Friday, November 22, 2013

Hongera serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kutoa Sera ya Gesi nchini

Hongera serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kutoa sera ya gesi ya mwaka 2013. Sera hii imeeleza wazi kuwa gesi ni mali ya taifa na inapaswa kuwanufaisha wananchi na pia itauzwa nje ya nchi pale tu mahitaji ya ndani yatapotimizwa. Sera hiyo imeainisha kuwa ni lazima serikali na wananchi wanufaike na rasilimali hiyo na pia kunakuwa na haki na usawa kwa wadau katika uvunaji na utumiaji wa rasilimali hiyo. Sera hiyo imesisitiza kujenga mifumo ya kitaasisi, miundombinu na nguvu kazi ya kuhudumia na kuendeleza sekta ya gesi nchini.

Hakika blogu hii inaipongeza sana serikali pamoja na wadau wengine kwa kufanikisha sera hii muhimu kwa taifa. Ni wakati muafaka kwa wadau na wananchi kuchangamkia fursa itakayotokana na uchimbaji na usambazaji wa gesi nchini. Ni matumaini ya blogu hii kuwa uchimbaji na usambazaji wa gesi utanufaisha taifa na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla. 

Photo:dullonet.com




Photo:dewjiblog.com


Wednesday, November 20, 2013

Hongera Mh. Ummy Mwalimu kwa kulinda na kutetea haki za watoto pamoja na kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji

Mh. Ummy Mwalimu leo ameshiriki katika maadhimisho ya siku ya Maombi na Vitendo kwa Watoto, katika viwanja vya Don Bosco mjini Dar es Salaam. Washiriki wengine katika maadhimisho hayo walikuwa Global Network of Religions for Children (GNRC), InterReligious Council of Peace Tanzania (IRCPT) na UNICEF. Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na UN Universal Children's Day. Ambapo KauliMbiu ya Mwaka huu ni "Zuia Ukatili Dhidi ya Watoto". Mh. Ummy alipata fursa ya kuelezea hatua mbalimbali za kisera na kisheria zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya Ukatili dhidi ya watoto. 

Mh. Ummy amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Mtoto imeanza kutekeleza Mpango wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto 2013-2016. Mpango huu umejielekeza katika kuimarisha mifumo ya kisheria katika utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya 2009 na katika kujenga mifumo imara ya ulinzi wa mtoto kwa ajili ya kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili. Mh Ummy ameiomba jamii kwa ujumla kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinakoma. Pia amewaomba wazazi, walezi, viongozi wa dini, watoto na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na kuzingatiwa. 

Hakika blogu hii inampongeza sana Mh. Ummy kwa jitihada anazofanya za kulinda na kutetea haki za watoto pamoja na kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wafanyiwavyo watoto.

Blogu hii inaomba jamii kwa ujumla kushirikiana na Mh Ummy pamoja na serikali kwa ujumla kupinga vitendo vya ukatili wa watoto. Pia jamii kuripoti kwenye vyombo vya dola waonapo uwepo wa vitendo vya ukatili kwa watoto. Blogu hii inaamini kwa kufanya hivyo, vitendo vya unyanyasaji vitapungua ama kwisha kabisa. Pia blogu hii inaomba mkakati wa kupinga unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto uanzie kwenye shule za awali, msingi mpaka sekondari. 

Sio lazima kukawa na mtaala rasmi ila kuna kitu kinaitwa "hidden curriculum" ambapo walimu watapewa maelekezo ama mafunzo ya namna ya kuwaelimisha watoto juu ya HAKI na WAJIBU wao. Baadhi ya nchi zinafanya hivyo, mfano mtoto akinyanyaswa anaelekezwa ama anafundishwa wapi apeleke taarifa hata kama atakayekuwa anamnyanyasa ni mzazi, mlezi ama ndugu. Mbali na kufundishwa HAKI na WAJIBU wao WATOTO pia wafundishwe kwa njia hiyo hiyo UZALENDO, USAFI NA MAZINGIRA, MICHEZO nk ili angalao utupaji wa taka ovyo ukome, rushwa ikome na MATOKEO yake ni baada ya miaka 10 ama 15 taifa litapiga hatua kubwa ya maendeleo!

Viwanja vya Don Bosco mjini Dar es Salaam

Thursday, November 14, 2013

Tuongeze kasi ya ujenzi wa viwanda ili kuwapa ajira vijana waliomaliza mafunzo ya ufundi VETA

Miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa na kiwanda cha kuunganisha magari makubwa yaitwayo SCANIA mjini Kibaha mkoani Pwani. Kiwanda hicho cha kuunganisha MAGARI ya aina hiyo mbali na kuinua uchumi wa nchi kupitia mapato kama vile kodi pia kilileta mchango mkubwa kwa vijana waliopitia mafunzo ya ufundi (siku hizi VETA nk).

Viwanda vya aina hii vipo sehemu nyingi duniani ikiwemo Afrika ya Kusini, katika jiji la Johannesburg. Kiwanda hiki kilichopo Afrika ya Kusini mbali na kuinua uchumi wa nchi hiyo kina ajili vijana waliomaliza mafunzo mbalimbali ya ufundi ikiwemo mafunzo kama yatolewayo na VETA nchini Tanzania.

Blogu hii inaomba kuwepo na viwanda vya aina hii na hasa kurudisha kiwanda cha kuunganisha SCANIA nchini Tanzania ili mbali na kuinua uchumi kupitia kodi na mauzo ya MAGARI husika ndani na nje ya nchi pia kitaajiri vijana wengi waliopitia mafunzo ya ufundi. Hali hii itawafanya vijana wapate ajira na kupunguza uhalifu nchini. 

Blogu hii inaamini serikali na wadau wengine wametumia pesa nyingi kujenga vyuo vya ufundi VETA, hivyo basi ili mafunzo hayo yalete matunda inabidi kuwe na viwanda vya aina hiyo.

Hata hivyo nchini Tanzania kuna ongezeko la viwanda mbalimbali ambavyo vinatoa fursa kwa vijana kupata ajira na kutumia ujuzi wao walioupata toka  vyuo mbalimbali vya VETA na hivyo kujiongezea kipato na kuinua uchumi wa nchi. 

Kasi ya kujenga viwanda kupitia sekta binafsi na wawekezaji wakubwa inabidi iongezwe kwa kushirikiana na serikali.

Picha: Geofrey Kalumuna




Monday, November 11, 2013

Rais UHURU KENYATTA wa KENYA asema KENYA iko tayari kushirikiana na Tanzania

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kupitia waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Mh. Amina Mohamed, ametuma salamu akisema kuwa nchi ya Kenya iko tayari kushirikiana na Tanzania. Hata hivyo, Rais wa Kenya amesema kwamba  walijiingiza katika mazungumzo na Uganda pamoja na Rwanda kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta na reli bila kufahamu kwamba ilikuwa inavunja misingi iliyowekwa na jumuiya hiyo.
 
Hakika hatua hii ya kistaarabu ni ya kipekee na inastahili kupokelewa kwa mikono miwili na watanzania pamoja na Rais wetu JK. Yalizungumzwa mengi, kabla ya Rais Kenyatta kutoa msimamo huo kupitia waziri wake wa mambo ya nje.
 
Blogu hii inaamini kuwa UMOJA NI NGUVU! NA UTENGANO NI UDHAIFU. Ikumbukwe, Tanzania ni sehemu ya AFRIKA MASHARIKI kijiografia, kihistoria, kiasili na pia itakuwa kosa kubwa sana kujitoa!. Ni furaha ya blogu hii kuwa kweli JK alizungumza vitu vya kweli vilivyotokea kabla. Hii inadhibitishwa na kauli ya UHURU na sasa angalau mambo yatakuwa shwari. AFRIKA MASHARIKI IDUMU!
 
Picha: mwananchi -  Mh. Bernard Membe (waziri wa mambo ya nje wa Tanzania) na Mh. Amina Mohammed (waziri wa mambo ya nje wa Kenya)

Saturday, November 9, 2013

Wazo la leo - Watanzania tujadili hoja za msingi zilizo mbele yetu

Watanzania tuache siasa za maji taka!!!Tujadili hoja za msingi zilizo mbele yetu kama vile elimu, katiba, madini, maliasili, upatikanaji wa maji na umeme nk. Tuache ushabiki wa uNCCR, uCUF, uCCM, uUDP, uCHADEMA nk!!! Tuache kudharirisha watu bila sababu za msingi. Kumbukeni JK ni RAIS tupende au tusipenda! kumdhihaki si jambo zuri hata kidogo. Twende kwenye hoja ya msingi kama mtanzania mmoja mmoja!! kuitana majuha haisaidii. Nitawapa mfano, JK ameonyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa, ameweza kukutana na makundi mbalimbali ya jamii na kisiasa na kusikiliza maoni yao. Hakika JK amewafunda wanasiasa wa Tz kuwa siasa sio fitna, matusi ama kubeza mawazo ya mwenzio bali siasa ni maridhiano, maelewano, upendo, maendeleo, amani bila ya kudharau maoni ya watu hata kama ni wengi ama wachache!! Watanzania hasa vijana badilikeni ili nchi yetu iweze kupiga hatua ya maendeleo. Mimi nimefurahi wakati JK anahutubia bunge majuzi Mwenyekiti na Mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alikuwa akipiga makofi mara kwa mara wakati JK alipokuwa anahutubia. Upigaji makofi ule umeonyesha hata wapinzani wanaunga mkono hoja zinazotolewa na upande wa pili wa shilingi hata kama mtoa hoja yuko chama tawala ama chama kingine! Hali hii ndio watanzania wanayohitaji. Tujadili hoja za msingi kwa watanzania na watanzania watawaunga mkono viongozi hao bila kujali wanatoka upande gani wa shilingi. JK bila kumugunya maneno ameonyesha weledi, ustaarabu, uungwana na ukomavu wa hali ya juu, amejali maslahi ya watanzania wote bila ubaguzi, nendeni youtube ama kwenye mitandao ya kijamii kuangalia hotuba yake hiyo aliyoitoa bungeni hivi karibuni Dodoma. Hakika JK amekuwa kama mwalimu JKN!! Sasa na sisi tufuate nyayo zake na tuache siasa za kuchafuana ambazo hazitatufikisha popote. Tanzania tunataka maendeleo ya kweli na sio malumbano yasiyo na tija. Tanzania kwanza, ubinafsi nyuma!