Friday, May 2, 2014

Pongezi serikali kwa kufikiria kupunguza kodi kwa wafanyakazi kuwa chini ya aslimia 10



Mojawapo ya taarifa zilizowafurahisha wafanyakazi hapa nchini ni uamuzi wa wa serikali ya Tanzania kuwapunguzia wafanyakazi kodi wanayotozwa kila mwezi kwenye mishahara yao. Makato ya kodi mpaka sasa kwenye mishahara ya wafanyakazi ni asilimia 13. Kuna uwezekano mkubwa kwa kodi hii kupungua na kuwa chini ya asilimia 10.
Katika siku ya MEI MOSI jijini Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete aliliambia taifa kuwa utekelezaji wa kupunguza kodi utaanza baada ya kupitishwa kwa bajeti ya mwaka ujao. Lengo kuu likiwa ni kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa kodi na kuwapa unafuu wa maisha.

Hakika blogu hii imefurahishwa na hatua ya serikali kupitia kwa Mh Rais Jakaya Kikwete kupunguza kodi kwa wafanyakazi. Wafanyakazi wa Tanzania wanakabiliwa na changamoto za maisha hivyo kwa kuwapunguzia kodi ya PAYE (Pay as You Earn) kutawawezesha wafanyakazi kupata nafuu katika maisha yao ya kila siku. Baadhi ya wafanyakazi kama vile walimu watafaidika sana na punguzo hili, hali hii itaongeza motisha katika utendaji wao wa kazi na matokeo yake watoto wetu watapata elimu bora kupitia kwa walimu wenye motisha.

Aidha blogu hii bado inaipongeza serikali kwa hatua zake za kupunguza kodi hii mwaka hadi mwaka. Mfano mwaka 2007, kodi hii ilikuwa kiasi cha asilimia 18 na ikashuka na kufika asilimia 13. Sasa kuna uwezekano kodi kuwa chini ya asilimia 10.Ni matumaini ya blogu hii punguzo hili la kodi kwa wafanyakazi litafidiwa na serikali kupitia vyanzo vingine ili uchumi wa nchi usiyumbe. 

Mwisho, blogu hii inawaomba wafanyakazi na hasa walimu kujiunga katika vikundi kama vile saccos, vikoba nk ili kuinua vipatao vyao kwa maana hakuna mshahara unaotosha!! Kwenye vikoba na saccos wanaweza kupata manufaa mengi sana ikiwemo kuwa na uwezo wa kujenga nyumba za kuishi.

Picha: fullshangweblog.com
  

Picha: farmlandgrab.org

No comments:

Post a Comment