Picha: wikipedia
Hongera Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli kwa kutetea rasilimali za Tanzania kupitia sekta ya madini. Blogu hii imefurahishwa na uamuzi wako wa kuteua Kamati Maalum ya kuchunguza mchanga wa mabaki ya madini ya dhahabu yanayosafirishwa nje ya nchi kupitia makontena.
Kamati hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Profesa Abdukarim Hamis Mruma imefanya kazi nzuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Pia blogu hii inakupongeza kwa uamuzi wako wa leo wa kuwawajibisha wahusika na kuvunja bodi ya TMAA. Kwa mujibu wa ripoti inaonekana taifa letu linapoteza mapato makubwa kutokana na tofauti ya kiasi cha madini kinachosafirishwa kupitia makontena ya mabaki ya dhahabu na madini mengine.

Aidha, blogu hii inaomba yafuatayo:
- Watendaji wa serikali pamoja na taasisi zake ziwe makini na kufuatilia kwa karibu thamani halisi ya madini yanayochimbwa na pia kusafirishwa nje kupitia mchanga wa madini au madini halisi;
- Ni vizuri taasisi kama TMAA, TRA, TBS na mamlaka za Bandari na viwanja vya ndege wafuatilie kwa umakini kiasi halisi cha madini kinachotoka nje ya nchi na kila taasisi ikiwezekana iwe na kumbukumbu zake;
- Pia kuwepo na vifaa vya kiteknolojia vya kuchunguza kwa umakini makontena au mizigo inayopita bandarini na viwanja vya ndege;
- Vyombo vya ulinzi na usalama vishiriki kikamilifu kulinda rasilimali za taifa na hasa kupitia katika mipaka ya nchi yetu;
- Suala la MAADILI litiliwe mkazo kwa watumishi wote wa umma;
- Taifa kupitia Wizara ya Nishati na Madini linunue kifaa cha kuchenjua madini "smelter" ili taifa liweze kupata faida ya rasilimali ya madini kwa uhalisia wake.
Kila la kheri Mh Rais Magufuli katika kulinda rasilimali za taifa. Watanzania tupo nyuma yako!
No comments:
Post a Comment