Sunday, June 22, 2014

Hongera Mh Ummy Mwalimu kwa kutilia mkazo upandaji wa miti nchini

Hongera sana Mh Ummy Mwalimu kwa kutilia mkazo upandaji wa miti nchini. Mh Ummy ameshiriki katika upandaji miti Same mkoani Kilimanjaro katika kijiji cha Mabilioni tarehe 17/06/2014 ikiwa ni siku ya kupambana na hali ya jangwa na ukame duniani.

Upandaji miti una faida nyingi ikiwa ni pamoja na utunzaji mazingira ambapo kwa sasa ni suala la kimataifa. Upandaji wa miti pia unapendezesha manthari ya sehemu husika. Na mwisho miti huongeza pato la taifa kwa maana ya uvunaji na uuzaji wa mazao yatokanayo na miti kama mbao. Pia blogu hii imefurahishwa na mkakati wa kuhakikisha Halmashauri nchini zinatilia mkazo suala la upandaji miti. Pia blogu hii imefurahishwa suala la kuhamasisha makundi hasa ya vijana katika suala zima la upandaji miti.

Blogu hii inaomba licha ya juhudi za kupanda miti nchini pia kuwe na sheria na kanuni za kukata miti. Kuwa na utaratibu huu utaokoa miti mingi inayokatwa bila sababu ya msingi na hivyo kuharibu mazingira. Ipo mifano mingi ya watu kukata miti bila sababu za msingi. Kuwepo kwa sheria na kanuni kutawabana wale wote wanaofikiria kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo. Tanzania inaweza kuwa na sheria ama kanuni ya kama mtu ama kikundi kikitaka kukata mti lazima kiombe kibali (tunaweza kuanzia katika ofisi za mtaa/kijiji) ambazo zinatambuliwa na Halmashauri. Ni vizuri kukumbushana katika nchi zilizoendelea sio rahisi kukata mti ovyo LAZIMA uombe kibali toka mamlaka husika, hivyo Tanzania tuige mfano huo.


Blogu hii inaomba wadau wengine wa mazingira wamuunge mkono Mh Ummy katika jitihada za kupanda miti na kutunza mazingira.

Mh Ummy Mwalimu akipanda mti, katika kijiji cha Mabilioni, Same mkoani Kilimanjaro tarehe 17/06/2014

Wednesday, June 18, 2014

Hongera Malinzi na TFF kwa kuipeleka Taifa Stars nchini Botswana kama sehemu ya maandalizi dhidi ya Msumbiji


Picha: bongo5.com


Picha: 24tanzania.com
Hongera Rais wa TFF, Jamal Malinzi na TFF kwa ujumla kwa kuipeleka Taifa Stars nchini Botswana kama sehemu ya mazoezi. Timu ya Taifa ya Tanzania inatarajiwa kuweka kambi ya mazoezi nchini Botswana kwa wiki mbili ikiwa ni maandalizi ya mechi dhidi ya Msumbiji. Taifa Stars inatarajiwa kupambana na Msumbiji Julai 20 mwaka huu 2014. Blogu hii inaamini haya ni maandalizi sahihi ya kiwango cha kimataifa ambayo kwa miaka mingi timu yetu iliyakosa. Hii mbali na kuwaandaa wachezaji vizuri inawapa motisha kubwa wachezaji. Wachezaji nao mbali ya kupata mazoezi stahili wanabaki na deni kwa watanzania na hivyo kucheza kwa kiwango kikubwa katika mechi ya mashindano.

Blogu hii inampongeza kwa dhati kabisa Rais wa TFF pamoja na TFF kwa ujumla kwa juhudi wanazo zionyesha katika kuisaidia Timu ya Taifa kusonga mbele na kufanya vizuri. Yapo mambo mengi ambayo TFF ya sasa imefanya ikiwa ni pamoja na kumleta kocha mzuri sana, Mholanzi Mart Nooij. Blogu hii inaomba TFF izidi kukuza mpira wa miguu nchini na hasa kwa kuangalia soka la vijana na watoto pamoja na kuhakikisha linapata mahitaji muhimu kama walimu bora, vifaa bora, viwanja bora, marefa bora, madaktari wa michezo bora, viongozi bora wa michezo kwa watoto pamoja kuwapa elimu ya darasani wakati wakiwa katika maboresho. Kazi hii inapaswa kufanywa na wadau wengine kama mashule, academy mbalimbali, wakati TFF inabaki kama mratibu na kuendesha mashindano. Kwa habari zaidi soma habari leo.

Saturday, June 14, 2014

Hongera Kikwete na Clouds Media kwa uzinduzi wa Tamasha la Uzalendo mjini Dodoma

Hongera Rais Kikwete na Clouds Media kwa uzinduzi wa Tamasha la Uzalendo mjini Dodoma. Tamasha hilo lilimezinduliwa rasmi na Mh Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dr Jakaya Mrisho Kikwete. Tamasha la Uzalendo ni jambo zuri sana na la kuungwa mkono na wazalendo na wananchi wa nchi hii kwa ujumla. Mbali na wasanii wa muziki wa kizazi kipya na Bongo MovieTamasha, pia Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda alikuwepo. Tamasha la Uzalendo lilienda pamoja na uzinduzi wa Video ya Wimbo Maalum wa Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 

Blogu hii imefurahishwa sana na uzinduzi wa Tamasha hili linaodumisha umoja, amani na upendo nchini. Uwepo wa upendo, amani na umoja ndio kichocheo cha maendeleo katika taifa lolote ikiwemo Tanzania. Asante Clouds Media, wasanii walioshiriki, wananchi walioshiriki pamoja na viongozi wakiongozwa na Mh Rais Kikwete.

Aidha lengo la jumla la tamasha hili ni kwa watanzania kudumisha uzalendo, upendo na kuithamini na kuipenda nchi yao. Helo helo watanzaniaaaa,Helo helo Upendoo wa kweli!

Picha:http://tanzaniatoday.co.tz/



Hongera uongozi unaomaliza muda wake wa Simba SS chini ya Mh Rage kwa kujenga UWANJA wa MAZOEZI Bunju

MATENGENEZO ya uwanja mpya na wa kisasa wa klabu ya Simba kama ilivyoahidiwa na uongozi unaomaliza muda wake chini yake Alhaj Ismail Aden Rage umeanza (Picha:mambouwanjani.blogspot.com)

Hongera sana uongozi wa Simba Sports Club unaomaliza muda wake kwa mambo makubwa yaliyofanyika na yanayofanyika sasa chini ya Mh Rage. Kwa baaadhi ya watanzania wataona mambo haya ni madogo na wengine wataanza yale maneno yetu "Kwanini hawakuanza zamani?? Kwanini sasa?? nk" Maswali haya, siyo ya msingi, maana uongozi wa Simba unaomaliza muda wake umetimiza ahadi kwa wanachama wao nao ni kujenga uwanja wa mazoezi. 

Blogu hii inaomba kuwaeleza wadau wake kuwa kujenga uwanja sio jambo dogo. Mafanikio ya UONGOZI wa Mh Rage katika hili ni:
  1. Kutafuta eneo la uwanja (limepatikana Bunju);
  2. Kujenga uwanja wa mazoezi katika eneo hilo (kazi inaendelea ya kuondoa udongo wa asili na kuweka nyasi zinazotakiwa-kazi inaendelea);
  3. Kuweka maandalizi ya kujenga hostel pale Bunju;
  4. Kuweka maandalizi ya uwanja wa kisasa (hiyo ni kazi ya viongozi watakaokuja baada ya Uchaguzi mwezi huu wa sita, 2014).


Blogu hii kwa makusudi kabisa inaupongeza uongozi unaomaliza muda wake chini ya mpiganaji asiyechoka Mh. Alhaji Ismail Aden Rage. Uongozi wa Mh Rage ndani ya Simba ulikabiliwa na upinzani usiokuwa na tija ambao ulisababisha baadhi ya mambo kutofanyika vizuri ama kwenda kinyume. Lakini bado blogu hii itamkumbuka sana Mh Rage na hasa kwa hili la kuwaachia wanamsimbazi UWANJA wa MAZOEZI ambao watakaokuja watajenga UWANJA mwingine MKUBWA pamoja na majengo ya hostel, ofisi nk. Hongera Mh Rage kwa kawaida mtu hathaminiwi kwao ila wachache tunatambua mchango wako. Hongera.

Ushauri kwa watani wa SIMBA yaani YANGA nao wafikirie kwenda Bunju ama Kisarawe ama kokote kule nje ya mji wa Dar es Salaam watakapopata eneo kubwa kama SIMBA walivyofanya ili kujenga "Complex ya michezo" yenye hosteli, ofisi, maduka ya vifaa vya michezo kama jezi, mahotel, sehemu ya kuogelea pamoja na UWANJA mkubwa wa kisasa.

Picha: 24tanzania.com

Wednesday, June 11, 2014

Hongera kwa jamii ya Tanzania kwa ongezeko la UMRI wa KUISHI toka miaka 50 mpaka 60


Picha: mapsofworld.com
Hongera kwa serikali pamoja na jamii nzima ya Tanzania kwa ongezeko la UMRI wa KUISHI hapa TANZANIA. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, umri wa kuishi kwa watanzania umeongezeka kutoka miaka 50 (sensa ya mwaka 1988) hadi kufikia miaka 61 (sensa ya mwaka 2012).

Hayo yalisemwa na mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa wakati akiwasilisha taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi kwenye hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Aidha, alisema wanawake wanaishi umri mrefu zaidi kuliko wanaume. Matokeo haya yanaonyesha wastani wa umri wa kuishi kwa wanawake ni miaka 63 tofauti na wanaume ambao ni miaka 60. 

Ongezeko la umri wa kuishi limetokana na kukua kwa uchumi na kupungua kwa umaskini wa kipato miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Aidha pia ongezeko hili linatokana na juhudi za serikali katika kuwaletea wananchi wake maendeleo na kutoa huduma za kijamii kama afya, elimu nk.

Blogu hii inaomba juhudi hizi ziimarishwe na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo wa nchi hii ili umri angalao ufikie miaka 70 ya kuishi. Wadau wa maendeleo sio tu wale wanaotoa msaada mikubwa kwa taifa letu BALI hata yale mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, taasisi na makampuni ya watu binafsi (mfano kuna hospitali na shule binafsi) nk. 

Kwa habari zaidi soma mwananchi.

Monday, June 9, 2014

Hongera sana Neema Loy kwa kuanzisha blogu ya "Hayana Tuinuke"

Picha Yangu
Picha: http://neemaloy.blogspot.com/ - Neema Loy

Hongera sana Neema Loy kwa kuanzisha blogu ya "Hayana Tuinuke" . Madhumuni ya blogu uliyoianzisha ni kwaajili ya mambo mbalimbali kama vile mambo ya kielimu, kisiasa, kiuchumina mengineyo. Hakika kama mdau na mmiliki wa blogu "tuijenge tanzania" nimefurahishwa sana na jinsi ulivyovikilia na kunzisha blogu ya namna hii. Ni imani yetu kuwa blogu uliyoianzisha itakuwa taa kwa vijana wenzako katika kujiletea maendeleo. 


Licha ya kutoa habari kwa watu mbalimbali lakini blogu ni uchumi ukiangalia kwa jicho la tatu. Sina maana ya kupata pesa kupitia matangazo (kama blogu zingine zinavyofanya) ila jinsi watu wengi watakavyotembelea blogu husika basi yenyewe inapata umaarufu ambao unakuunganisha na fursa ambazo kwa sasa utaona kama ndoto. Karibu kwenye fani hii.

Hongera JK kwa kuliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wezi wa fedha za wakulima wa tumbaku mkoa wa Tabora

Picha:mwananchi.co.tz - Kilimo cha Tumbaku 
Hongera Rais Jakaya Kikwete kwa kuliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wezi wa fedha za wakulima wa tumbaku mkoa wa Tabora. Agizo hilo la Rais litawafanya wezi hao wakamatwe na kufikishwa mahakamani. Mh Rais alitoa agizo hilo wakati akizindua uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwenye Viwanja vya Chipukizi, mkoani Tabora.
Hakika blogu hii imefurahishwa na kauli hii ya Rais ya kuwashughulikia wezi wa mali za umma hasa vyama vya ushirika nchini. Blogu hii inaamini vyama vya ushirika ndio msingi wa maendeleo kwa wakulima na wanaushirika nchini. Uimara wa vyama vya ushirika ndio uimara wa uchumi wa nchi yetu. Kinyume chake kama vyama vya ushirika vinashiriki katika matendo yasiyofaa, maendeleo ya wakulima, wanaushirika na wananchi kwa ujumla hayatakuwepo na hii itasababisha uchumi wetu kuyumba. Hii haikubaliki hata kidogo. 
Blogu hii inaomba vyombo vya dola vimulike vyama vyote nchini ili kama kuna wezi wa mali za wanaushirika ama wakulima washughulikiwe kikamilifu. Blogu hii inakumbuka miaka ya nyuma jinsi vyama vya ushirika vilivyoweza kuleta mchango mkubwa katika maendeleo nchini. Mfano mzuri wa zamani ni vyama vya ushirika mkoani Kilimanjaro na Kagera kupita zao la Kahawa. Vyama imara vya ushirika ndio msingi mkuu wa maendeleo ya nchi yetu ambapo sehemu kubwa ya wananchi ni wakulima.

Hongera sana Mh Leticia Nyerere kwa kuwa mzalendo

Picha:parliament.go.tz - Mh Leticia Nyerere

Hongera sana Mh Leticia Nyerere kwa kuwa mzalendo. Hakika blogu hii imefurahishwa sana kwa jinsi alivyokuwa akichangia hoja ya kuridhia itifaki ya SADC fedha na uwekezaji katika bunge la bajeti linalofanyika Dodoma, Tanzania tarehe 06/06/2014. Mh Leticia amesikitishwa na jinsi watanzania wasivyo wazalendo, wanaoshabikia masuala ya ajabu ajabu. Amesikitishwa jinsi watanzania wasivyojivunia nchi yao na kuipenda. Ameshauri serikali iwaandae watanzania kushiriki katika jumuia hizi kama SADC na sio kuridhia tu. Watendaji wa serikali pamoja na watanzania wakiandaliwa vyema watakuwa washiriki wazuri katika SADC na kukuza uchumi wa nchi yetu. Pia watendaji wakiwa wazalendo nchi yetu itapata manufaa makubwa sana. Mh Leticia amesema watanzania wakiandaliwa na kushirikishwa kikamilifu, taifa litapiga hatua kubwa ya maendelo. Kwa kuridhia ya SADC fedha na uwekezaji, Tanzania itaweza kushirikiana na nchi nyingine katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Tuwe WAZALENDO, ili tupige hatua kubwa ya maendeleo. Asante sana Mh Leticia Nyerere kwa kuwa mzalendo.


Hakika, blogu hii imekumbushwa maneno ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere miaka ya 60, “binadamu wote ni sawa na Afrika ni MOJA

Thursday, June 5, 2014

Hongera kamati ya Bunge kwa kuitaka TRA kutoa sharti kwa TFF kutumia tiketi za kieletroniki

Picha:parliament.go.tz - Mh Luhaga Joelson Mpina (Kisesa-CCM)
Hongera kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kwa kwa kuitaka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kutoa sharti kwa Chama Cha Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kutumia mfumo wa tiketi za kieletroniki ili kuongeza mapato. Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mh. Luhaga Joelson Mpina (Kisesa-CCM) kwenye bunge la bajeti mjini Dodoma.

Hakika blogu hii imefurahishwa sana na kauli hii ya Mh. Mpina wa kuitaka TRA iweke sharti kwa TFF ili kuongeza mapato. Aidha,kwa kutumia tiketi hizi za kieletroniki zitasaidia si tu kuongeza mapato ya nchi bali pia zitaongeza mapato ya vilabu pamoja na vyama vya soka vya mikoa na wilaya ikiwemo TFF yenyewe. Hii itaongeza uwazi miongoni mwa wadau wa soka nchini Tanzania. Pia matumizi ya tiketi hizi za kielektroniki yatapunguza hujuma na kuongeza hamasa kwa wavuja jasho (wachezaji).

Blogu hii inaomba kutoa takwimu zinazoonyesha uwezekano wa mapato kuhujumiwa na kukubaliana na hoja ya Mh. Mpina ya matumizi ya tiketi za kieletroniki. Blogu hii inakumbuka wakati timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars na Msumbiji zilipocheza mnamo septemba 2007 katika mchezo huo mapato yalikuwa zaidi ya milioni 600 (605,020,000)!!! Kulikuwa na hamasa na uwazi kupita kiasi LAKINI tangia wakati huo eti Tanzania haijawahi kupata mapato kama hayo!!!! ama yanayokaribia hayo!! na tena hata kabla ya mechi hiyo miaka yote ya nyuma hakujawahi kuwa na mapato kama hayo!!! Sasa ni zaidi ya miaka 6 tangu Tanzania icheze mechi ile kubwa katika uwanja huo lakini mapato yanayopatikana katika mechi zingine za kitaifa na kimataifa ni chini ya nusu ya mapato ya mechi ile ya ufunguzi wa uwanja wa mkuu wa taifa!!! Je, hii ni sawa???

Ndio maana blogu hii inaamini kuna hisia kwamba mapato ya mechi nyingi hupotea ama uliwa na wajanja HIVYO basi UTARATIBU huu utaweka UWAZI na serikali kupitia TRA kuchukua KODI halisi ili kujenga nchi yetu TANZANIA kupitia michezo hasa mchezo wa SOKA.



Wednesday, June 4, 2014

Hongera Halmashauri ya Kinondoni kwa kuhamisha kituo cha daladala cha Mwenge ILA bado kuna changamoto

Hongera Halmashauri ya Kinondoni kwa kuhamisha kituo cha daladala cha Mwenge na kukipeleka Makumbusho. Aidha blogu hii inaipongeza Halmashauri kwa kutoa sababu ya kuhamisha na kubomoa kituo hicho. Sababu kuu ni kupisha upanuza wa barabara ya Morocco kwenda Mwenge (sababu hii ni ya msingi), sababu ya pili ni kuboresha usafi (ni ya msingi pia). Blogu hii inashauri Halamashauri kujenga barabara za lami kwa njia zote zinazoingia na kutoka kituo kipya cha makumbusho. Njia za sasa sio za lami na hii itasababisha barabara kuchimbika sana kutokana na magari makubwa (mabasi) kupita njia hizo zisizo na lami na kusababisha usumbufu hasa wakati wa mvua. Pia blogu hii inashauri uwezekano wa kupanua kituo cha Makumbusho kwa kubomoa sehemu ya soko. Kwa mtazamo wa blogu hii kituo ni kidogo. Pia utaratibu wa kituo ubadilishwe kwa maana mabasi yakae kituoni si kwa zaidi ya dakika 5 (yaani yaingie na kutoka SIO kukaa muda mrefu ili kujaza abiria). 

Pia blogu hii inaomba suala la USAFI lizingatiwe KIKAMILIFU katika KITUO kipya cha MAKUMBUSHO. 
  • Halmashauri iweke utaratibu wa kukisafisha muda wote kituo hiki (ikiwezekana kampuni ipewe zabuni ya usafi); 
  • Kuwepo na huduma za vyoo; 
  • Kuwepo na sehemu nyingi za kutupa takataka (siyo kila sehemu ni jalala); 
  • Kuwepo na faini kwa mtu yoyote atakaye tupa takataka ama uchafu wa aina yoyote; 
  • Ikiwezekana kuwe na mahakama ya papo kwa papo.
unnamed (5)
Picha:http://dewjiblog.com/ - sehemu ya kituo cha daladala cha mwenge baada ya kuzuiwa

Hongera Taifa Stars kwa kuitoa Timu ya Taifa ya Zimbabwe kwa jumla ya magoli 3-2

Hongera Taifa Stars kwa kuitoa Timu ya Taifa ya Zimbabwe kwa jumla ya magoli 3 kwa 2. Hakika huo ni ushindi mzuri ambao watanzania wote wanajivunia. Blogu hii inaomba TFF kuiandaa mapema Timu yetu kabla ya kukutana na Timu ya Taifa ya Msumbiji. Tuna amini kwa juhudi zinazoonyeshwa na wachezaji na benchi la ufundi pamoja na shirikisho la mpira Tanzania (TFF), Timu yetu itasonga mbele kwa kuing'oa Timu ya Msumbiji. Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya kocha wa Kiholanzi Mart Nooij inatarajiwa kuingia kambini jumatano ijayo. Blogu hii inaomba TFF kuhakikisha Timu yetu inapata mechi mbili za kimataifa za maandalizi kabla ya kupambana na Msumbiji. Blogu hii inawaomba wadau wasibweteke na ushindi na wajue ushindi ulipatikana kutokana na maandalizi mazuri pamoja na mechi za majaribio za kimataifa (Burundi na Malawi mara mbili). Ukiangalia hapo hizo zilikuwa mechi 3, ya kwanza tulifungwa ila ya mwisho tukashinda dhidi ya Malawi. Kwa hiyo ushindi haukuja kiwepesi ila ni kutokana na mipango, maandalizi na mechi za kimataifa za majaribio. Hivyo, blogu hii inasisitiza maandalizi na mechi za majaribio kabla ya kukutana na Msumbiji.  

Picha: bongo5.com