Tuesday, May 27, 2014

Hongera Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuboresha huduma za ndege nchini

Hongera Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuboresha huduma za ndege. Hakika blogu hii imefurahishwa na maboresho ya huduma za ndege hapa nchini. Shirika la ndege katika siku za karibuni limeongeza huduma zake katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania na nje ya nchi. Kwa uchache kuna usafiri wa ndege kupitia ATCL Dar - Mwanza - Dar, Dar - Kigoma - Dar, Dar - Mbeya - Dar, Dar - Mtwara - Dar, Dar - Mbeya - Dar, Dar - Bujumbura - Dar, Arusha - Zanzibar - Arusha nk.

Shirika hili ni la taifa, hivyo basi kama wazalendo wa nchi hii hatuna budi kuipongeza serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Uchukuzi Mh Dr. Harrison Mwakyembe kwa juhudi za kuboresha huduma na usafiri kupitia shirika letu la taifa. Pia blogu hii inawapongeza manejimenti na wafanyakazi wa ATCL kwa ujumla kwa juhudi wazifanyazo ambazo zimeonyesha matunda haya. Tanzania ni nchi kubwa na inastahili kuwa na shirika bora la umma la ndege. Si ni a ya blogu hii kuonyesha mafanikio ya mashirika ya ndege ya nchi nyingine barani Afrika BALI Tanzania tunapaswa kuwafikia na kuwazidi wengine (nchi nyingine za Afrika). Kwa habari zaidi tembelea ATCL ili ujionee mwenyewe. Mwenye MACHO AAMBIWI TAZAMA.

Picha: http://www.mwananchi.co.tz

Thursday, May 22, 2014

Hongera serikali kwa kujali njia za mchepuko katika kupunguza msongamano magari jijini Dar es Salaam

Hongera Wizara ya Ujenzi kwa kutenga jumla ya Tshs 28.94 bilioni kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara za mchepuko ili kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam. Pia blogu hii inapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi John Pombe Magufuli kwa utendaji uliotukuka wa ujenzi wa barabara ndani ya jiji la Dar es Salaam na nchini kwa ujumla. Kiasi cha Tshs 28.94 bilioni zitatumika katika kupanua baadhi ya barabara, kukarabati baadhi ya barabara na kujenga barabara mpya kwa kiwango cha lami jijini Dar es Salaam. Hakika blogu hii imefurahishwa na hatua hii ya serikali ya kuhakikisha inapunguza msingamano wa magari katika njia kuu za magari jijini Dar es Salaam. Msongamano wa magari jijini Dar es Salaam licha ya kuwafanya wakazi jiji la Dar es Salaam kupoteza muda mwingi barabarani bali Taifa linapoteza pato kubwa.

Blogu hii inaomba hatua hii nzuri ya serikali isihishie katika barabara kumi bali iendelee kwa barabara nyingine kama vile barabara toka Mwananyamala Hospitali kuelekea kituo kipya cha daladala cha Makumbusho kuelekea Mwenge kupitia nyuma ya Jengo la Sayansi "COSTECH" mpaka makutano ya barabara ya Shekilango. Blogu hii ingependa mara barabara hii ikikamilika basi magari toka Mwananyamala Hospital mpaka Mwenge yapite njia hiyo ili kupunguza msongamano. 

Pia blogu hii inaomba hatua hii isiishie Dar es Salaam pekee bali hata mikoa mingine kama vile Arusha, Mwanza, Tanga, Mbeya nk inahitaji njia za michepuko ili kukabiliana na msongamano wa magari siku za usoni. Kwa habari zaidi soma mwananchi.

Picha:globalpublishers.info

Thursday, May 15, 2014

Hongera SSRA kwa kuenzi lugha ya KISWAHILI, taasisi na makampuni mengine yaige mfano huo



Hongera Social Security Regulatory Authority (SSRA) kuwa miongoni mwa taasisi za umma ambazo tovuti (website) yake iko kwa lugha ya taifa ya KISWAHILI. Lugha ya KISWAHILI ndiyo lugha inayoeleweka kwa watanzania wengi. Mara nyingi watanzania tumekuwa na utamaduni wa kutumia lugha ya kiingereza hata pale tunapojua kwa hakika watumiaji wa taarifa zetu ni waswahili wanao jua Kiswahili vizuri. Pia, yapo makampuni ambayo yanatangaza bidhaa mbalimbali nchini lakini bado wanatumia lugha ya kiingereza! Aidha, tovuti nyingi hapa nchini bado zinatumia lugha ya kigeni wakati wasomaji na wafuatiliaji wake ni waswahili wa kitanzania. 


Blogu hii haina maana ina dharau matumizi ya kiingereza LA HASHA ila ni vyema kama habari ina walenga waswahili wa kitanzania ambao kwa hakika wanajua na kutumia lugha ya kiswahili vizuri kuliko kiingereza ni vyema taasisi ama makampuni kutumia lugha ya Kiswahili kwa faida ya wengi.


Blogu hii imefurahishwa na jinsi taasisi hii ya SSRA ilivyoweza kuenzi lugha adhimu ya Kiswahili na kuwajali watanzania. Na pia blogu hii imefurahishwa na  jinsi walivyoweka kiunganishi (link) kingine kwa wanaopenda kutumia lugha ya kiingereza. Blogu hii inashauri taasisi zingine na hasa za umma kuiga mfano wa taasisi hii ya SSRA ya kuenzi lugha ya Kiswahili kwa ajili ya watanzania. Tembele tovuti ya SSRA ujionee mwenyewe!

Picha: ukurasa wa mbele wa tovuti ya SSRA