Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania imesema iko mbioni kushusha bei ya umeme nchini mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mh. Stephen Masele jana ndani ya ukumbi wa Bunge wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mh. Martha Mlata. Naibu Waziri aliwaomba wananchi kuvuta subira kwani mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia kati ya 80 na 90.
Aidha Naibu Waziri amesema kwa sasa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) linanunua umeme kutoka kwa makampuni yanayofufua umeme kwa gharama za uniti moja kwa senti za dola za kimarekani 38 mpaka 55. Wakati ambapo TANESCO inawauzia wateja wake uniti moja kati ya senti za dola za kimarekani 10 mpaka 19. Hii inaifanya TANESCO kupata hasara kubwa.
Naibu Waziri amesema mara baada ya kukamilika kwa mradi wa Bomba la Gesi toka Mtwara mpaka Dar es Salaam, TANESCO wana uwezo wa kuwauzia wateja wake uniti moja kwa senti 8 hadi 9 za kimarekani.
Hakika blogu hii imefurahishwa na kauli hii ya serikali ya kufikiria kupunguza gharama za umeme kwa wananchi. Hii itachochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Aidha nafuu hii itachochea wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuongezeka. Pia hii itaokoa ukataji miti ovyo kwa ajili ya kutengenezea mkaa na hivyo kutunza mazingira.
Blogu hii inashauri kwa kuwa kuna neema inakuja ni vyema serikali kupitia TANESCO na Wakala wa Umeme Vijijini kuongeza kasi ya kuwafungia wananchi wengi umeme. Kwa habari zaidi soma Habari Leo.
Picha:simbadeo
No comments:
Post a Comment