Tuesday, December 23, 2014

Asante Rais KIKWETE kwa kuwabeba watanzania kupitia hotuba ya kuhitimisha sakata la Tegeta ESCROW

Picha: tanzaniatoday.co.tz

Jumatatu, ya tarehe 22 Desemba 2014 itakuwa siku ya kukumbukwa na watanzania ambapo Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alipohutubia taifa kupitia wazee wa jiji la Dar es Salaam. Kwa namna ya pekee kabisa blogu hii inampongeza kwa dhati Rais kwa hotuba yake nzuri katika kuhitimisha sakata la “account” ya Tegeta ESCROW.  

Rais alielezea historia nzima kiasi kwamba watanzania wengi wamepata uelewa mpana wa suala lenyewe. Aidha kwa namna ya pekee blogu hii inamshukuru kwa dhati kabisa kwa kukubaliana na mapendekezo ya Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kitendo cha Rais kuwashukuru wabunge wote ni cha kuigwa na watanzania wote.

Blogu hii haina haja ya kueleza hatua gani zimechukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa juu ya suala hili lakini hatua ya Rais ya kulivalia njuga suala hili kupitia hotuba yake kumeleta mwanga wa matumaini kwa watanzania na kuongeza utulivu na amani nchini. Kwa hakika blogu hii imeona ni kwa jinsi gani watanzania wasivyopenda vitendo viovu viendelee kutamalaki katika jamii zetu. Blogu hii imeshuhudia pia hata wapenzi wa chama tawala wamefurahishwa na hatua ambazo Rais amechukuwa za kupambana na maovu kupitia sakata hili. 

Kwa namna ya pekee blogu hii imefurahishwa kwa namna ambavyo Rais alivyo/anavyo chukua hatua juu ya sakata hili bila kuleta migongano kwa mihimili mingine na kwa jinsi anavyochukuwa tahadhari kuhakikisha haki inatendeka kwa kufuata sheria na taratibu za nchi. Kufuata haki, sheria na taratibu za nchi hata kwa wanaotuhumiwa katika sakata hili ni jambo zuri na linafaa kuigwa kwa viongozi wengine ndani na nje ya nchi yetu ili kuondoa dhana ya kumwonea mtu. Hii inadhihirisha utawala wa haki, sheria na kidemokrasia.

Blogu hii inaomba suala la maadili kwa wote na hasa watumishi wa serikali na viongozi wa umma litiliwe mkazo unaostahili. Tume ya Maadili ipewe nguvu zaidi, ipewe rasilimali watu zaidi na vitendea kazi bora ili iweze kufuatilia masuala ya kimaadili kwa ustadi mkubwa. Aidha mapambano ya rushwa yanatakiwa kupewa nguvu zaidi kwa kuimarisha taasisi ya kupambana na rushwa katika ngazi zote ikiwemo hata kwa serikali za mitaa ambapo ndipo chimbuko la uongozi wa nchi. 

Mwisho viongozi wapewe mafunzo ya uongozi, wajue uongozi ni dhamana, wajue wananchi ni nani na nini matarajiyo yao kutoka kwao. Miaka iliyopita chuo cha Kivukoni kilitumika pamoja na mambo mengine kuwaandaa na kuwapa maadili viongozi. Blogu hii inaomba utamaduni na utaratibu huo urudi, ili viongozi na hasa viongozi vijana wajue nini maana ya uongozi. Hii italifanya taifa letu lipige hatua kubwa ya maendeleo.


Asante JK kwa kuwabeba watanzania.   

No comments:

Post a Comment