Tuesday, March 25, 2014

Hongera Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kutangaza mauzo ya nyumba 214 Mwongozo, Kigamboni jijini Dar es Salaam

Hongera Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kutangaza mauzo ya nyumba 214 Mwongozo, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena leo Jumanne, Machi 25, 2014 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewatangazia wananchi mauzo ya nyumba 214 zinazojengwa eneo la Mwongozo, Kigamboni Jijini Dar es salaam. Maelezo hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara, Bw. David Shambwe kwenye kikao na waandishi mbalimbali wa habari nchini. 

Hakika blogu hii imefurahishwa na juhudi za shirika hili la umma la kuwapatia wananchi wa Tanzania maisha bora kupitia ujenzi wa nyumba bora. Blogu hii inapenda kuliomba shirika hili liongeze kasi ya ujengaji, uuzaji na ukodishaji nyumba kwa ajili ya watanzania.Hakika blogu hii inapendezwa na uongozi imara wa Shirika hili la umma.

Pia blogu hii inaomba shirika la nyumba liende kwenye taasisi za binafsi na serikali na kuingia mikataba ya muda mrefu na wafanyakazi kupitia waajiri wao ili wananchi wengi waweze kupata nyumba bora za kuishi. Mfano, kuna wafanyakazi wa serikali ambao wana umri wa miaka 25 na ambao wanaweza kuingia mkataba na shirika la nyumba kwa miaka hata 35 kwa kukatwa asilimia fulani kwenye mshahara wakati huo huo mhusika akiwa kwenye nyumba yake tayari. Hii ni faida kubwa kwa mfanyakazi wa umma ama wa binafsi maana hata kama atakuwa hajamaliza mkopo bado atakuwa anaishi kwenye nyumba hiyo kana kwamba analipa kodi kwa kiasi kidogo. 

Kwa habari zaidi kuhusu taarifa hii na kwa mtanzania anayetaka nyumba hizi, Tembelea link hii ya Shirka la Nyumba la Taifa (NHC) kwa maelezo zaidi.


Picha: http://www.nhctz.com/mwongozo/

Monday, March 24, 2014

Hongera kampuni ya simu ya Tigo kwa kutoa msaada wa vitabu vya wanafunzi katika Shule ya Msingi Kilimani

Hongera kampuni ya simu ya Tigo kwa kutoa msaada wa vitabu vya wanafunzi wa darasa la saba na nne katika Shule ya Msingi Kilimani wenye thamani ya shilingi za kitanzania milioni sita. Aidha, meneja wa Huduma za Kijamii kutoka Tigo, Woinde Shisael alisisitiza kuwa kampuni hiyo ya Tigo inatambua umuhimu wa elimu kama mojawapo ya kiungo katika kuchangia mabadiliko ndani ya jamii ama Taifa. Hakika, huo ni ukweli mtupu.

Vile vile kwa kupitia wafanyakazi wa Tigo shule hiyo ilikabidhiwa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita takribani elfu nne za maji. Tenki hilo lina thamani ya shilingi za kitanzania laki sita na elfu hamsini na tatu.

Hakika blogu hii imefurahishwa na juhudi za kampuni hii ya simu za mkononi kwa kutambua mchango wa elimu katika taifa letu. Pia blogu hii imefurahishwa na wafanyakazi wa kampuni hii ya simu ya Tigo kwa kutoa msaada muhimu wa tenki la maji kwa shule hiyo. Blogu hii inawaomba Tigo kuendelea kuwasaidia watanzania kwa njia mbali mbali na hasa kwa kupitia sekta ya elimu. Elimu ni kila kitu kwa binadamu yoyoye. Waswahili wanasema "elimu ni ufunguo wa maisha". Hivyo kwa Tigo kutoa mchango wa aina hiyo wameweza kuchochea maendeleo ya elimu nchini. Asante Tigo!

Blogu hii imeona ni vyema kuwaunganisha wadau wake na Tigo kama ni namna mojawapo ya kukubali juhudi zao kwa watanzania! 

Aidha blogu hii inayaomba makampuni mengine kuiga mfano mzuri wa Tigo katika kuchangia maendeleo ya nchi na wananchi hasa kupitia sekta ya elimu. Kwa habari zaidi bofya hapa.


Picha:en.wikipedia.org

Thursday, March 20, 2014

Hongera Rose Ndauka kwa kuanzisha kampeni ya usafi nchini Tanzania.

Hongera Rose Ndauka kwa kuanzisha kampeni ya usafi nchini Tanzania. Rose Ndauka ni msanii wa filamu nchini Tanzania. Hivi karibuni Rose akiwa na wasanii wenzake walifanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Mnazi Mmoja ndani ya jiji la Dar es Salaam. Aidha msanii huyo amezindua kampeni ya usafi iitwayo 'Amka Badilika, Nga'risha Tanzania'.

Hakika blogu hii imefurahishwa na kitendo cha kuanzisha kampeni ya usafi nchini pamoja na kufanya usafi kivitendo.

Jiji la Dar es Salaam pamoja na majiji na halmashauri zingine nchini zinakabiliwa na changamoto ya usafi. Jukumu la kuhakikisha usafi katika majiji ama manispaa ama halmashauri liko mikononi mwa taasisi husika pamoja na wadau wengine wakiwemo wananchi kama msanii Rose Ndauka alivyofanya.

Blogu hii inaomba majiji, manispaa na halamashauri nchini zimpe Rose ushirikiano unaostahili katika kufanikisha azma yake ya usafi. Pia ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira itoe ushirikiano wa dhati juu ya juhudi zozote zinazofanywa na wadau kama Rose Ndauka.

Vile vile blogu hii inaomba majiji, manispaa na halmashauri zihakikishe maeneo yao yanakuwa safi muda wote. Kuyafanya majiji ama manispaa ama halmashauri kuwa safi ni jambo linalowezekana. Taasisi hizi zinapaswa kutenga fedha za kodi kwa kiasi fulani ili kuhakikisha maeneo yote yanakuwa safi. Pia kuna by-laws ambazo majiji ama manispaa kupitia kata husika wanaweza kuzitekeleza ili kulazimisha watu na jamii zifuate kanuni ya usafi. Mfano mtu akitupa taka ovyo hata kama ni ganda la embe by-laws ziko wazi achukuliwe hatua papo hapo. Vile vile katika maeneo ama nyumba za watu ama vituo vya daladala kuwe na vyombo vya uchafu ili watu waweze kutupa taka taka. Magari ya abiria kama dala dala yawe masafi na kuwa na vyombo vya kuhifadhia uchafu. 

Pia askari mgambo wa majiji, manispaa ama halmashauri wapewe mafunzo mazuri ili kusimamia zoezi la usafi nchini Tanzania.

Taasisi husika kama vile majiji, manispaa na halmashauri zinaweza pia kuanzisha miradi ya kutumia taka kuzalisha gesi ama umeme. Na pia taka zingine zinaweza kubadilishwa na kutumiwa tena kama bidhaa. Baadhi ya nchi kwa mfano wanatumia taka kuzalisha umeme ambao unaingizwa kwenye gridi ili kuwapa wananchi wake umeme. Hivyo blogu hii inaamini usafi ni jambo linalowezekana na pia ni sekta ambayo ikitumiwa vizuri itaajiri vijana wengi na kutoa faida zingine kama vile gesi na umeme. Ni jukumu la taasisi husika zikafanyia kazi masuala haya ili kufanikisha usafi katika mazingira yetu.

Falsafa ambayo mdau wa blogu hii aliipata nje ya nchi hii ni kuwa ukitaka kufanikisha usafi katika eneo lolote ni lazima "utumie uchafu kama fursa". Nini maana yake? Uchafu upo! Ila unatakiwa kuratibiwa. Mfano mabaki ya chakula yakikusanywa toka majumbani yanaweza kutumika kutoa gesi ama mbolea.Gesi ama mbolea itokanayo na taka inaleta faida kwenye uchumi wa nchi na mtu moja mmoja pia.

Blogu hii inaamini USAFI nchini UNAWEZEKANA kama WADAU wote kwa ujumla watashirikiana kikamilifu.

Kwa habari zaidi na picha bofya hapa.

Picha: http://pro-24.blogspot.com
Rose Ndauka akiwa na Meya wa Ilala, Jerry Slaa pamoja na wanafunzi na wasanii wenzake wakifanya usafi katika eneo la Mnazi Mmoja ikiwa ni kampeni ya kufanya usafi jiji zima la Dar es Salaam

Friday, March 14, 2014

Wazo la serikali la kuwa na mfumo wa bei elekezi wa ada kwa shule za msingi na sekondari ni zuri sana!

Wazo la kuwa na mfumo wa bei elekezi wa ada kwa shule za msingi na sekondari ni zuri sana. Wazo hilo limesemwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dr Shukuru Kawambwa wakati alipokuwa akizindua mfumo wa ada elekezi kwa vyuo vya Elimu ya Juu nchini.

Hakika, blogu hii imefurahishwa na hatua hiyo ya serikali kwa kuwa itaboresha sekta ya elimu nchini. Bei elekezi ya ada inakokotolewa kitaalamu kwa kuweka gharama zote za uendeshaji chuo ama shule. Hii itatoa unafuu kwa wazazi ama taasisi zinazofadhili wanafunzi kwa maana ya kuwa na gharama za ukweli hata kama zitakuwa juu. Hii itapelekea ubora wa elimu kuongezeka kwa maana kama ada itajumuisha matumizi ya maabara na kemikali katika ufundishaji kivitendo basi mwanafunzi atatarajiwa kupata elimu ya kiwango hicho na siyo vinginevyo. 

Kuhusu wazo la kuwa na ada elekezi kwa shule za msingi na sekondari ni kuwa suala hili ni la msingi sana. Baadhi ya shule za msingi nchini kwetu zimekuwa na kasumba ya kupandisha ada kiholela kwa sababu zisizo za kitaalamu. Zipo shule za msingi ambapo ada kwa mwaka kwa mwanafunzi mmoja inazidi ada ya mwanafunzi kwa ngazi ya shahada ama stashahada kwa baadhi vyuo nchini. Hii HAIKUBALIKI! na sio KWELI!

Mbali na kuipongeza serikali kwa kuwa na wazo zuri sana la kuwa na ada elekezi, Blogu hii inaishauri serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuanzisha taasisi ama "agency" ya serikali itakayosimamia viwango hivi vya ada elekezi. Kwa maneno mengine kuwe na "regulator" ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kulingana na ada inayolipwa. Bila ya kuwa na "regulator" suala hili licha ya kuwa zuri utekelezaji wake utakuwa na walakini. Taasisi hii itakayoanzishwa inaweza pia hata kuhusika na masuala ya UKAGUZI wa shule ili Wizara ibaki kama msimamizi mkuu wa elimu kisera.
 
Waziri wa Elimu Dr Shukuru Kawambwa wakati wa uzinduzi wa kituo kiitwacho "Teachers Professional Center" DUCE tarehe 23 oktoba 2013. Katikati ni Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Gharib Bilal

Wednesday, March 12, 2014

Hongera sana Mhe Samwel Sitta kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba

Hongera sana Mhe Samwel Sitta kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba. Mhe. Sitta ameshinda kwa kupata kura nyingi dhidi ya mpinzani wake Mhe Hashim Rungwe katika uchaguzi huo. Ushindi wa Mhe Sitta ni mkubwa kwa maana amepata zaidi ya asilimia 80% ya kura zote zilizopigwa na wajumbe wa Bunge la Katiba. 

Hakika blogu hii inampongeza sana Mhe Sitta kwa ushindi huo mkubwa. Wajumbe wa Bunge la Katiba bila kujali itikadi za kisiasa na siasa za makundi wamekuwa na imani na Mhe Sitta. Aidha blogu hii inawapongeza wajumbe wote kwa kumchagua Mhe Sitta kuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Blogu hii inaamini chini ya Mhe Sitta, Bunge hili litaendeshwa vizuri na kufanikiwa kupitisha rasimu ya katiba ambayo itapelekwa kwa wanachi kupigiwa kura.

Mchakato huu wa upatikanaji katiba mpya ni muhimu sana kwa taifa letu. Hivyo kupatikana kwa Mhe Sitta kunatoa imani kwa wananchi wa nchi hii kuwa mchakato katika hatua hii utaenda vizuri. 


Picha: Sundayshomari.com

Wednesday, March 5, 2014

Hongera Bi Jane Magigita kwa kutunukiwa tuzo ya haki ya mwaka 2014 ya Dr Martin Luther King

Hongera Bi Jane Magigita kwa kutunukiwa tuzo ya haki ya mwaka 2014 ya Dr Martin Luther King baada ya mchango wako wa kutetea haki za kisheria za wanawake kutambuliwa. Kwa sasa Bi Jane ni mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali iitwayo "Equality for Growth". Bi Jane ametunukiwa tuzo hiyo na kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Virginia Blaser.

Bi Jane ametunukiwa tuzo hiyo kwa juhudi zake za kutetea haki za wanawake hususan katika kupinga ukatili wa kijinsia, matatizo ya urithi na matumizi ya ardhi.

Blogu hii inampongeza sana Bi Jane kwa kupata tuzo hii. Tuzo hii imeifanya dunia kutambua mchango wake kwa kuwasaidia wanawake maskini nchini Tanzania. Tuzo hii pia imeifungua Tanzania katika uso wa dunia kuwa ni nchi inayokabiliana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

Blogu hii inamuomba Bi Jane aendelee katika juhudi zake za  kuwapigania wanawake nchini Tanzania. Wanawake ni dada, mama na bibi zetu na ni lazima sote tuwapiganie kwakuwa wametutoa mbali katika maisha ya kila mmoja wetu. Pia wanawake kama walivyo wanaume wanastahili haki sawa. Hongera sana Bi Jane Magigita na MUNGU akutie NGUVU zaidi. Kwa habari zaidi soma Habari leo

Monday, March 3, 2014

Hongera Young Africans Sports Club aka YANGA kwa kuifunga timu mashuhuri kutoka nchini Misri National Al Ahly jumamosi 01/03/2014 ndani ya uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam

Hongera Dar es Salaam Young Africans aka Yanga kwa kuifunga timu mashuhuri kutoka nchini Misri National Al Ahly. Timu hii ni bingwa wa Afrika kwa sasa. Hakika blogu hii imefurahishwa na jinsi vijana wa jangwani walivyocheza siku ile ya jumamosi 01/03/2014 katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. Pia blogu hii inawapongeza viongozi wa Yanga kwa uongozi madhubuti uliopelekea timu kupata ushindi nyumbani. Pia blogu hii inawapongeza makocha wote wa Yanga kwa mbinu za hali ya juu zilizoiwezesha Yanga kupata ushindi huo.

Blogu hii pia inawapongeza mashabiki wa mpira nchini na hasa wale waliojitokeza kuishangilia Yanga. Hakika blogu hii ilifarijika kwa kuona jinsi wapenzi walivyokuwa nyuma ya wachezaji na timu nzima ya Yanga. Blogu hii inaomba viongozi, benchi la ufundi na wachezaji kujiandaa kikamilifu kwenye mechi ya marudiano itakayofanyika tarehe 09/03/2014 nchini Misri katika jiji la Cairo. Ni vyema wachezaji wakaandaliwa kisaikolojia na kimbinu ili Yanga iweze kusonga mbele. Ikiwezekana mikakati ya ushindi inapidi iandaliwe kama vile kuhakikisha timu inakwenda na maji na chakula chake ama mpishi wake maalum. Pia kuwepo na tahadhari wakati wote ndani ya ardhi ya Misri. Ulinzi uwe asilimia 100%. Pia wachezaji wahakikishe wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu na hasa wanapokuwa kwenye eneo lao. Pia watambue kuwa kutakuwa na filimbi zisizo rasmi ambazo zinaweza kuwachanganya wanapokuwa wanaenda lango la timu pinzani. Hapo wanatakiwa kusikiliza filimbi ya refarii tu na si vinginevyo.

Hakika blogu hii imegundua kumbe timu zetu zikiwa na juhudi, nia na malengo pamoja na nidhamu ya kimchezo uwezekano wa kuzifunga timu ziitwazo kubwa barani Afrika upo. MUNGU ibariki Yanga....MUNGU ibariki Tanzania. Mapambano bado yanaendelea!