Picha:thehabari.com
Maneno hayo yamesemwa leo (02/03/2015) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete wakati akihutubia
taifa. Hakika kauli hiyo inapaswa kuingia akilini kwa watu wote na hasa kwa wale wenye imani potofu juu ya walemavu wa ngozi. Rais kwa mshangao alisema “kama kuwa na kiungo cha albino ndio kupata utajiri basi albino wote ndio wangekuwa matajiri wakubwa duniani”. Alisisitiza kama ingekuwa
kweli basi wahusika (albino) ndio wangekuwa na utajiri mkubwa kwa kuwa
wao wenyewe wana viungo hivyo mwili mzima!
Hivyo amewaomba watu wapuuze ujinga uliopo
kuwa viungo vya watu wenye changamoto ya viungo (albino) vinaleta utajiri. Janga hili ni kubwa na la ajabu ambalo dunia inatutizama kwa jicho la kustaajabu. Kila mmoja wetu kwa nafasi aliyonayo apambane na janga hili kwa nguvu kubwa.
Blogu hii inampongeza sana Rais kwa kauli yake hii na pia inaomba vyombo vya
serikali kuchukua na kutumia kauli hii katika kuondoa fikra mbovu ya baadhi ya
watu wenye kufikiri viungo vya albino vinaleta utajiri. Pia blogu hii inaomba
vyombo vya dola kupambana na waovu hawa kwa kasi kubwa. Pili
mahakama ziendeshe kesi za waovu hawa kwa kasi kubwa pia. Blogu hii inaomba
taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali pamoja na Bunge la
Jamhuri ya Muungano kukemea mauaji haya ya wenzetu wenye changamoto ya ngozi.
Blogu hii inaamini sekta ya elimu ina mchango mkubwa katika kuwaelimisha watu toka wakiwa wadogo mashuleni na vyuoni ili kuondokana na dhana hii mbovu vichwani mwa watu.
Mwisho, blogu hii inatarajia wanaharakati wa haki za binadamu kupambana na uovu huu mkubwa.
J
No comments:
Post a Comment