Hongera Mh. Zitto Kabwe na
Mh. Deo Filikunjombe pamoja na wajumbe wote wa kamati ya “PAC”. Hakika mmewatendea
haki watanzania katika kipindi chote cha uchunguzi, uchambuzi na uwasilishwaji
wa maadhimio yaliyohitimishwa Jumamosi tarehe 29 mwaka 2014.
Sakata la
“account” ya Tegeta ESCROW halikuwa jambo dogo. Uimara na umahili
wenu kwa kusaidiana na wajumbe wote wa PAC umewafuta machozi watanzania bila
kujali itikadi ya vyama. Kamati yenu, imetukumbusha kuwa “cheo ni dhamana”,
imetukumbusha “cheo siyo dharau”, imetukumbusha “uongozi ni uadilifu, ukweli,
kutenda haki na uaminifu.
Kazi yenu
imeleta heshima ya nchi yetu, na kurudisha imani kwa watanzania kupitia
wawakilishi wao. Aidha mmesaidia kuokoa rasilimali za nchi hii kwa wakati huu na kwa miaka ijayo,
mmedumisha nidhamu kwa wote hususan watendaji na viongozi.
Blogu
hii inawapongeza sana, Mwenyezi Mungu Awabariki Sana. Blogu hii inapendekeza nchi yetu
itilie mkazo suala la MAADILI siyo kwa viongozi wa umma pekee ila hata kwa watendaji
wote ikiwemo sekta binafsi.
Kuwepo na vyombo vya kuhakikisha nidhamu inakuwepo
kwa watu wote. Blogu hii inafurahi uwepo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa “PCCB”, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali “CAG”, Ofisi ya Maadili
nk. Blogu hii inaomba vyombo hivi vipewe nguvu na nyenzo zaidi kikatiba ili
kulinda maslahi ya Taifa letu. Kazi ya kwanza kwa vyombo hivi na vingine ikiwemo
Polisi, Usalama wa Taifa ni kulinda maslahi ya nchi yetu ikiwemo ya kiuchumi
pamoja na rasilimali za nchi.
Kuna haja ya vyombo hivi na vingine vikafanya
kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi wa kimaadili, usalama na uzalendo.
Suala la usalama ni pamoja na ulinzi wa rasilimali za Taifa ikiwemo pesa za
serikali na walipa kodi.
No comments:
Post a Comment