Wednesday, November 20, 2013

Hongera Mh. Ummy Mwalimu kwa kulinda na kutetea haki za watoto pamoja na kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji

Mh. Ummy Mwalimu leo ameshiriki katika maadhimisho ya siku ya Maombi na Vitendo kwa Watoto, katika viwanja vya Don Bosco mjini Dar es Salaam. Washiriki wengine katika maadhimisho hayo walikuwa Global Network of Religions for Children (GNRC), InterReligious Council of Peace Tanzania (IRCPT) na UNICEF. Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na UN Universal Children's Day. Ambapo KauliMbiu ya Mwaka huu ni "Zuia Ukatili Dhidi ya Watoto". Mh. Ummy alipata fursa ya kuelezea hatua mbalimbali za kisera na kisheria zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya Ukatili dhidi ya watoto. 

Mh. Ummy amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Mtoto imeanza kutekeleza Mpango wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto 2013-2016. Mpango huu umejielekeza katika kuimarisha mifumo ya kisheria katika utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya 2009 na katika kujenga mifumo imara ya ulinzi wa mtoto kwa ajili ya kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili. Mh Ummy ameiomba jamii kwa ujumla kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinakoma. Pia amewaomba wazazi, walezi, viongozi wa dini, watoto na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na kuzingatiwa. 

Hakika blogu hii inampongeza sana Mh. Ummy kwa jitihada anazofanya za kulinda na kutetea haki za watoto pamoja na kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wafanyiwavyo watoto.

Blogu hii inaomba jamii kwa ujumla kushirikiana na Mh Ummy pamoja na serikali kwa ujumla kupinga vitendo vya ukatili wa watoto. Pia jamii kuripoti kwenye vyombo vya dola waonapo uwepo wa vitendo vya ukatili kwa watoto. Blogu hii inaamini kwa kufanya hivyo, vitendo vya unyanyasaji vitapungua ama kwisha kabisa. Pia blogu hii inaomba mkakati wa kupinga unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto uanzie kwenye shule za awali, msingi mpaka sekondari. 

Sio lazima kukawa na mtaala rasmi ila kuna kitu kinaitwa "hidden curriculum" ambapo walimu watapewa maelekezo ama mafunzo ya namna ya kuwaelimisha watoto juu ya HAKI na WAJIBU wao. Baadhi ya nchi zinafanya hivyo, mfano mtoto akinyanyaswa anaelekezwa ama anafundishwa wapi apeleke taarifa hata kama atakayekuwa anamnyanyasa ni mzazi, mlezi ama ndugu. Mbali na kufundishwa HAKI na WAJIBU wao WATOTO pia wafundishwe kwa njia hiyo hiyo UZALENDO, USAFI NA MAZINGIRA, MICHEZO nk ili angalao utupaji wa taka ovyo ukome, rushwa ikome na MATOKEO yake ni baada ya miaka 10 ama 15 taifa litapiga hatua kubwa ya maendeleo!

Viwanja vya Don Bosco mjini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment