Thursday, September 24, 2015

Nchi hii inahitaji mtu kama huyu (Nehemiah Mchechu Mkurugenzi wa NHC)

Hongera Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Ndugu Nehemiah Kyando Mchechu kwa ujenzi wa makazi bora kabisa nchini. Hakika nchi hii inahitaji watu wenye akili, ujasiri na uthubutu kama wewe. Blogu hii inakutakia kila la kheri wewe na manejimenti nzima ya NHC katika ujenzi wa makazi bora. Ombi la blogu hii ni kuomba kwa kadri itakavyowezekana zijengwe nyumba za bei nafuu kwa wananchi wa kawaida. Na pia NHC iangalie uwezekano wa kuwakopesha watumishi wa umma nyumba kwa mikopo ya muda mrefu kama miaka 30+.


Monday, September 14, 2015

Hongera JK kwa kuzindua Taasisi ya MOYO ya Jakaya Kikwete

Picha: Habari leo
Hongera Mh. Dkt. Jakaya Kikwete kwa kuzindua Taasisi ya MOYO ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam. Kupitia Taasisi hii Serikali itakuwa ikiokoa TShs Bilioni 2.5 kwa mwaka kutokana na upelekaji wa wagonjwa nje ya nchi.

Blogu hii inampongeza sana JK na serikali kwa ujumla kupitia wizara ya afya kwa uzinduzi wa taasisi hii ya kisasa ya magonjwa ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki. Blogu hii inaomba jengo na vitendea kazi vitunzwe ili lengo la serikali likamilike. Aidha blogu hii inaishukuru serikali ya China kwa kutoa msaada wa Tshs Bilioni 16.6 katika ujenzi wa jengo la taasisi hii kutokana na jitihada zilizofanywa na Rais Kikwete alipotembelea China na kukutana na Rais Hu Jintao.

Hongera JK kwa kuzindua kampeni ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia UTALII

Picha: Wizara ya Maliasili na Utalii
Hongera Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuzindua kampeni maalum ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia mtandao na kampeni ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Blogu hii inampongeza sana Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyarandu pamoja na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Dkt, Adelhelm Meru na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Utalii. Bi. Devota Mdachi kwa kuandaa mtazamo mpya wa kutangaza vivutio vya Utalii kimataifa.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali, wadau wa uhifadhi pamoja na wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Katika mpango huo vivutio vya utalii vitaonekana katika vituo vya kimataifa kama BBC, CNN nk na hii itachochea sekta ya Utalii nchini.
Blogu hii inaishukuru sana serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuandaa mpango wa kutangaza vivutio vya UTALII nchini. Blogu hii inaomba yafuatayo:

  1. Kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vyombo vya habari vingine hasa majarida na magazeti ya kimataifa;
  2. Kutangaza vivutio kwa watanzania kupitia televisioni za hapa nchini na magazeti ya kila siku (tusisahau utalii kwa watu wa ndani);
  3. Kuimarisha miundombinu kama barabara na viwanja vya ndege nk ili kuchochea utalii nchini.
Kwa habari zaidi bofya hapa.

Hongera Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuahidi kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha miundombinu ya Utalii nchini

Picha:Wizara ya Maliasili na Utalii

Hongera Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuahidi kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha miundombinu ya Utalii nchini kwa kusudi ya kuwavutia watalii wengi zaidi kutembelea vivutio vingi vya utalii vilivyopo Tanzania. Miundombinu kama barabara zimekuwa katika hali mbaya na kukwamisha jitihada za serikali kuongeza watalii nchini.

Akizungumza katika mkutano wa sita wa Uchumi wa Tanzania ulioandaliwa na Benki ya Dunia katika Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, Rais Mstaafu wa Tanzania Mh Benjamini Mkapa alisema ni lazima sekta binafsi ishirikiane na Serikali badala ya Serikali kufanya kila kitu. SERIKALI HAIWEZI KUFANYA KILA KITU HIVYO SEKTA BINAFSI LAZIMA ISHIRIKISHWE KATIKA KUINUA UCHUMI.

Blogu hii imefurahishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ya kukubali kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza sekta hii muhimu nchini kwa ustawi wa taifa letu. Pia blogu hii inawaomba watanzania na hasa wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa hii ili kujipatia kipato na kuinua pato la taifa.

Kwa habari zaidi, bofya hapa.

Saturday, September 12, 2015

Hongera Taifa stars kwa kuionyesha dunia kuwa mnaweza


Picha: Mwananchi.co.tz

Hongera Taifa stars kwa kuonyesha dunia kuwa mnaweza katika mechi kati ya Tanzania "Taifa stars" na Nigeria "Green Eagles" iliyochezwa jijini Dar es Salaam. Mechi hiyo iliyochezwa Septemba 5 2015 kuwania tiketi ya kufuzu AFCON 2017. Hakika wachezaji wamecheza kwa bidii sana wakiongozwa na Mbwana Samatta na Haji Mwinyi. Hakika kila mchezaji ameonyesha kiwango kikubwa. Haikuwa rahisi kuona tofauti ya kiuchezaji kati ya wachezaji wa kulipwa wa Nigeria na wale wanaocheza ligi ya ndani ya Tanzania. Benchi la ufundi nalo linastahili pongezi za dhati likiongozwa na Charles Boniface Mkwassa aka "Master" na Abdallah "King" Kibadeni aka "Mputa". Aidha blogu hii inaipongeza TFF kwa jitihada ilizofanya za kuibadili timu hii. Blogu hii inaomba juhudi hizo ziendelezwe. Pia blogu hii inaiomba serikali izidi kushirikiana na TFF katika kuisaidia timu ya Taifa.