Tuesday, October 8, 2013

Hongera Mh. Magufuli kwa kusimamia sheria na kulinda barabara zetu nchini Tanzania

Hakika kwa hili la kulinda barabara Mh. John Pombe Magufuli unastahili pongezi za dhati. Barabara zote duniani hulindwa na pia zinastahili kulindwa kikamilifu. Nchi nyingi zimeendelea kwa kujenga na kulinda miundombinu hasa barabara na reli. Kama tujuavyo barabara zinatengenezwa kwa gharama kubwa sana hapa nchini Tanzania na kwingineko. Hivyo wenye malori na magari yanayobeba mizigo ni vyema wakafuata sheria ili kulinda barabara. Kuzidisha uzito kwenye barabara si jambo jema hata kidogo (kiuhalisia na kisheria). Barabara zote duniani zinalindwa sana, tena za wenzetu zina viwango vikubwa vya lami hasa uko ulaya na amerika pamoja na nchi za asia. Hivyo malori yanayozidisha uzito yanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu barabara na taifa linaingia kwenye gharama kubwa ya matengenezo ya mara kwa mara. 
 
Blogu hii inampongeza sana Mh. Magufuli kwa kusimamia sheria pamoja na kulinda barabara. Pia blogu hii inawaomba wenye malori na magari yanayobeba mizigo kuzingatia uwezo wa barabara na kufuata sheria ili kuimarisha uchumi kwa njia ya barabara. Hakika nchi hii inahitaji viongozi wakali na wenye msimamo. Bila ya kufuata sheria hatutafika kokote. Mh. Magufuli ameonyesha mfano ingawa kwa wengine inaweza kuonekana ni jeuri lakini kama tunataka kuendelea lazima tufuate sheria na sio kila mtu afanye atakavyo. Labda nimalizie kwa kusema hivi, kuna baadhi ya nchi duniani zina barabara za ghorofa kuanzia moja mpaka saba na kule kuna uzito wa magari unaostahili kupita. Sasa je kwa kutofuata sheria, hapa Tanzania tutakapokuja kujenga barabara za juu na kuruhusu kila gari lipite bila kujali uzito nini kitatokea? majanga! Pia tukumbuke zipo barabara za mitaani ambazo magari makubwa hayatakiwi kupita kwa sababu ya kiwango cha lami na ukubwa wa barabara husika, je hilo wenye malori hawajui?
 
Mwisho, blogu hii inaomba wenye malori na magari makubwa yanayobeba mizigo wafuate sheria. Pia ni wakati muafaka sasa kwa serikali kujenga na kuimarisha reli ili kupunguza mizigo mingi inayosafirishwa kwa barabara.
Kwa habari zaidi bofya hapa
 
Picha: geofreymtenzi.blogspot.com
 
 

No comments:

Post a Comment