Sunday, November 30, 2014

Pole na karibu Rais Mh Jakaya Mrisho Kikwete toka nchini Marekani

jk3
Picha:dewjiblog.com

Blogu hii inapenda kukupa pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Jakaya Mrisho Kikwete kwa kurudi salama Tanzania toka Marekani ulipokuwa unashughulikia afya yako. Afya yako ni afya ya watanzania wote. Blogu hii imeona ni busara kukupa pole kwa niaba ya watanzania na kukukaribisha tena ili kuzidi kuwaletea maendeleo wananchi.


Blogu hii imefurahishwa na ujasiri wa kuelezea afya yako kwa wananchi siku ya Jumamosi tarehe 29 mwaka 2014 ulipowasili toka nchini Marekani. Hakika umetufundisha somo la kupima afya zetu mara kwa mara ili kubaini tatizo mapema. Somo hili hasa la kupima afya mara kwa mara ni muhimu ukizingatia watanzania kutokuwa na utamaduni huo hata kama kuna fursa ya huduma za afya.  Pole sana Rais wetu na karibu nchini uzidi kuwaletea wananchi maendeleo.

Hongera Mh Mizengo Pinda kwa busara, subira na uvumilivu wakati wa mjadala wa sakata la Tegeta ESCROW ndani ya Bunge

Image result for pinda mizengo
Kwa namna ya pekee blogu hii inampongeza Waziri Mkuu “mtoto wa mkulima” Mh. Mizengo Pinda kwa busara, heshima, ustahimilifu na subira juu ya Sakata la “account” ya Tegeta ESCROW. Hakika umetufundisha kitu katika sakata hili na kudhihilisha kuwa uongozi ni kujali maslahi mapana ya wananchi na siyo vinginevyo. 

Blogu hii inakupongeza kwa jinsi ulivyotoa maneno ya kuwaunganisha watanzania wakati wa kufunga Bunge jumamosi tarehe 29 mwaka 2014. Ustahimilifu, subira, heshima, busara uliyoonyesha ni SIFA ya KIONGOZI MKUU. Hakika SIFA hizo unazo. Pia blogu hii imependa kauli zako ikiwemo “Yaliyopita si ndwele tungange na yajayo”, ni kauli nzuri kwa ustawi wa taifa lolote.

Ni matumaini ya blogu hii na watanzania kuwa mapendekezo ya wabunge wetu wote juu ya sakata hili yatafanyiwa kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa chini ya UONGOZI WAKO. Blogu hii imejionea kuwa kauli zako katika suala hili ni za kuwaunganisha watanzania. Aidha ahadi ulizotoa zimewafuta machozi watanzania wote bila kujali itikadi zao.

Hongera wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia sakata la Tegeta ESCROW

Picha: thehabari.com

Hongera wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi mlivyosimamia suala zito la Sakata la “account” ya Tegeta ESCROW. Blogu hii inaamini suala hili lilikuwa nyeti, gumu na lililokuwa linagusa nyoyo za watanzania. Ni suala ambalo lilikuwa na majibu mawili moja kujenga ama kubomoa taifa. Hakika wabunge wote mmerudisha imani kwa wananchi wa nchi hii kwa kuweka mbele maslahi mapana ya nchi yetu. Wabunge mmetukumbusha kuwa uongozi ni dhamana, uongozi ni uadilifu, uongozi ni uwajibikaji, uongozi ni ukweli. Kiongozi asiye mkweli ni tatizo, kiongozi asiye mwadilifu ni tatizo. 

Blogu hii inaomba kuwataja wabunge wachache kwa niaba ya wabunge wote kwa jinsi walivyosaidia kuwatetea na kuwaunganisha watanzania, Mh Zitto Zuberi Kabwe, Mh Deo Filikunjombe, Mh Mwigulu Nchemba, Mh David Kafulila, Mh James Mbatia, Mh Ole Sendeka, Mh Dr Hamisi Kingwangala, Mh William Lukuvi, Mh Freeman Mbowe, Mh Kangi Lugola, Mh Stephen Wasira, Mh John Mnyika nk.  

Blogu hii inaomba mwelekeo huu uendelee hata katika masuala mengine ya kitaifa, na bila kusahau wajibu wenu wa kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali ili ilete maendeleo ya kweli kwa wananchi wake. Hakika siku ya Jumamosi tarehe 29 mwaka 2014 ni siku ya kukumbukwa kwa taifa letu. Mwenyezi MUNGU awabariki WABUNGE wote wa BUNGE hili kwa kutenda HAKI na KUWABEBA WATANZANIA.

Hongera kamati ya PAC chini ya Mh Zitto na Mh Filikunjombe juu ya sakata la Tegeta ESCROW

Image result for zitto kabweImage result for filikunjombe
Hongera Mh. Zitto Kabwe na Mh. Deo Filikunjombe pamoja na wajumbe wote wa kamati ya “PAC”. Hakika mmewatendea haki watanzania katika kipindi chote cha uchunguzi, uchambuzi na uwasilishwaji wa maadhimio yaliyohitimishwa Jumamosi tarehe 29 mwaka 2014. 

Sakata la “account” ya Tegeta ESCROW halikuwa jambo dogo. Uimara na umahili wenu kwa kusaidiana na wajumbe wote wa PAC umewafuta machozi watanzania bila kujali itikadi ya vyama. Kamati yenu, imetukumbusha kuwa “cheo ni dhamana”, imetukumbusha “cheo siyo dharau”, imetukumbusha “uongozi ni uadilifu, ukweli, kutenda haki na uaminifu.  

Kazi yenu imeleta heshima ya nchi yetu, na kurudisha imani kwa watanzania kupitia wawakilishi wao. Aidha mmesaidia kuokoa rasilimali za nchi hii kwa wakati huu na kwa miaka ijayo, mmedumisha nidhamu kwa wote hususan watendaji na viongozi. 

Blogu hii inawapongeza sana, Mwenyezi Mungu Awabariki Sana. Blogu hii inapendekeza nchi yetu itilie mkazo suala la MAADILI siyo kwa viongozi wa umma pekee ila hata kwa watendaji wote ikiwemo sekta binafsi. 

Kuwepo na vyombo vya kuhakikisha nidhamu inakuwepo kwa watu wote. Blogu hii inafurahi uwepo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa “PCCB”, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali “CAG”, Ofisi ya Maadili nk. Blogu hii inaomba vyombo hivi vipewe nguvu na nyenzo zaidi kikatiba ili kulinda maslahi ya Taifa letu. Kazi ya kwanza kwa vyombo hivi na vingine ikiwemo Polisi, Usalama wa Taifa ni kulinda maslahi ya nchi yetu ikiwemo ya kiuchumi pamoja na rasilimali za nchi. 

Kuna haja ya vyombo hivi na vingine vikafanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi wa kimaadili, usalama na uzalendo. Suala la usalama ni pamoja na ulinzi wa rasilimali za Taifa ikiwemo pesa za serikali na walipa kodi. 

Hongera Mh. Mama Anne Semamba Makinda kwa KUWABEBA WATANZANIA kwa kusimamia sakata la Tegeta ESCROW

Image result for anna makinda
Hongera Mh. Mama Anne Semamba Makinda kwa uongozi uliotukuka katika kusimamia sakata la Tegeta ESCROW. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo! Ubunifu wako wa maridhiano, subira, heshima kwa wote, watanzania wameiona. Mama Makinda, blogu hii ya “tuijengetanzania” inatoa pongezi za dhati kwa jinsi ulivyosimamia na kuendesha Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, hususan katika sakata hili na kuweza kuhitimisha maadhimio ya Bunge zima siku muhimu ya Jumamosi tarehe 29 mwaka 2014. 

Kukubali kwako kuiamini na kuipa kazi kamati ya “PAC” chini ya Mh. Zitto Kabwe na Mh. Deo Filikunjombe kumeleta matumaini mapya kwa watanzania. Pia uongozi wako uliotukuka umewatendea haki watanzania wote. Hakika umetufundisha kazi ya Bunge ni kuisimamia na kuishauri serikali na siyo vinginevyo. Umetukumbusha kazi ya wabunge ni ya wananchi na pia umetukumbusha wananchi wanawategemea wabunge wao ambao ni wawakilishi wao. 

Pia umetukumbusha msemo wakati wa Mwalimu Nyerere usemao “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwisho”. Kazi uliyoifanya siyo imeongeza sifa ya Bunge letu tukufu bali pia imelinda rasilimali za nchi hii sasa na siku za usoni. Umetukumbusha MAADILI kuwa ni jambo muhimu katika kuwaletea maendeleo wananchi. Blogu hii inakuomba kupitia Bunge lako Tukufu kuhakikisha suala la MAADILI kwa wote (viongozi, watendaji na wananchi) linatiliwa mkazo na kunakuwa na vyombo vya kulazimisha watu wafuate maadili mema. Vyombo kama polisi, usalama wa taifa, CAG, PCCP na vinginevyo kufanya kazi na kuwapeleka wahusika pasipo kusubiri Bunge kujadili tuhuma. Kwa maneno mengine tuhuma hizi zinatakiwa kumalizwa na vyombo hivi na nchi kuwa salama.

Suala la maadili ni pana na si kwa viongozi pekee, ni suala hata mitaani watu wanapaswa kuwa waadilifu katika mambo mengi sana mfano kuna tabia ya watu wadogo mitaani kutukana matusi bila kuogopa wala kuchukuliwa hatua yoyote, kuna vitendo vya unyanyasaji wa watoto wadogo toka kwa ama wazazi, walezi ama watu wazima, kuna rushwa ndogo ndogo, kuna watendaji wa chini kutotimiza wajibu wao mfano mzuri uwepo wa uchafu katika mitaa tunayoishi, hapa ni kuwa kuna ukosefu wa maadili hata kwa watu wa chini.

Pia suala la MAADILI lipelekwe kwenye shule zetu tokea chekechea mpaka Vyuo Vikuu. Watoto wafundishwe haki, usawa, utu, kukataa rushwa nk tangia wakiwa wadogo. Mitaala yetu pamoja na mambo mengine ijikite katika maadili. Sifa ya kiongozi na mwananchi iwe UADILIFU. 

Kuna wakati mdau wa blogu hii aliwahi kutembelea nchini Sweden, huko alikutana na jambo dogo lakini kubwa kimaadili, kuna mtoto wa shule moja ya msingi alichukuwa kalamu ya rafiki yake shuleni kwa bahati mbaya, alipofika nyumbani na kubaini amechukua kalamu ya mwenziye, alimshauri baba yake ampeleke nyumbani kwa rafiki yake ili amrudishie kalamu yake, baba yule akasema utampa kesho, mtoto yule hakufurahi! Nini maana yake? Ni kuwa suala la MAADILI linaanzia shuleni, linaanzia tokea utoto, linajengwa tangu awali.

Blogu hii inaamini kuwa maendeleo ya kweli yatakuja kwa kila mmoja kuwa na maadili mema apende asipende. Hakika blogu hii inakutakia maisha marefu katika utumishi wako uliotukuka. Hakika nani kama Mama, hakuna. Asante Mama Anne Semamba Makinda kwa KUWABEBA WATANZANIA, MWENYEZI MUNGU AKUBARIKI HAPA DUNIANI NA HATA MILELE AMINA


Monday, November 17, 2014

Hongera Wizara ya Ujenzi kwa kuleta kivuko kitakachotoa huduma kati ya Bagamoyo hadi Dar es Salaam

Hongera Wizara ya Ujenzi, hususan waziri wake Mchapakazi Mh Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi na kuleta kivuko kitakachotoa huduma ya usafiri kati ya Bagamoyo hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam kupitia mwambao wa bahari ya hindi. Pongezi za jumla ziende kwa serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutimiza ahadi ya kufanikisha ujio wa kivuko hiki muhimu. Aidha, blogu hii inaipongeza TEMESA "Wakala wa Ufundi na Umeme" kwa kufanikisha jambo hili muhimu kwa wananchi wakazi wa Dar es Salaam na Bagamoyo. 

Huduma ya kivuko (Mv Dar es Salaam) hiki kitapunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, hususan wale watokao Bagamoyo kupitia mwambao wa Bahari ya Hindi hadi katikati ya jiji. Kivuko hiki kitawasaidia wakazi wa Bagamoyo, Bunju, Tegeta, Boko, Kunduchi nk kuwahi kufika katikati ya jiji la Dar es Salaam na kuokoa muda mwingi unaopotea.

Kivuko hiki ni muendelezo wa juhudi za Wizara ya Ujenzi kupitia kwa Mh. Magufuli katika kupunguza msongamano ndani ya jiji la Dar es Salaam kama vile ujenzi wa barabara ya New Bagamoyo toka kwenye makutano ya barabara ya Kawawa kwenda Tegeta, miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT), njia za juu makutano ya Tazara na Ubungo, barabara pete "Dar es Salaam Outer Ring Roads", barabara ya Dar es Salaam kwenda Chalinze "Express way", upanuzi wa barabara ya lami sehemu ya Gerezani pamoja na ujenzi wa daraja la Kigamboni.

Blogu hii inaomba mamlaka itakayokuwa inasimamia kivuko hiki kujitahidi kukitunza ili malengo yaliyokusudiwa yatimie. Pia Blogu hii inazidi kuiomba serikali pamoja na Wizara ya Ujenzi kununua kivuko kingine. Lengo la kununua kivuko kingine ni kuwa wakati kivuko kimoja kinatoka Bagamoyo basi kuwe na kingine kinachotoka Dar es Salaam kwa wakati huo huo ili wananchi wasisubiri kivuko kwa muda mrefu.

Picha: Michuzi Blog