Monday, February 17, 2014

Vita dhidi ya ujangili nchini Tanzania inastahili kuungwa mkono na wananchi wote wa Tanzania

Vita dhidi ya ujangili nchini Tanzania inastahili kuungwa mkono na wananchi wote wa Tanzania. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Kikwete akizungumza na shirika la habari la kimataifa la BBC juu ya juhudi za serikali kupambana na ujangili. Rais ameonyesha dhamira ya kweli ya kupambana na majangili hao. Kumekuwepo na operationi mbalimbali ambazo serikali imefanya kama vile operationi kipepeo na hii ya hivi karibuni ya operationi tokomeza ujangili.

Hakika blogu hii inaungana na serikali pamoja na Mkuu wa nchi katika mapambano dhidi ya vita ya ujangili. Blogu hii inampongeza Mh Rais kwa serikali yake kwa kuutambua mtandao mpana wa ujangili na kuzidi kupambana nao. Hakika ujangili unarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Blogu hii inaviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuzidisha kasi ya kuhakikisha majangili wanashindwa ili kuokowa tembo na faru ambao wako hatarini kutoweka. Juhudi kama tokomeza ujangili ilikuwa na lengo zuri sana ingawa kwa namna moja ama nyingine ilileta athari kwa wengine. Blogu hii inaiomba serikali kwa kutumia vyombo vyake kuifufua operationi tokomeza ujangili kwa namna ya kupambana na majangili hawa bila ya kuleta athari kwa wengine.

Nchi yetu inasifika sana kwa utalii. Utalii huu kwa namna moja unategemea uwepo wa wanyama hawa. Utalii huu, unaongeza pato la taifa ambalo linaiwezesha serikali kusukuma maendeleo kwa wananchi. Majangili kuendelea kuuwa tembo na faru ni kuhujumu uchumi wa taifa letu na kuikosesha serikali mapato ya kuwaletea wananchi maendeleo. Tuukatae ujangili kwa kauli moja!


Picha: Ayoubmzee.blogspot.com

PichaJourno Tourism


Thursday, February 13, 2014

Bila kulipa kulipa kodi tusitegemee maendeleo, wafanyabiashara wakubali kutumia mashine za EFD kulipa kodi!

Tukitaka maendeleo ya kweli kwa taifa letu ni kulipa kodi. Hivi karibuni serikali kupitia mamlaka ya kodi nchini (TRA) ilianzisha utaratibu wa wafanyabiashara kulipa kodi kupitia mashine za EFD. Ikumbukwe matumizi ya mashine hizi kwa wafanyabiashara umepitishwa na bunge la Tanzania mwaka 2011. Viongozi wengi wamesisitiza matumizi na faida ya mashine hizi za EFD. 

Bila kumung'unya maneno, baadhi yetu nchini tumekuwa na utamaduni wa kutopenda kulipa kodi. Kodi ni maendeleo, kodi ndizo zinazojenga miundombinu kama barabara, reli; kodi ndizo zinazowezesha serikali kujenga mashule na kuajiri waalimu wenye sifa; kodi ndizo zinawezesha serikali kujenga hospitali na vituo vya afya pamoja na kuajiri wauguzi na madaktari. Hakika bila kukusanya kodi taifa lolote ikiwemo Tanzania halitapiga hatua.

Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wagumu kukubali matumizi ya mashine hizi. Kuna baadhi wana sababu za msingi ambazo mamlaka ya mapato TRA inapaswa kuzifanyia kazi. Ila kuna dalili ya baadhi ya wafanyabiashara kwa makusudi wamekuwa hawataki matumizi ya mashine hizi. Hali hii itaifanya serikali kukosa mapato toshelezi ya kuwahudumia wananchi.

Blogu hii inawaomba wafanyabiashara kukubali kutumia mashine hizi kwa ustawi na maendeleo ya taifa letu. Nchi zilizoendelea kama vile Sweden zimefanikiwa kuwaletea wananchi wao maendeleo ya kweli kupitia kodi. Nchi hizo zinakusanya kodi. Moja ya njia nzuri ya kukusanya kodi kwa nchi hizi zilizoendelea ni kutumia mfumo wa mtandao wa kompyuta. Mfumo huu unawezesha kila mlipa kodi (mfanyabiashara/biashara) kulipa kodi. Hapa Tanzania, serikali inajaribu kwenda huko kwa wenzetu, yaani kukusanya kodi kwa njia ya kisasa, yaani kutumia mfumo wa mtandao wa kompyuta. Matumizi ya mashine ya EFD ni mojawapo ya mifumo ya mitandao ya kompyuta ambayo itaiwezesha TRA kukusanya kodi kikamilifu ili kuifanya serikali kupata fedha za kuwaletea wananchi maendeleo.

Blogu hii inaiomba TRA kuzidi kutoa elimu ya umuhimu wa kutumia mashine hizi za kieletroniki za EFD kwa wafanyabiashara. Pia blogu hii inaomba TRA kurekebisha kasoro za msingi zinazotolewa na wafanyabiashara. 

Picha: Barabara kama hizi hujangwa kutokana na kodi (hii picha toka nchini Mauritus inaonyesha jinsi gani nchi ikikusanya kodi vizuri na hasa kwa kutumia mashine za EFD za TRA inavyoweza kupata maendeleo)

Tuesday, February 11, 2014

Maktaba za kisasa zinawezekana nchini Tanzania

Hakika katika Chuo chochote maktaba ndio msingi wa maarifa, ni sehemu ambayo maarifa, taarifa na ujuzi unapatikana hapo. Mwanafunzi yoyote makini akipewa kazi na mwalimu wake ama akitoka darasani lazima aende maktaba kupata taarifa zaidi ili zimwongezee ujuzi na maarifa zaidi ya yale aliyoyapata darasani. Tanzania katika vyuo vikuu kuna maktaba kubwa na nzuri. Mfano wa maktaba kubwa na nzuri nchini Tanzania ni maktaba ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Nikiwa kama mdau wa blogu hii napenda kuwaeleza na kuwaonyesha watanzania na hasa wadau wa Elimu ya juu nchini Tanzania jinsi maktaba za wenzetu zilivyo na nini tunapaswa kuiga ili tupige hatua kitaaluma. Kitu kikubwa wenzetu walichofanya ni kuhakikisha mbali ya maktaba kuwa na vitabu na machapisho ya kisasa na ya kutosha pia wame hakikisha kuwa maktaba inakuwa kimbilio la wanafunzi kwa maana maktaba inakuwa inavutia na kumfanya mwanafunzi apende kuwa maktaba kwa muda mwingi. Maktaba ya Chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden ina mambo mengi yanayomfanya mwanafunzi apende kwenda maktaba. Katika maktaba hii mbali ya kuwa kama maktaba zetu nchini Tanzania lakini kuna sehemu za kupunzika, kula, kupaki magari na baiskeli, sehemu za vyumba vidogo vya majadiliano, sehemu ya kuangalia TV nk. Kuna kompyuta za kutosha na mtandao wa uhakika wa Internet na pia wanaruhusu wanafunzi kujua na simu, laptop ili waweze kupata taarifa za kimasomo kupitia Internet. Pia wana majalida, machapisho na vitabu vya kutosha vinavyokwenda na wakati. Pia wana vitabu na machapisho ya kimtandao yaani e-books na e-articles na e-journals za kutosha.

Uwepo wa e-books unasaidia kupungu tatizo la nafasi katika maktaba maana mwanafunzi sio lazima waje maktaba bali wanaweza kusoma vitabu (e-books ama e-journals) mahali popote iwe nyumbani ama sokoni. Hii inampa mwanafunzi uhuru na uwanja mpana wa kutumia maktaba mtandao "digital library" masaa 24 kwa siku!

Blogu hii inawaomba wadau wa Elimu ya juu nchini Tanzania kuiga  na kuwa na maktaba kama hizi. Huduma hizi zinaweza kuwekwa kwenye maktaba zetu pia. Mfano kuna "links" ambazo zinapatikana bure ambazo maktaba zetu zinaweza kujiunga na kuwawezesha watumiaji wa maktaba kutumia e-books na e-journals kama wanavyofanya wenzetu. Pia suala la kuweka vitu vingine kama sehemu ya kupunzika, kuzungumza yaani "discussion", kula, kupaki magari na baiskeli vyote vinawezekana.

Kuna mambo ambayo hayaitaji rasilimali fedha ambayo yanaweza kufanyika na kuzifanya maktaba zetu kuwa kimbilio la wanafunzi.


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden kuna "collection" 
za vitabu kama maktaba zingine za kawaida


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wamewekewa kompyuta kwa ajili ya kutafuta e-journals, e-books na huduma nyingi 
za kimtandao kwa ajili ya masomo yao


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden, sehemu hii 
inaitwa "information desk"


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wamewekewa vyumba vya mazungumzo ya kimasomo "discussion"


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wamewekewa sehemu ya kupunzika na kujipatia vinywaji bila ya kutoka nje ya
maktaba


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wana fursa ya kujisomea vitabu na machapisho mbalimbali kama maktaba za kawaida


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wamewekewa sehemu ya kujipatia vinywaji bila ya kutoka nje ya
maktaba


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wamewekewa sehemu ya kujipatia vyakula na vinywaji bila ya kutoka nje ya
maktaba


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wamewekewa mashelvu ya vitabu kama maktaba zingine


Picha: Kuna sehemu ya maegesho ya baiskeli kwa wanafunzi nje ya maktaba ya 
chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden


Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden, 
ni sehemu inayoonyesha vitabu vipya katika maktaba "newly arrival books"


Picha: Kuna sehemu ya maegesho ya baiskeli kwa wanafunzi nje ya maktaba ya 
chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden

Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wana fursa ya kutafuta vitabu na majalida na machapisho wayatakayo kama zilivyo
maktaba zingine za kawaida

Picha: Ndani ya maktaba ya chuo kikuu cha Karlstad nchini Sweden wanafunzi 
wamewekewa meza nzuri za kusomea ambazo zina soketi ya umeme juu ya meza

Monday, February 10, 2014

Elimu ya vitendo inawasaidia wanafunzi kuelewa mada ngumu, Wadau wa elimu Tanzania Tubadilike!

Hakika elimu kwa vitendo ni suala ambalo sisi watanzania na hasa wizara yetu ya elimu inapaswa kulitilia mkazo kwa kiwango kikubwa. Nchini Sweden, wanafunzi wa chekechea na shule za msingi wanajifunza kwa vitendo kwa kiasi kikubwa. Tanzania, tulikuwa tunaita elimu ya kujitegemea. Nakumbuka zamani miaka ya semanini hapa Tanzania kulikuwa na masomo ya sayansi kimu, maarifa ya nyumbani n.k. Nchini Sweden licha ya maendeleo makubwa waliyonayo bado hawajaacha kuwafundisha watoto wao maarifa ya nyumbani kama vile kushona, kuranda, kuchonga, kuchora n.k. 

Blogu hii inaiomba serikali ya Tanzania kupitia wizara husika kurudisha elimu kwa vitendo katika masomo tunayofundisha wanafunzi wetu. Kuna visingizio kwa baadhi ya wadau wa elimu kuwa hatuna vitendea kazi! Si kweli kwani kama mdau wa blogu hii nimeshuhudia kwa macho yango baadhi ya vifaa wanavyotumia sisi hapa Tanzania tunaweza kuvipata bila gharama yoyote. Vitu kama miti, udongo, maji, moto, uzi, kamba, majani, chupa zilizotumika n.k ni vitu ambavyo vinaweza kutumika kuwasaidia wanafunzi kuelewa somo vizuri.

Chupa mbili tupu zinatumika katika somo la fikizia, vitambaa vilivyotumika na uzi vinaweza kutumika kutengeneza midoli kwa wanafunzi.

Blogu hii inaomba watanzania hasa wadau wa elimu wabadilike na tuwafundishe wanafunzi kwa vitendo. Bila elimu ya vitendo itakuwa vigumu kwa wanafunzi wetu kuelewa mada ngumu. Elimu ya kujitegemea itiliwe mkazo sana na wakaguzi wa shule wafuatilie kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa kwa vitendo ili kudumisha dhana ya elimu ya kujitegemea. 
Picha: Moja ya shule ya msingi nchini Sweden, ambapo wanafunzi wanajifunza mpaka useremala!

Picha: Moja ya shule ya msingi nchini Sweden, ambapo wanafunzi wanatumia kamba, 
mabaki ya miti (fimbo na vipande vya mbao) kaika kujifunzauseremala!

Picha: Moja ya shule ya msingi nchini Sweden, ambapo vipande vya nguo vinatumika kutengeneza 
midoli na vitu vingine vya ushonaji!

Uwepo wa maktaba mashuleni unaongeza maarifa na ujuzi kwa walimu na wanafunzi.

Maktaba katika mashule ni suala ambalo Tanzania inatakiwa kulitilia mkazo. Nchini Sweden, takriban shule zote kuanzia chekechea, msingi mpaka sekondari kuna maktaba za shule. Maktaba hizi zinawasaidia wanafunzi kupata vitabu, majalida na machapisho mbalimbali kwa ajili ya masomo yao. Vile vile walimu nao hupata wasaa wa kutumia maktaba kwa ajili ya kuandaa mada mbali mbali za masomo kwa ajili ya wanafunzi.

Tanzania tunatakiwa kuiga mfano huo wa kuwa na maktaba za kisasa zenye vitabu, machapisho na majalida kwa ajili ya wanafunzi na walimu. Hii itawasaidia sana wanafunzi kuongeza ujuzi na maarifa wa mambo wanayojifunza shuleni.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inabidi itilie mkazo suala la maktaba mashuleni kwa kuweka vitabu, majalida na machapisho kulingana na mitaala husika na pia kuhakikisha wanaajili wakutubi waliohitimu toka taasisi zinazotoa mafunzo ya kimaktaba. Hii itasaidia kuwezesha wanafunzi na walimu kupata msaada wa kitaalamu toka kwa wataalamu (wakutubi).

Pia ni vyema kwa serikali kuwa na sera ya kuwa na maktaba katika shule zetu na kuhakikisha wakaguzi wa shule wanakagua uwepo wa maktaba za shule kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.


Uwepo wa maktaba mashuleni unaongeza maarifa na ujuzi kwa walimu na wanafunzi.


Picha: Mojawapo ya MAKTABA katika shule ya msingi nchini Sweden

Wednesday, February 5, 2014

Hongera Radio one stereo kwa kurusha matangazo kupitia internet

Hongera Radio one stereo kwa kurusha matangazo kupitia internet. Hakika blogu hii imefurahishwa sana na Radio hii kwa kuwapasha habari mbalimbali watanzania walioko ndani na nje ya Tanzania. Kama mdau wa blogu hii ya tuijenge tanzania nimefurahi sana kupata habari za Tanzania kupitia Radio One kwa njia ya mtandao wa internet nikiwa nchini Sweden. Nikiwa Sweden nimeweza kusikiliza kipindi  cha michezo cha saa moja na nusu usiku. Hakika nimeweza kumsikiliza live Maulid Kitenge kwenye kipindi hiki cha michezo. Pia unaweza kupata taarifa za moja kwa moja toka radio hii kwa vipindi vingine vingi kupitia internet. Hakika watanzania walioko nje ya Tanzania wanajifunia kuwa na radio hii.

Mtanzania yoyote aliye nje ya Tanzania anaweza kupata matangazo ya radio hii kupitia link hii. Hakika ukiwa popote pale duniani unapata uhondo na habari toka Tanzania kupitia radio hii. Aidha, ukiingia ndani ya ukurasa/link hii utakuta sura mbalimbali za watangazaji wa radio one kama vile Maulid Kitenge, Omary Katanga, Amina Chengo, Tumie Omary, Lugendo Madege, Isaac Gamba, Salma Dakota nk.

Blogu hii inaomba radio nyingine za Tanzania ziingie katika mfumo huu wa kimataifa ili kuwapasha watanzania habari mbalimbali.


Picha: ippmedia.com

Monday, February 3, 2014

Hongera MBWANA SAMATTA aka SAMA GOAL kwa kuwa mchezaji bora wa klabu ya TP Mazembe 2013

Mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta aka "Sama goal" amekuwa mchezaji bora wa klabu ya TP Mazembe kwa mwaka 2013. Klabu ya Tout Puissant Mazembe ni mojawapo ya klabu maarufu barani afrika na yenye mafanikio makubwa.
Aidha, mshambuliaji huyo wa kimataifa toka nchini Tanzania amewashinda wachezaji wenzake maarufu wa klabu hiyo kama vile Solomon Asante pamoja na Robert Kidiaba. Kwa mujibu wa taarifa Samatta alipata kura zipatazo 248. Wengine waliopata kura ni Asante Solomon aliyepata kura 219 akifuatiwa na Robert Kidiaba aliyepata kura 200, Nathan Sinkala aliyepata kura 97 na Rainford Kalaba aliyepata kura 67.
Samatta amekuwa tegemeo la ufungaji wa mabao kwa klabu yake ya TP Mazembe kuanzia Ligi Kuu ya CONGO DRC, Ligi ya Mabingwa Afrika nk.
Blogu hii inampongeza sana SAMATTA na kumuomba aongeze juhudi ili aje siku moja kuwa mchezaji mkubwa kwa ligi kubwa duniani hasa nchini uingereza, hispania, ufaransa nk. Pia blogu hii inawaomba wachezaji wengine wa tanzania wafuate nyayo za SAMATTA ili nao waweze kuitangaza nchi yetu na kuipa mafanikio. 
Blogu hii pia inaiomba TFF kuweka utaratibu mzuri wa soka la vijana kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa. Kwa njia hiyo nchi yetu itawapata wakina SAMATTA wengi zaidi na kuiwezesha nchi yetu kuwa tishio barani Afrika. Serikali nayo ina mchango mkubwa kwa kuhakikisha tunakuwa na miundo mbinu ya kisasa kama viwanja vikubwa na vya mazoezi mikoani na wilayani pamoja na kuhakikisha tunaifanya michezo kama somo la lazima katika shule za awali, msingi na sekondari. Maana ya kufanya hivyo ni kuwa sehemu kama shuleni ndipo penye chimbuko la wachezaji wanaojitambua. Pia serikali kupita wizara zake kama elimu na michezo ama utamaduni wanawajibika kuweka sera madhubuti za michezo na kuhakikisha wadau wengine kama mashule, vyama vya michezo, academy nk wanatekeleza sera za serikali kikamilifu.
Picha:in2eastafrica.net

Sunday, February 2, 2014

Hongera Clouds FM radio kwa kurusha matangazo kupitia mtandao wa internet- Radio ya watu

Hongera Clouds FM radio kwa kurusha matangazo kupitia mtandao wa internet. Hakika blogu hii imefurahishwa na juhudi zenu za kuwapasha habari watanzania walioko ndani na nje ya Tanzania. Nikiwa kama mdau wa blogu hii ya tuijenge tanzania nimefurahi sana kupata habari za Tanzania kupitia radio hii kwa njia ya mtandao wa internet nikiwa ulaya nchini Sweden. Nikiwa Sweden nimeweza kusikiliza takribani vipindi vingi vya radio hii hasa kipindi maarufu nikipendacho cha michezo cha saa tatu usiku kiitwacho sports xtra. Mbali na kusikiliza matangazo ya radio hii kupitia internet pia waweza kupata matangazo live vile vile. Hakika watanzania walioko nje ya Tanzania wanajifunia kuwa na radio hii ya kisasa inayokata anga. Na ndio maana ilikuwa ikiitwa mawingu studio enzi hizooo.

Mtanzania yoyote aliye nje ya Tanzania anaweza kupata matangazo ya radio hii kupitia link hii (ustream) ama kupitia kwenye mtandao wa radio hii. Aidha kwa kupitia mtandao wa internet waweza kupata matangazo ya Clouds Tv!! Hakika ukiwa popote pale duniani unapata uhondo na habari toka Tanzania.

Blogu hii inaomba radio nyingine za Tanzania ziingie katika mfumo huu wa kimataifa ili kuwapasha watanzania habari mbalimbali.


Picha: perfecttz.com

Hongera serikali ya Tanzania kwa kutoa punguzo la kuunganisha umeme vijijini hadi kufikia TShs 27,000 tu!

Serikali ya Tanzania imepunguza gharama za kuunganisha umeme kwa maeneo ya vijijini. Kabla ya punguzo hilo gharama ilikuwa TShs 177,000 tu lakini sasa ni TShs 27,000 tu. Aidha punguzo la awali lilikuwa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara lakini kwa sasa punguzo hilo ni kwa nchi nzima. Hakika blogu hii imefurahishwa na juhudi hizi za serikali za kusambaza umeme vijijini kupitia REA. Maendeleo ya kweli yanatoka vijijini ambako ndiko kuna uzalishaji kupitia kilimo na mifugo.

Pia blogu hii inaamini wananchi waishio vijijini watatumia fursa hii ili kuwa na umeme kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kimaendeleo. Kupitia juhudi hizi za serikali ni rahisi kwa wawekezaji kuamia vijijini kutokana na fursa ya umeme. Hii itachochea maendeleo kwa kuwa ni rahisi kuwa na viwanda vidogo na vikubwa vya usindikaji mazao. Hii itaongeza thamani ya mazao toka kwa wakulima ambao wengi wao wanaishi vijijini.


Picha:simbadeo

Saturday, February 1, 2014

Wawekezaji wa sekta ya madini nchini kulipa kodi ya asilimia 30 kwa mujibu wa sheria

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospiter Muhongo, amesema kuwa wawekezaji wa madini nchini watalazimika kulipa kodi ya asilimia 30 kwa mujibu wa sheria. Awali, wawekezaji walikuwa hawalipi kodi kwa kiasi hicho kwa madai kuwa walikuwa wakipata hasara. Kwa sasa wawekezaji wa sekta ya madini watalazimika kulipa kodi hiyo na kuleta mchango mkubwa kwa taifa.

Profesa Muhongo alisema kwa sasa sekta ya madini kwa sasa inachangia asilimia 3.5 ya pato lote la Taifa. Aidha Profesa Muhongo amesema malengo ya serikali ni kuhakikisha kuwa sekta hii ya madini inachangia zaidi ya asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Vilevile, lengo la serikali ni kuhakikisha sekta ya madini inaleta mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa. Blogu hii inampongeza Waziri wa Nishati na Madini kwa kauli hiyo ambayo inaleta matumaini kwa taifa letu changa. Ni imani ya blogu hii kuwa sekta ya madini itachochea maendeleo kwa taifa kama sheria hii ya kodi itasimamiwa vyema na serikali na wadau wengine. 

Picha: mwananchi.co.tz