya mitandao ya kijamii imekuwa kwa kiasi kikubwa siyo ya kusaidia kujifunza kwa wanafunzi wa kitanzania INGAWAJE mitandao hiyo ina mchango mkubwa katika elimu na katika kujifunza. Hivyo, kuwa na sera ni jambo muhimu sana.

Picha:ippmedia.com
No comments:
Post a Comment