Saturday, March 28, 2015

Hongera JK kwa kuzindua treni ya kubeba mizigo toka Dar es Salaam kwenda nchi jirani

Uzinduzi wa treni ya mizigo toka Dar es Salaam kwenda nchi jirani hususan Rwanda ni jambo jema sana kwa ustawi wa nchi za maziwa makuu na ukanda wa Afrika Mashariki. Aidha uzinduzi wa treni ya mizigo mbali na kupunguza gharama kubwa za usafirishaji pia zitapunguza kwa kiasi kikubwa muda unaopotea njiani kutokana na vikwazo mbalimbali barabarani. Pia uzinduzi huu utapunguza usumbufu usiokuwa wa lazima.

Blogu hii inaipongeza sana serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Dr Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutimiza lengo muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na nchi jirani. Hakika haya ndiyo maendeleo wananchi wanayoyataka. 

Blogu hii inaomba serikali ijikite zaidi kuhakikisha kuna kuwa na usafiri wa treni kila siku kwa ajili ya kusafirisha mizigo na abiria toka Dar es Salaam kwenda mikoani na nchi jirani. Usafiri wa treni duniani kote ni usafiri wenye usalama na gharama nafuu ukilinganisha na usafiri wa mabasi. Aidha blogu hii inaomba serikali iwekeze katika usafiri wa reli ndani ya majiji kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Tanga na Arusha ili kukabiliana na msongamano wa magari barabarani. 

Kwa habari zaidi tembelea wavuti

Rais Kagame akinyanyua bendera kuashiria uzinduzi wa Treni ya Mizigo 
toka Dar es Salaam kwenda Rwanda (http://www.wavuti.com)

Saturday, March 7, 2015

Hakuna kama Azam Tv nchini Tanzania.


Picha: tanzaniatoday.co.tz

Hakuna kama Azam Tv. Jana tarehe 06 mwezi 03 mwaka 2015 itakuwa siku ya kukumbukwa katika sekta ya habari ya nchini Tanzania mara baada ya kituo cha Azam Tv kuzindua studio mpya ya kisasa yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 31 (zaidi ya bilioni 56 za kitanzania). 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Jakaya Kikwete ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo na ndiye aliyekata utepe akiambatana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Dr Fenella Mukangara sambamba na viongozi na wafanyakazi wa Azam Tv Tabata Relini jijini Dar es salaam.

Hakika blogu hii inaipongeza sana Azam Tv hususan wamiliki na uongozi wake kwa ujumla kwa juhudi za dhati za kuboresha sekta ya habari nchini. Kituo hiki ambacho kina mwaka mmoja toka kianzishwe kimepiga hatua kubwa sana. Moja ya hatua kubwa ambayo kila mtanzania anaiona ni kuonyesha "live" ligi mbalimbali za michezo ikiwemo Ligi Kuu ya Vodacom. Blogu hii inaamini Azam Tv itakuwa na ubora kama vituo vingine vya kimataifa kama vile BBC, CNN SKY nk. SISI ni Azam Tv wewe je?

Asante Mh. Dr. Magufuli kwa kumfagilia Mh. Mbowe na kuonyesha kuwa siasa sio chuki bali ni maendeleo

Picha:mwananchi.co.tz

Asante sana mpiganaji, mchapakazi na mzalendo wa kweli Mh Dr. John Pombe Magufuli kwa kuwafundisha wananchi wa Tanzania kuwa siasa sio chuki wala ugomvi. Siasa ni kuwa na mitazamo tofauti yenye nia moja ya kuwaletea wananchi maendeleo na si vinginevyo. Mh Dr. Magufuli alimtaja kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Mh. Freeman Mbowe (Mbunge wa Hai) kuwa ni kiongozi anayefuatilia maendeleo ya watu wake bila ya kujali itikadi za kisiasa. Mh Dr. Magufuli aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara inayotoka Kwasadala kupitia Masama mpaka Machame hivi karibuni.

Blogu hii inampongeza sana Mh Dr. Magufuli kwa kauli yake nzuri inayoleta umoja na amani ya kweli kwa watanzania. Blogu hii inawaomba wanasiasa wengine kuiga mwenendo huu kwani mitazamo tofauti ya siasa sio nongwa! Tuepuke watu wanaopenda kuona taifa hili ama viongozi wa kisiasa wakikinzana bila sababu ya msingi.

Kwa habari zaidi soma mwananchi.


Monday, March 2, 2015

Asante Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa kauli dhabiti "kama kuwa na kiungo cha albino ndio kupata utajiri basi albino wote duniani ndio wangekuwa na utajiri mkubwa kuliko wote"

Image result for kikwete
Picha:thehabari.com
Maneno hayo yamesemwa leo (02/03/2015) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete wakati akihutubia taifa. Hakika kauli hiyo inapaswa kuingia akilini kwa watu wote na hasa kwa wale wenye imani potofu juu ya walemavu wa ngozi. Rais kwa mshangao alisema “kama kuwa na kiungo cha albino ndio kupata utajiri basi albino wote ndio wangekuwa matajiri wakubwa duniani”. Alisisitiza kama ingekuwa kweli basi wahusika (albino) ndio wangekuwa na utajiri mkubwa kwa kuwa wao wenyewe wana viungo hivyo mwili mzima! 

Hivyo amewaomba watu wapuuze ujinga uliopo kuwa viungo vya watu wenye changamoto ya viungo (albino) vinaleta utajiri. Janga hili ni kubwa na la ajabu ambalo dunia inatutizama kwa jicho la kustaajabu. Kila mmoja wetu kwa nafasi aliyonayo apambane na janga hili kwa nguvu kubwa. 

Blogu hii inampongeza sana Rais kwa kauli yake hii na pia inaomba vyombo vya serikali kuchukua na kutumia kauli hii katika kuondoa fikra mbovu ya baadhi ya watu wenye kufikiri viungo vya albino vinaleta utajiri. Pia blogu hii inaomba vyombo vya dola kupambana na waovu hawa kwa kasi kubwa. Pili mahakama ziendeshe kesi za waovu hawa kwa kasi kubwa pia. Blogu hii inaomba taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano kukemea mauaji haya ya wenzetu wenye changamoto ya ngozi. 

Blogu hii inaamini sekta ya elimu ina mchango mkubwa katika kuwaelimisha watu toka wakiwa wadogo mashuleni na vyuoni ili kuondokana na dhana hii mbovu vichwani mwa watu.

Mwisho, blogu hii inatarajia wanaharakati wa haki za binadamu kupambana na uovu huu mkubwa.
J