Tuesday, December 23, 2014

Asante Rais KIKWETE kwa kuwabeba watanzania kupitia hotuba ya kuhitimisha sakata la Tegeta ESCROW

Picha: tanzaniatoday.co.tz

Jumatatu, ya tarehe 22 Desemba 2014 itakuwa siku ya kukumbukwa na watanzania ambapo Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alipohutubia taifa kupitia wazee wa jiji la Dar es Salaam. Kwa namna ya pekee kabisa blogu hii inampongeza kwa dhati Rais kwa hotuba yake nzuri katika kuhitimisha sakata la “account” ya Tegeta ESCROW.  

Rais alielezea historia nzima kiasi kwamba watanzania wengi wamepata uelewa mpana wa suala lenyewe. Aidha kwa namna ya pekee blogu hii inamshukuru kwa dhati kabisa kwa kukubaliana na mapendekezo ya Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kitendo cha Rais kuwashukuru wabunge wote ni cha kuigwa na watanzania wote.

Blogu hii haina haja ya kueleza hatua gani zimechukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa juu ya suala hili lakini hatua ya Rais ya kulivalia njuga suala hili kupitia hotuba yake kumeleta mwanga wa matumaini kwa watanzania na kuongeza utulivu na amani nchini. Kwa hakika blogu hii imeona ni kwa jinsi gani watanzania wasivyopenda vitendo viovu viendelee kutamalaki katika jamii zetu. Blogu hii imeshuhudia pia hata wapenzi wa chama tawala wamefurahishwa na hatua ambazo Rais amechukuwa za kupambana na maovu kupitia sakata hili. 

Kwa namna ya pekee blogu hii imefurahishwa kwa namna ambavyo Rais alivyo/anavyo chukua hatua juu ya sakata hili bila kuleta migongano kwa mihimili mingine na kwa jinsi anavyochukuwa tahadhari kuhakikisha haki inatendeka kwa kufuata sheria na taratibu za nchi. Kufuata haki, sheria na taratibu za nchi hata kwa wanaotuhumiwa katika sakata hili ni jambo zuri na linafaa kuigwa kwa viongozi wengine ndani na nje ya nchi yetu ili kuondoa dhana ya kumwonea mtu. Hii inadhihirisha utawala wa haki, sheria na kidemokrasia.

Blogu hii inaomba suala la maadili kwa wote na hasa watumishi wa serikali na viongozi wa umma litiliwe mkazo unaostahili. Tume ya Maadili ipewe nguvu zaidi, ipewe rasilimali watu zaidi na vitendea kazi bora ili iweze kufuatilia masuala ya kimaadili kwa ustadi mkubwa. Aidha mapambano ya rushwa yanatakiwa kupewa nguvu zaidi kwa kuimarisha taasisi ya kupambana na rushwa katika ngazi zote ikiwemo hata kwa serikali za mitaa ambapo ndipo chimbuko la uongozi wa nchi. 

Mwisho viongozi wapewe mafunzo ya uongozi, wajue uongozi ni dhamana, wajue wananchi ni nani na nini matarajiyo yao kutoka kwao. Miaka iliyopita chuo cha Kivukoni kilitumika pamoja na mambo mengine kuwaandaa na kuwapa maadili viongozi. Blogu hii inaomba utamaduni na utaratibu huo urudi, ili viongozi na hasa viongozi vijana wajue nini maana ya uongozi. Hii italifanya taifa letu lipige hatua kubwa ya maendeleo.


Asante JK kwa kuwabeba watanzania.   

Sunday, December 14, 2014

WANAWAKE WANAWEZA!!!! Hongera Jonisia Rukyaa kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchezesha MECHI kubwa ya SIMBA na YANGA ya NANI MTANI JEMBE 2

Hongera mwanamama (Jonisia Rukyaa) toka mkoa wa Kagera kwa kuwa mwanamke wa kwanza nchini Tanzania kuchezesha mechi kubwa ya watani wa jadi, Simba Sports Club (Simba) na Young Africans Sports Club (Yanga) kupitia shindano la Bia ya Kilimanjaro ya NANI MTANI JEMBE 2. Katika mechi hiyo iliyofanyika jana (jumamosi, 13/12/2014) jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Taifa, ambapo SIMBA waliibuka na ushindi wa mabao 2 kwa 0. Blogu hii inaomba wanawake wengine wajitokeze katika nyanja mbalimbali hususan michezo ili kufuata nyayo za mwanamama huyu hodari.

Hakika blogu hii inakupongeza sana licha ya changamoto chache zilizojitokeza ambazo hata upande wa waliopoteza (YANGA) wanazikubali. Blogu hii inakuomba utafute mkanda wa mechi ile na uondoe makosa machache ambayo WOTE tuliyaona. Ila kwa kiasi kikubwa ulijitahidi sana. Big UP mwanamama, Kweli WANAWAKE wanaweza!! Tembelea michuzi ujionee picha za mchezo huo muhimu.

Picha: Michuzi blog

Wednesday, December 10, 2014

Hongera Idris Sultan kwa kujizolea kitika, takriban milioni 500 za kitanzania toka shindano la Big Brother Hotshots nchini Afrika Kusini

Hongera Idris Sultan kwa kujizolea kitika, takriban milioni 500 za kitanzania. Blogu hii imefurahishwa na ushindi huu ulioupata toka BBA katika shindano la Big Brother Hotshots nchini Afrika Kusini. Ushindi huu si wa Idris pekee bali ni ushindi wa watanzania wote. Ushindi huu pia unawafundisha vijana wengine wa kitanzania katika nyanja zote za michezo, sanaa na muziki kuwa inawezekana kupata ushindi. Blogu hii inaomba vijana wengine katika nyanja zote waige mfano wa kujituma bila ya kukata tamaa kama alivyoonyesha Idris katika shindano hili. Hongera sana Idris. Kwa habari zaidi bofya

Picha:bigbrotherafrica


Monday, December 1, 2014

Hongera Bodi ya Utalii kwa kutangaza vivutio vya utalii vyaTanzania kupitia Ligi Kuu ya Uingereza

Picha:tanzaniatoday.co.tz

Hongera Bodi ya Utalii ya Tanzania kwa kutangaza vivutio vya utalii kupitia ligi maarufu duniani, Ligi Kuu ya Uingereza. Kila mmoja wetu anajua umaarufu wa Ligi hii duniani. Ni ligi inayofuatiliwa na kutazamwa na watu wengi sana duniani kupitia njia mbalimbali ikiwemo matangazo ya Luninga. Katika mechi kati ya Sunderland na Chelsea ambapo wachezaji wa Sunderland walivalia jezi za mazoezi (T-shirts) zilizokuwa na tangazo “Visit Tanzania” Mechi hiyo iliyofanyika nchini Uingereza iliishia kwa timu hizo kutoka suluhu ya bila kufungana. Ni matumaini ya blogu hii watu wengi walitazama tangazo hilo na hata kumbukumbu kubaki katika mitandao mbalimbali duniani. 

Hakika hili ni jambo zuri kwa maana lina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa taifa kupitia utalii. Tanzania ni nchi yenye vivutio vingi vya utalii ikiwemo Mbuga ya Serengeti, Mikumi, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, vivutio vya Zanzibar na Bagamoyo nk. Kupitia Tangazo hili nchi yetu itatembelewa na watalii wengi zaidi na kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.

Blogu inaipongeza serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kuitangaza Tanzania. Vile vile Bodi ya Utalii pamoja na Wizara husika zinastahili pongezi za dhati. Juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa. Blogu hii inaishauri serikali kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa abiria (watalii) kupitia viwanja vyetu vya ndege, hivyo ni wakati muafaka wa kiviboresha zaidi na kuwa na hadhi na mahitaji ya kimataifa. Blogu hii inatambua upanuzi wa kiwanja cha Mwalimu Julius Nyerere cha Dar es Salaam, hata hivyo viwanja vingine hasa Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar vinapaswa kuboreshwa ili kupokea wingi wa watalii na wageni toka nje ya nchi.

Kwa habari zaidi tembelea Tanzania tourist board  uone vivutio vilivyoko Tanzania.