Sunday, October 27, 2013

Wazo la busara toka kwa mdau wa elimu Geofrey Kalumuna - wadau wa elimu na walimu tubadilike!

Nilichoongea wakati wa uzinduzi wa jengo la " Teachers Professional Center" pale DUCE, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu! hakikuwa kitu cha ajabu sana. Ni mambo wenzetu wanayoyafanya siku zote. Kwa dunia ya sasa huwezi kwenda kasi ya maendeleo bila ya kukopa toka ICT. Huwezi kuwafikia walimu ambao ndio nguzo ya taifa bila ICT. Nitawapa mfano mmoja ili mwanafunzi wa kawaida aelewe somo vizuri bila kukalili lazima ASOME (hapa sisi walimu wengi ndio tunapoteza nguvu zetu! Kuwasomea wanafunzi tukizani tunawafundisha! Hiyo haitoshi!), AONE (hapa ndipo wenzetu wanapotuacha na ndio wanatilia mkazo -ICT inaingia hapa unaweza tumia ICT kutengeneza animations ukaziweka kwenye CD au ukachukua video kuelezea concept ya "reproduction" badala ya kulazimisha kuwasomea), na KUTENDA (hapa pia wenzetu nchi zingine wanatupiga bao! Hatufanyi hivyo kwa visingizio kibao eti hakuna mahabara nk wakati waweza tumia ICT ama vitu vinavyopatikana kwenye mazingira yako na wanafunzi wakafanya na kuelewa somo! Mfano tuna vyura wengi kwenye mazingira yetu na kwenye baadhi ya mitihani ya kidato cha nne wanafunzi wanatakiwa kufanya practicals za kupasua vyura lakini ni mara ngapi walimu wa biology wanafanya practical hizo kwa wanafunzi wao ili kuwaelewa concepts kwa vitendo? Ila tunasingizia hatuna vifaa wakati tuna mapanya tena mapanya buku mitaani bila kuacha machura yanayotupigia kelele usiku). Kwa kifupi nilichozungumza sio kitu kigeni ila ni utamaduni wetu wa kutotumia fursa kama walimu na wadau wa elimu. Teknolojia niliyozungumza ambayo yaweza saidia "in-service teachers" vyuo vingi wanatumia kule University of UP Daudi Danda unajua mambo online teaching ya illuminate! Sasa kwa jinsi gani teknolojia hiyo inaweza kutusaidia kuwapa maarifa na ujuzi walimu wetu kwa gharama nafuu! Maana sio rahisi kuleta walimu wote kwenye chuo kama DUCE na kuwapa mbinu za kisasa bila ya kutumia teknolojia!
Mdau: Geofrey Kalumuna


Saturday, October 26, 2013

Tanzania 10 - Msumbiji 0 - Hakika Timu ya Taifa ya Wanawake walio chini ya miaka 20 watatupeleka Canada kwenye kombe la dunia!

Hongera Timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 kwa ushindi mnono mlioupata leo kwenye uwanja wa taifa.
Mchezo wa leo ni harakati za Timu yetu kuwania kuingia fainali za wanawake zitakazofanyika nchini Canada mwakani kupitia kanda ya Afrika. Timu yetu imepata ushindi wa mabao 10 kwa 0!
Hakika Timu hii imetutoa kimasomaso licha ya wadau wa michezo nchini kuwa bize na uchaguzi wa bodi ya ligi na ule uchaguzi wa shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF).
Lakini blogu hii inaungana na wadau wa michezo nchini hususan kandanda kuipongeza Timu yetu ya wanawake kwa ushindi mkubwa walioupata.
Tunaomba wale wote walio bize na uchaguzi wahakikishe wakishachaguliwa wanatilia mkazo uanzishwaji wa ligi ya wanawake nchini Tanzania ili tuweze kupata wachezaji bora watakaoliwakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa.
Picha: landboybeibe

Thursday, October 24, 2013

Hongera Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na DUCE kwa kujenga kituo maalum "Teachers Professional Center"

 
 


Hongera serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kujenga kituo maalum katika chuo kikuu kishiriki cha DUCE kiitwacho "Teachers Professional Center". Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Gharib Bilal alikuwa mgeni rasmi katika halfa hiyo ya uzinduzi iliyofanyika Jumatano ya tarehe 23 mwezi wa kumi mwaka 2013.

 

Aidha kama mdau nilipata fursa ya kutoa mada mbele ya Makamu wa Rais Mh Gharib Bilal jinsi gani kituo cha "Teacher Professional Center" kinachomilikiwa na DUCE kinavyoweza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuchangia ubora wa Elimu nchini na hasa kuweza kuwapa maarifa na ujuzi walimu (in-service teachers) kupitia Teknolojia ya kisasa ili kuongeza maarifa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini na kuongeza ufaulu. 

 

Uzinduzi wa kituo hiki unaenda pamoja na kauli mbiu ya "Big Results Now" yaani "Matokeo Makubwa Sasa" katika sekta ya elimu nchini Tanzania.

 

Blogu hii inapenda kuipongeza serikali ya Tanzania chini ya Mh Rais Jakaya Kikwete kwa ujenzi wa kituo hiki maalum kitakacho chochea kasi ya elimu nchini na hasa kitakachokuwa kikitumika kutoa mafunzo kwa walimu walio makazini kupitia Teknolojia ya kisasa. Aidha blogu hii inakipongeza chuo kikuu kishiriki cha Elimu DUCE kwa kuweza kutekeleza ujenzi wa kituo hiki. Vile vile blogu hii inawapongeza wadau na wafanyakazi wa DUCE pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika kusimamia ujenzi wa kituo hiki.

 

Pia blogu hii inatoa pongezi na shukrani za pekee kwa Benki ya Dunia (World Bank) kupitia mpango mahsusi uitwao "Science Technology and Higher Education Program (STHEP) " uliofanikisha miradi mingi nchini kwenye sekta ya elimu juu ukiwemo mradi huu wa wa ujenzi wa  "Teacher Professional Center" ndani ya chuo kikuu kishiriki cha DUCE.

 

Blogu hii inaomba kituo hiki kitunzwe na pia kitumike kikamilifu ili kukizi lengo la kituo chenyewe pamoja na kufikia malengo ya BIG RESULTS NOW! Pamoja tutafika!
 

 







 



 


Friday, October 18, 2013

Hongera YANGA kwa kuonana na Mstahiki Meya wa Ilala ya kuomba nyongeza ya eneo la kujenga uwanja

Hongera sana klabu ya YANGA kwa kuwa na wazo la uwanja wa kisasa ambao michoro ya awali ishachorwa na wataalamu. Pili blogu hii ina upongeza uongozi wa klabu ya YANGA kwa kuonana na Mshahiki Meya wa Manispaa ya Ilala na kutuma maombi ya kuongeza eneo la kiwanja. Hakika juhudi hizi zinastahili kuungwa mkono na wadau wote wa michezo hususan mpira wa miguu aka kandanda AMA kabumbu. Kwa mujibu wa mtandao wa YANGA Meya wa Manisapaa ya Ilala jijini Dar es salaam mstahiki Jerry Slaa leo amepokea maombi ya klabu ya Young Africans kuhusu kuomba eneo la ziada kwa ajili ya kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa uwanja wa kisasa eneo la jangwani.
Juhudi hizi sio ndogo na zinapaswa kuendelezwa. Wapo watu wanafikiri hii ni ndoto la hasha bali inawezekana kwa Klabu kama YANGA kujenga uwanja wa kisasa. YANGA ina wadau wengi sana ndani na nje ya nchi. 
Kinachohitajika ni kwa YANGA kuunda kamati ya ujenzi itakayowashirikisha wadau wa YANGA wakiwemo wataalamu mbalimbali wa ujenzi, wataalamu wa masoko, wataalamu wa ardhi na miundombinu, makocha, wachezaji wa zamani, wafanyabiashara, wanasiasa bila kusahau wakeleketwa YANGA wakiwemo na wanachama na baadhi ya wajumbe toka kwenye uongozi wa YANGA. Muhimu kamati iwe na watu makini na wanaoaminika ili moja ya jukumu ni kuandaa mpango mkakati na pia kuusimamia mpango huo. Mpango huo uonyeshe roadmap ya kupata fedha na na namna pesa itakavyotumika.Klabu nyingine zinapaswa kuiga mtizamo wa YANGA ili Tanzania ipige hatua kwenye maendeleo ya soka.
Kwa habari zaidi bofya hapa.

Wednesday, October 16, 2013

Hongera blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania"

Hongera blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania" ambayo lengo lake kuu ni kuwasaidia wafugaji nchini Tanzania kupata elimu bora ya kisasa ya ufugaji ili waweze kupata matokeo mazuri na kuwasaidia kupata kipato kwa kupunguza hasara ambazo zinaweza kutokea kutokana na magonjwa mbalimbali.
 
Blogu ya "tuijengetanzania" inaipongeza blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania" kwa kuanzisha blogu inayowasaidia wafugaji nchini ili kuwasaidia katika kupambana na changamoto za ufugaji kama vile magonjwa ili kuweza kuwafanya wafugaji kupata faida kubwa.
 
Wadau wa ufugaji na hasa wafugaji wadogo wadogo nchini Tanzania wanaombwa kutembelea blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania" ili kuweza kupata taarifa na maarifa juu ya ufugaji. Taarifa na maarifa watakayopata yatawafanya waepuke magonjwa na kuweza kujua dalili, kinga na matibabu ya magonjwa ya wanyama wafungwao na kupata faida kubwa.
 
 
 
 

Tuesday, October 15, 2013

Hongera serikali ya Tanzania kwa kuanzisha Tume ya TEHAMA “ICT” nchini

Hongera serikali ya Tanzania kwa kuanzisha Tume ya TEHAMA “ICT” nchini Tanzania. Hakika hatua hii ya serikali ni ya kuungwa mkono. Wadau wa TEHAMA nchini tumefurahi na kufarijika sana baada ya kusikia serikali ipo kwenye mchakato wa kuanzisha tume ya TEHAMA. Tume hii itaratibu, itasimamia na kuendeleza shughuli zote ya TEHAMA nchini. Sekta hii ya TEHAMA inakuwa kwa kasi sana duniani na hapa nchini. Sekta hii pia inaingia kwenye kila nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Hivyo ili Tanzania iwe na mafanikio kupitia sekta hii, Tume ya kuratibu TEHAMA ni ya umuhimu sana.
Kwa uchache, TEHAMA ina chagamoto zake kama vile uwepo suala la usalama wa taarifa za watu mbalimbali (e-security), haki ya faragha (e-privacy),  pamoja na haki ya wanachi kupata taarifa (freedom of information). Mambo haya kwa kweli yana umuhimu wake lakini yanakinzana. Nchi mbalimbali bado zinachangamoto ya kuweka mstari kati ya haya mambo matatu.
Hivyo basi pamoja na mambo mengine Tume hii tunatarajia itakuja na mfumo ama uwezo wa kulinganisha masuala haya matatu ili yasilete athari nchini.
Pia ni wakati muafaka kwa serikali kupitia tume hii kuanzisha sera mbalimbali za TEHAMA kama vile sera ya mitandao ya kijamii (social media policy), sera ya mkonga wa internet (broadband internet policy) pamoja na kupitia tena sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 (ICT policy of 2003). Sera hii imekaa kwa muda mrefu na inahitaji mapitio  “review”.
Kuna mambo mengi sana ambayo tume hii ina kazi kubwa ya kufanya. Lingine ni kuhamasisha na kutoa kipaumbele sehemu za vijijini kuwa na TEHAMA na huduma za internet na data. Njia mojawapo ni kwa tume kuweka “incentive” kwa makampuni ama watu wataowekeza vijijiji ili taifa letu liweze kupiga kasi inayostahili. Incentive hii inaweza kuwa kwenye kodi.
Hakika kuna mambo mengi ya kufanya, hivyo kama wadau tunaipongeza sana serikali kwa kuwa na wazo hili la kuanzisha tume ya TEHAMA nchini. Hakika tupo pamoja na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha TEHAMA inakuza uchumi na kuleta ustawi nchini.
Picha: sundayshomari.com
prisca_tena_fee8f
Afisa Habari Mwandamizi toka Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia Bi. Prisca Ulomi(kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu Uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, wakati wa Mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO)

Mh. Ummy Mwalimu atumia siku ya kimataifa ya mtoto wa kike  jijini Tanga kuzindua Mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga kupitia TAWODE

Siku ya tarehe 11 oktoba mwaka huu ilikuwa siku ya kimataifa ya Mtoto wa Kike. Mh. Ummy Mwalimu Naibu waziri wa maendeleo ya wanawake, jinsia na watoto alitumia siku hiyo  jijini Tanga kuzindua Mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga chini ya Taasisi ya Tanga Women Development Initiative (TAWODE).
 
Mgeni rasmi alikuwa Mhe Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga. Kupitia mradi huu Mh. Ummy  ametekeleza kwa vitendo dhamira yake kama kiongozi - aliyechaguliwa na wanawake wa mkoa wa Tanga katika kuchangia na kuboresha maisha ya wanawake wa mkoa wa Tanga.

Mradi huu  utakaotekelezwa katika Wilaya za Pangani, Muheza, Mkinga, Lushoto na Tanga Mjini, umelenga kuchochea uwezo na ubora wa wasichana wenye umri wa miaka 10-24 kutambua weledi na umuhimu wao kwa maendeleo yao na ya jamii zao. Kupitia Mradi huu Mh. Ummy na wenzake wamedhamiria kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wasichana waliopo katika shule za Serikali za Msingi na Sekondari, kuboresha hali ya afya ya uzazi, kupunguza mimba za mapema, ndoa za utotoni na maambukizi ya virusi vya ukimwi. Aidha wamepanga kuwafikia moja kwa moja wasichana 16,000 na zaidi ya 100,000 kupitia njia mbalimbali ikiwemo mabango, Radio jingles (Mwambao FM 106.0), matamasha ya wasichana nk. Aidha Wasichana 1,000 waliopo shuleni na wanaoishi katika mazingira magumu wataingizwa katika Mfuko wa Bima ya afya ili kuweza kupata huduma za afya bure. Ni imani ya Mh. Ummy kuwa jitihada hizi zitachochea maendeleo ya wanaTanga kwa jumla. 

 
Hakika blogu hii imefurahishwa sana na Juhudi azifanyazo Mh. Ummy na wenzake. Blogu hii inamwomba Mh. Ummy azidi kuongeza Juhudi hizi ndani ya mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Blogu hii pia bado inatambua mchango wa Mh. Ummy nchini Tanzania katika kusimamia masuala ya wanawake na watoto.
 
Blogu hii inamwomba Mh. Ummy kupitia wizara yake kuweka sheria kali zinazowalinda watoto mfano sheria zinazokataza watu wenye umri mkubwa kufanya ngono na vitendo vya kingono na watoto wadogo chini ya miaka 16 ama 18. Sheria hizi zipo kwa wenzetu na ni kali ambazo zinawalinda watoto hasa wa kike na watu wajulikanao kama "sugar dad". Hakika zipo sheria nyingi ambazo kupitia wizara husika wanaweza kuziingiza kwenye system
 


 



Saturday, October 12, 2013

Hakika Azam TV na TBC1 mnastahili pongezi za dhati kwa kuonyesha michezo ya ligi kuu Tanzania Bara

Hakika Azam TV na TBC1 mnastahili pongezi za dhati.  Azam TV kwa sasa inaonyesha michezo ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara. Azam TV wameonyesha mapinduzi makubwa katika soka nchini kwa kuonyesha michezo ya ligi kuu kwa kiwango bora na cha kimataifa. Nchi jirani zinaonyesha ligi zao kupitia vituo vingine vya nchi za ng'ambo. Hakika watanzania na hasa wana wanamichezo wanajivunia mafanikio haya ya Azam TV.

Juhudi hizi za Azam TV zinastahili kuungwa mkono na wadau wote wa michezo ikiwemo serikali. Thamani ya mpira wa Tanzania itakuwa kwa msaada wa Azam TV. Vile vile wachezaji kitanzania wataonekana kimataifa na kufanya soko lao kuwa kubwa.
Picha:deejaydeo.blogspot.com 

Tuesday, October 8, 2013

Hongera Mh. Magufuli kwa kusimamia sheria na kulinda barabara zetu nchini Tanzania

Hakika kwa hili la kulinda barabara Mh. John Pombe Magufuli unastahili pongezi za dhati. Barabara zote duniani hulindwa na pia zinastahili kulindwa kikamilifu. Nchi nyingi zimeendelea kwa kujenga na kulinda miundombinu hasa barabara na reli. Kama tujuavyo barabara zinatengenezwa kwa gharama kubwa sana hapa nchini Tanzania na kwingineko. Hivyo wenye malori na magari yanayobeba mizigo ni vyema wakafuata sheria ili kulinda barabara. Kuzidisha uzito kwenye barabara si jambo jema hata kidogo (kiuhalisia na kisheria). Barabara zote duniani zinalindwa sana, tena za wenzetu zina viwango vikubwa vya lami hasa uko ulaya na amerika pamoja na nchi za asia. Hivyo malori yanayozidisha uzito yanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu barabara na taifa linaingia kwenye gharama kubwa ya matengenezo ya mara kwa mara. 
 
Blogu hii inampongeza sana Mh. Magufuli kwa kusimamia sheria pamoja na kulinda barabara. Pia blogu hii inawaomba wenye malori na magari yanayobeba mizigo kuzingatia uwezo wa barabara na kufuata sheria ili kuimarisha uchumi kwa njia ya barabara. Hakika nchi hii inahitaji viongozi wakali na wenye msimamo. Bila ya kufuata sheria hatutafika kokote. Mh. Magufuli ameonyesha mfano ingawa kwa wengine inaweza kuonekana ni jeuri lakini kama tunataka kuendelea lazima tufuate sheria na sio kila mtu afanye atakavyo. Labda nimalizie kwa kusema hivi, kuna baadhi ya nchi duniani zina barabara za ghorofa kuanzia moja mpaka saba na kule kuna uzito wa magari unaostahili kupita. Sasa je kwa kutofuata sheria, hapa Tanzania tutakapokuja kujenga barabara za juu na kuruhusu kila gari lipite bila kujali uzito nini kitatokea? majanga! Pia tukumbuke zipo barabara za mitaani ambazo magari makubwa hayatakiwi kupita kwa sababu ya kiwango cha lami na ukubwa wa barabara husika, je hilo wenye malori hawajui?
 
Mwisho, blogu hii inaomba wenye malori na magari makubwa yanayobeba mizigo wafuate sheria. Pia ni wakati muafaka sasa kwa serikali kujenga na kuimarisha reli ili kupunguza mizigo mingi inayosafirishwa kwa barabara.
Kwa habari zaidi bofya hapa
 
Picha: geofreymtenzi.blogspot.com
 
 

Monday, October 7, 2013

Hongera eGA (serikali matandao) kwa kuwa na mpango mkakati wa miaka mitano

Hongera eGA (serikali matandao) kwa kuwa na mpango mkakati wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2012/13 mpaka 2016/17. Shabaha kubwa katika mpango huo mkakati ni kuziwezesha idara zote na taasisi za serikali zikiwemo wizara zote nchini pamoja na serikali za mitaa kutumia TEHAMA katika shughuli za kila siku za utendaji ili kuongeza uwazi na ufanisi pamoja na kuwafanya wananchi kupata taarifa mbali mbali za serikali.
Blogu hii inaipongeza idara eGA kwa kazi kubwa iliyofanya na inayofanya ya kuwezesha serikali kutoa huduma kwa haraka na ufanisi mkubwa kupitia matumizi ya mtandao wa Internet nchini. Blogu hii inaomba juhudi hizi ziendelezwe ili kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi iliyopiga hatua katika matumizi ya TEHAMA duniani. Kwa taarifa zaidi bonyeza hapa

Picha:http://www.ega.go.tz/

Thursday, October 3, 2013

Mafunzo ya ufundi kwa vijana ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote

Picha: Toka kwenye mojawapo ya chuo mjini Melbourne, Australia
Mafunzo ya ufundi kwa vijana ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote.

Nchini Australia katika mji wa Melbourne, vijana wengi waliokosa fursa ya kuendelea na masomo ya juu yaani kwenda vyuo vikuu huingia katika mafunzo haya ya ufundi kwa vitendo. Mafunzo haya huku Australia yanaitwa Vocational Education & Training (VET). Mafunzo haya kwetu Tanzania yanaendeshwa na VETA.

Mafunzo haya ni muhimu kwa taifa lolote hasa Tanzania maana yanatoa na kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi mbalimbali kuanzia wahudumu wa hoteli, mafundi wa magari na mashine ndogo na kubwa, wajenzi wa barabara na madaraja, wajenzi wa majumba nk.
Uchumi wa nchi yoyote hapa duniani unategemea watu wa aina hii. Hata wale vijana wanaomaliza vyuo vikuu bado na wao wanatakiwa kupata mafunzo haya ya ufundi kwa vitendo ili kupata ujuzi wa kazi. Vijana toka vyuo vikuu huwa ni wazuri kwenye eneo la nadharia (theory) lakini huwa na upungufu kwenye eneo la vitendo. Hivyo kwa wenzetu huwa wanawahimiza wanafunzi wa vyuo vikuu kujiunga na vyuo vya ufundi kwa vitendo kupata ujuzi kwa vitendo.

Blogu hii inaomba mafunzo haya yatiliwe mkazo ili taifa letu liwe na wajuzi wa kazi kwa vitendo na kuifanya Tanzania kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

Blogu hii pia inaiomba serikali ya Tanzania kutenganisha shughuli za VETA na kuwa taasisi ya kutoa mafunzo (service provider) pekee na kuanzisha taasisi nyingine ya kusimamia (regulator) ili kuwe na ufanisi katika mafunzo kwa vitendo (vocational skills training). Pia kunaweza pia kuwa na taasisi nyingine ya kusaidia hasa katika masuala ya utoaji fedha na vifaa kwa ajili ya mafunzo na usimamizi wa hayo mafunzo.

Kwa maneno mengine kuna kuwa na mfumo wa namna hii
Service Provider - Regulator - Facilitator

Kwa sasa shughuli zote hizi zinafanywa na VETA, hivyo inakuwa vigumu kuendesha kwa ufanisi yaani kutoa mafunzo kama "service/training provider", kusimamia mafunzo "regulator", kusaidia mafunzo kifedha na vifaa "facilitation"

Kitu cha muhimu kukumbuka ni kuwa kuna vyuo vingi vya VETA nchini vinavyoendeshwa na VETA yenyewe na pia kuna vyuo vingine vya binafsi vinavyosimamiwa na VETA.

Blogu hii inaona kuwa kukiwa na mgawanyo wa majukumu, fani ya ufundi kwa vitendo (vocational education training) hapa nchini itapiga hatua kuwa na kuchangia maendeleo ya Taifa.