Friday, December 27, 2013

Waziri wa Elimu Dr Kawambwa amewaagiza Maafisa Elimu nchini kuhakikisha walimu wapya wanalipwa stahili zao mapema

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr Shukuru Kawambwa amewaagiza Maafisa Elimu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha walimu wapya wanalipwa stahili zao mapema. Aidha waziri huyo amewaagiza maafisa hao wa elimu kuhakikisha walimu wapya wanapokelewa vizuri katika maeneo yao ya kazi.


Blogu hii inapenda kumpongeza Waziri Dr Kawambwa kwa kauli hiyo ya kuwataka maafisa elimu nchini kuhakikisha walimu wapya wengi wao wakiwa walimu vijana kulipwa stahili zao mapema. Hii itawafanya walimu hao wapya wasikatishwe tamaa ya kukaa katika vituo vyao walipopangiwa. Pia kuwajali walimu hasa wanapoajiriwa kwa mara ya kwanza inakuwa kama motisha kwao. Aidha Waziri amewaagiza maafisa hao kuhakikisha kuwa wanafuatilia suala zima la ufundishaji mashuleni na kuwa na walimu wakuu wenye sifa. 


Aidha blogu hii inaomba, wizara ya elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha walimu hao wapya wanapokelewa vizuri na wanahudumiwa ipasavyo. Ni vyema kukawa na ufuatiliaji wa karibu katika kuhakikisha walimu wanapatiwa mahitaji yao ya lazima na hasa kwa hawa wlimu wapya.


Duniani kote mwalimu ni nguzo ya Taifa na hakuna maendeleo bila elimu bora na elimu bora inatoka kwa mwalimu aliyeandaliwa na kuhudumiwa vizuri. Kwa habari zaidi soma majira


Picha: 24tanzania

Monday, December 16, 2013

Hongera Rais JK kwa kutoa hotuba nzuri sana katika mazishi ya MANDELA kijijini kwake Qunu

Sikiliza hotuba ya JK Qunu katika mazishi ya MANDELA 15/12/2013

Picha:Pool/AFP, Odd Andersen


Jana tarehe 15/12/2013 nikiwa nyumbani kwangu nikiangalia matangazo ya moja kwa moja ya luninga toka Qunu nchini Afrika ya Kusini kupitia chaneli ya MADIBA niliona na kusikiliza mambo mengi lakini mojawapo ni hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh Jakaya Mrisho Kikwete. Hakika katika hotuba hiyo JK alifunika. Kikwete aliwakumbusha wananchi wa Afrika ya Kusini walipotoka katika masuala ya kukomboa nchi yao. Kikwete aliwakumbusha wasauzi kuwa Tanzania iliwapa hifadhi pamoja na baadhi yao hati za kusafiria. Mandela alipewa yote hayo! Wasauzi enzi za ubaguzi wa rangi iliwapa hifadhi katika maeneo kama vile Kongwa, Mgagao, Mazimbu, Dakawa nk. 

Rais JK alisema Tanzania ilitoa ushirikiano wa hali ya juu na kusimamisha maendeleo yake kwa ajii ya Afrika ya Kusini. Wakati Mandela alipokuja Tanzania hakuwa na hati ya kusafiria "passport" ila alipewa "travel documents" toka Tanzania na aliweza kusafiri nchi mbalimbali. Tanzania ilianzisha Radio Freedom iliyokuwa inatangaza toka Tanzania Dar es Salaam kwa ajili ya ukombozi wa wananchi waliokuwa wanabaguliwa wa Afrika ya Kusini. Radio hii ilisaidia kuimarisha juhudi za ukombozi kusini mwa Afrika. Pia JK alisema, MANDELA alipokuwa anakuja Tanzania alikuwa haishi hotelini bali kwa watu binafsi ili kulinda usalama wake.

Hakika JK amewafungua macho na masikio wasauzi juu ya uhusiano uliokuwepo kati ya wananchi wa nchi hizi mbili na hasa wakati wa ukombozi. Hakusau kusema kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipigania sana ukombozi wa wananchi wa Afrika ya Kusini na alikuwa rafiki wa MANDELA. MANDELA alianza kutembelea Tanzania kutoka Afrika ya Kusini akipitia Northern Rhodesia, Tanganyika (Town of Mbeya) mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya kuomba msaada wa ukombozi na kupatiwa mafunzo ya wapigania uhuru na ubaguzi wa rangi.

JK alisema, Mandela alipotolewa gerezani na kutembela Tanzania miaka ya 90 alipokelewa na wananchi wengi waliokuwa na shauku ya kumuona mwanamapinduzi huyo. JK alisema licha ya mvua kubwa wananchi wa Tanzania walizidi kujitokeza kumshangilia. Nakumbuka wakati huo na mimi nilipata fursa ya kumuona akiwa pamoja na Mwalimu Nyerere na Winnie Mandela kwenye gari la wazi wakielekea Ikulu toka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam.

Blogu hii inampongeza sana JK kwa kutoa hotuba nzuri na kuwaeleza jinsi Tanzania ilivyoshiriki kikamilifu katika ukombozi kusini mwa afrika na hasa ukombozi dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Blogu hii inaomba taasisi husika ziweze kutunza kwa umakini na umaridadi mambo yote ili vizazi vijavyo na wageni waweze kujua jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika ukombozi. Maeneo yote ambayo kulikuwa na historia ya ukombozi hasa maeneo ya Morogoro yawe chini ya makumbusho ya Taifa ili pamoja na mambo mengine iwe mojawapo ya pato la taifa kupitia wageni toka nje nchi. Pia kuwe na matangazo kupitia radio, luninga, magazeti, internet juu ya historia, makumbusho na vitu vya kale vilivyopo Tanzania. Wenzetu mambo haya yanaingiza fedha na sisi tuchangamke!

Sikiliza hotuba ya JK Qunu katika mazishi ya MANDELA 15/12/2013

Sunday, December 8, 2013

Hongera sana IVO MAPUNDA kwa kutupeleka NUSU FAINALI kombe la Challenge nchini Kenya

HONGERA kipa wa KILIMANJARO stars IVO MAPUNDA. Katika mechi ya robo fainali ya kombe la challenge dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda, mlinda mlango huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Kenya akidakia moja ya vilabu nchini humo ameonyesha umahili wa hali ya juu sana. Katika mechi hiyo ya robo fainali iliyofanyika jumamosi tarehe 7 disemba 2013, MAPUNDA aliokoa penati mbili ambazo ziliiwezesha Kilimanjaro stars kutinga Nusu Fainali. MAPUNDA alikuwa kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Tanzania miaka ya nyuma lakini baadae alitemwa!! Mwaka huu kocha wa Timu ya Taifa ya Bara alimjumuisha kwenye kikosi cha Kili stars.

Lakini MAPUNDA inaonekana sasa amerudi kwenye kiwango chake na ameonyesha uwezo na kujituma. Hakika blogu hii inampongeza MAPUNDA kwa kutupeleka NUSU FAINALI lakini pia kwa kulipigania TAIFA kwa umahili mkubwa. Kwa walioangalia mechi ile na zingine watakubaliana na blogu hii kuwa MAPUNDA alijituma sana na kuonyesha juhudi kubwa. Blogu hii inaomba wachezaji wengine wa kitanzania waonyeshe juhudi kama alivyoonyesha MAPUNDA. Kwa kucheza kwa juhudi kama alivyofanya MAPUNDA kunaweza kutufikisha mbali katika mashindano ya kimataifa.

Picha:footballzz.com

Tuige siasa za Komredi MANDELA kumuenzi _ aliwaunganisha watu wote bila ya kubeza wengine!

Hakika Kifo cha Komredi Nelson Mandela wenyewe wanamwita MADIBA kimetikisa dunia hasa Tanzania. Kiongozi huyu tunaweza kusema ni wa kufikirika! Alipinga ubaguzi wa rangi dhidi ya utawala wa makaburu kule Afrika ya Kusini. Alifungwa zaidi ya miaka 27 na kuteswa sana. Licha ya mateso hayo alizidi kuwa mtetezi wa wanyonge akiwa gerezani na kukataa msamaha wenye masharti.

Baada ya kutolewa gerezani miaka ya tisini alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza mweusi katika utawala wa kidemokrasia nchini Afrika ya Kusini. Kikubwa ambacho wengi KINATUSHINDA! ni kuwa aliwasamehe wote waliomkosea wakati wa UBAGUZI WA RANGI!! Aliwasihi waafrika weusi WASILIPIZE KISASI dhidi ya wazungu! Aliwahimiza WAAFRIKA weusi wasiwabeze na kuwasimanga WAZUNGU ila washirikiane kujenga TAIFA JIPYA. 

Mandela aliamini adui alikuwa ni ubaguzi wa RANGI!!! na sio RANGI ya MTU!! Kibinadamu sio rahisi kusamehe watu waliokupa mateso makali. Mandela aliepusha mauaji ya kisasi dhidi ya wazungu. Kama angekuwa kiongozi wa visasi, Afrika Kusini kungekuwa na mauaji ya kutisha dhidi ya watu weupe. Hii ingetokana na waafrika weusi kulipiza kisasi na kuwabeza weupe!! Mandela alikataa hayo yote na kuchukuliwa wananchi wote wa Afrika ya Kusini kama kitu kimoja bila kujali RANGI ya MTU!! Hakika Dunia itamkumbuka sana Mandela!

Blogu hii inaomba hulka, tabia na mwenendo wa MANDELA uigwe na VIONGOZI wa sasa ndani ya DUNIA hii ambayo tupo kwa MUDA tu. Blogu hii inaomba siasa za kubezana, za visasi na zisizo na tija kuepukwa na viongozi na watu wote. Lengo kwa wote ni kuleta maendeleo na sio kubezana na siasa zisizo msaidia mtu wa kawaida. Ukiangalia MANDELA hakuwahi hata siku moja kufurahia udhaifu wa wengine mara baada ya kuwa RAIS wa Afrika Kusini ila aliwashika mkono hata wale walioaminika kuwa walikuwa maadui zake enzi za ubaguzi wa RANGI.

Hakika, MANDELA ni SOMO kubwa kwa WAAFRIKA, katika kuleta ustawi na maendeleo ya kistaarabu ya bara hili lenye migogoro isiyo na tija.

R.I.P MANDELA!! MWENYEZI MUNGU UIWEKE ROHO YAKE MAHALA PEMA PEPONI AMINA!!!
Picha:consortiumnews.com

Friday, November 22, 2013

Hongera serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kutoa Sera ya Gesi nchini

Hongera serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kutoa sera ya gesi ya mwaka 2013. Sera hii imeeleza wazi kuwa gesi ni mali ya taifa na inapaswa kuwanufaisha wananchi na pia itauzwa nje ya nchi pale tu mahitaji ya ndani yatapotimizwa. Sera hiyo imeainisha kuwa ni lazima serikali na wananchi wanufaike na rasilimali hiyo na pia kunakuwa na haki na usawa kwa wadau katika uvunaji na utumiaji wa rasilimali hiyo. Sera hiyo imesisitiza kujenga mifumo ya kitaasisi, miundombinu na nguvu kazi ya kuhudumia na kuendeleza sekta ya gesi nchini.

Hakika blogu hii inaipongeza sana serikali pamoja na wadau wengine kwa kufanikisha sera hii muhimu kwa taifa. Ni wakati muafaka kwa wadau na wananchi kuchangamkia fursa itakayotokana na uchimbaji na usambazaji wa gesi nchini. Ni matumaini ya blogu hii kuwa uchimbaji na usambazaji wa gesi utanufaisha taifa na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla. 

Photo:dullonet.com




Photo:dewjiblog.com


Wednesday, November 20, 2013

Hongera Mh. Ummy Mwalimu kwa kulinda na kutetea haki za watoto pamoja na kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji

Mh. Ummy Mwalimu leo ameshiriki katika maadhimisho ya siku ya Maombi na Vitendo kwa Watoto, katika viwanja vya Don Bosco mjini Dar es Salaam. Washiriki wengine katika maadhimisho hayo walikuwa Global Network of Religions for Children (GNRC), InterReligious Council of Peace Tanzania (IRCPT) na UNICEF. Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na UN Universal Children's Day. Ambapo KauliMbiu ya Mwaka huu ni "Zuia Ukatili Dhidi ya Watoto". Mh. Ummy alipata fursa ya kuelezea hatua mbalimbali za kisera na kisheria zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya Ukatili dhidi ya watoto. 

Mh. Ummy amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Mtoto imeanza kutekeleza Mpango wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto 2013-2016. Mpango huu umejielekeza katika kuimarisha mifumo ya kisheria katika utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya 2009 na katika kujenga mifumo imara ya ulinzi wa mtoto kwa ajili ya kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili. Mh Ummy ameiomba jamii kwa ujumla kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinakoma. Pia amewaomba wazazi, walezi, viongozi wa dini, watoto na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na kuzingatiwa. 

Hakika blogu hii inampongeza sana Mh. Ummy kwa jitihada anazofanya za kulinda na kutetea haki za watoto pamoja na kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wafanyiwavyo watoto.

Blogu hii inaomba jamii kwa ujumla kushirikiana na Mh Ummy pamoja na serikali kwa ujumla kupinga vitendo vya ukatili wa watoto. Pia jamii kuripoti kwenye vyombo vya dola waonapo uwepo wa vitendo vya ukatili kwa watoto. Blogu hii inaamini kwa kufanya hivyo, vitendo vya unyanyasaji vitapungua ama kwisha kabisa. Pia blogu hii inaomba mkakati wa kupinga unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto uanzie kwenye shule za awali, msingi mpaka sekondari. 

Sio lazima kukawa na mtaala rasmi ila kuna kitu kinaitwa "hidden curriculum" ambapo walimu watapewa maelekezo ama mafunzo ya namna ya kuwaelimisha watoto juu ya HAKI na WAJIBU wao. Baadhi ya nchi zinafanya hivyo, mfano mtoto akinyanyaswa anaelekezwa ama anafundishwa wapi apeleke taarifa hata kama atakayekuwa anamnyanyasa ni mzazi, mlezi ama ndugu. Mbali na kufundishwa HAKI na WAJIBU wao WATOTO pia wafundishwe kwa njia hiyo hiyo UZALENDO, USAFI NA MAZINGIRA, MICHEZO nk ili angalao utupaji wa taka ovyo ukome, rushwa ikome na MATOKEO yake ni baada ya miaka 10 ama 15 taifa litapiga hatua kubwa ya maendeleo!

Viwanja vya Don Bosco mjini Dar es Salaam

Thursday, November 14, 2013

Tuongeze kasi ya ujenzi wa viwanda ili kuwapa ajira vijana waliomaliza mafunzo ya ufundi VETA

Miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa na kiwanda cha kuunganisha magari makubwa yaitwayo SCANIA mjini Kibaha mkoani Pwani. Kiwanda hicho cha kuunganisha MAGARI ya aina hiyo mbali na kuinua uchumi wa nchi kupitia mapato kama vile kodi pia kilileta mchango mkubwa kwa vijana waliopitia mafunzo ya ufundi (siku hizi VETA nk).

Viwanda vya aina hii vipo sehemu nyingi duniani ikiwemo Afrika ya Kusini, katika jiji la Johannesburg. Kiwanda hiki kilichopo Afrika ya Kusini mbali na kuinua uchumi wa nchi hiyo kina ajili vijana waliomaliza mafunzo mbalimbali ya ufundi ikiwemo mafunzo kama yatolewayo na VETA nchini Tanzania.

Blogu hii inaomba kuwepo na viwanda vya aina hii na hasa kurudisha kiwanda cha kuunganisha SCANIA nchini Tanzania ili mbali na kuinua uchumi kupitia kodi na mauzo ya MAGARI husika ndani na nje ya nchi pia kitaajiri vijana wengi waliopitia mafunzo ya ufundi. Hali hii itawafanya vijana wapate ajira na kupunguza uhalifu nchini. 

Blogu hii inaamini serikali na wadau wengine wametumia pesa nyingi kujenga vyuo vya ufundi VETA, hivyo basi ili mafunzo hayo yalete matunda inabidi kuwe na viwanda vya aina hiyo.

Hata hivyo nchini Tanzania kuna ongezeko la viwanda mbalimbali ambavyo vinatoa fursa kwa vijana kupata ajira na kutumia ujuzi wao walioupata toka  vyuo mbalimbali vya VETA na hivyo kujiongezea kipato na kuinua uchumi wa nchi. 

Kasi ya kujenga viwanda kupitia sekta binafsi na wawekezaji wakubwa inabidi iongezwe kwa kushirikiana na serikali.

Picha: Geofrey Kalumuna




Monday, November 11, 2013

Rais UHURU KENYATTA wa KENYA asema KENYA iko tayari kushirikiana na Tanzania

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kupitia waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Mh. Amina Mohamed, ametuma salamu akisema kuwa nchi ya Kenya iko tayari kushirikiana na Tanzania. Hata hivyo, Rais wa Kenya amesema kwamba  walijiingiza katika mazungumzo na Uganda pamoja na Rwanda kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta na reli bila kufahamu kwamba ilikuwa inavunja misingi iliyowekwa na jumuiya hiyo.
 
Hakika hatua hii ya kistaarabu ni ya kipekee na inastahili kupokelewa kwa mikono miwili na watanzania pamoja na Rais wetu JK. Yalizungumzwa mengi, kabla ya Rais Kenyatta kutoa msimamo huo kupitia waziri wake wa mambo ya nje.
 
Blogu hii inaamini kuwa UMOJA NI NGUVU! NA UTENGANO NI UDHAIFU. Ikumbukwe, Tanzania ni sehemu ya AFRIKA MASHARIKI kijiografia, kihistoria, kiasili na pia itakuwa kosa kubwa sana kujitoa!. Ni furaha ya blogu hii kuwa kweli JK alizungumza vitu vya kweli vilivyotokea kabla. Hii inadhibitishwa na kauli ya UHURU na sasa angalau mambo yatakuwa shwari. AFRIKA MASHARIKI IDUMU!
 
Picha: mwananchi -  Mh. Bernard Membe (waziri wa mambo ya nje wa Tanzania) na Mh. Amina Mohammed (waziri wa mambo ya nje wa Kenya)

Saturday, November 9, 2013

Wazo la leo - Watanzania tujadili hoja za msingi zilizo mbele yetu

Watanzania tuache siasa za maji taka!!!Tujadili hoja za msingi zilizo mbele yetu kama vile elimu, katiba, madini, maliasili, upatikanaji wa maji na umeme nk. Tuache ushabiki wa uNCCR, uCUF, uCCM, uUDP, uCHADEMA nk!!! Tuache kudharirisha watu bila sababu za msingi. Kumbukeni JK ni RAIS tupende au tusipenda! kumdhihaki si jambo zuri hata kidogo. Twende kwenye hoja ya msingi kama mtanzania mmoja mmoja!! kuitana majuha haisaidii. Nitawapa mfano, JK ameonyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa, ameweza kukutana na makundi mbalimbali ya jamii na kisiasa na kusikiliza maoni yao. Hakika JK amewafunda wanasiasa wa Tz kuwa siasa sio fitna, matusi ama kubeza mawazo ya mwenzio bali siasa ni maridhiano, maelewano, upendo, maendeleo, amani bila ya kudharau maoni ya watu hata kama ni wengi ama wachache!! Watanzania hasa vijana badilikeni ili nchi yetu iweze kupiga hatua ya maendeleo. Mimi nimefurahi wakati JK anahutubia bunge majuzi Mwenyekiti na Mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alikuwa akipiga makofi mara kwa mara wakati JK alipokuwa anahutubia. Upigaji makofi ule umeonyesha hata wapinzani wanaunga mkono hoja zinazotolewa na upande wa pili wa shilingi hata kama mtoa hoja yuko chama tawala ama chama kingine! Hali hii ndio watanzania wanayohitaji. Tujadili hoja za msingi kwa watanzania na watanzania watawaunga mkono viongozi hao bila kujali wanatoka upande gani wa shilingi. JK bila kumugunya maneno ameonyesha weledi, ustaarabu, uungwana na ukomavu wa hali ya juu, amejali maslahi ya watanzania wote bila ubaguzi, nendeni youtube ama kwenye mitandao ya kijamii kuangalia hotuba yake hiyo aliyoitoa bungeni hivi karibuni Dodoma. Hakika JK amekuwa kama mwalimu JKN!! Sasa na sisi tufuate nyayo zake na tuache siasa za kuchafuana ambazo hazitatufikisha popote. Tanzania tunataka maendeleo ya kweli na sio malumbano yasiyo na tija. Tanzania kwanza, ubinafsi nyuma!

Sunday, October 27, 2013

Wazo la busara toka kwa mdau wa elimu Geofrey Kalumuna - wadau wa elimu na walimu tubadilike!

Nilichoongea wakati wa uzinduzi wa jengo la " Teachers Professional Center" pale DUCE, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu! hakikuwa kitu cha ajabu sana. Ni mambo wenzetu wanayoyafanya siku zote. Kwa dunia ya sasa huwezi kwenda kasi ya maendeleo bila ya kukopa toka ICT. Huwezi kuwafikia walimu ambao ndio nguzo ya taifa bila ICT. Nitawapa mfano mmoja ili mwanafunzi wa kawaida aelewe somo vizuri bila kukalili lazima ASOME (hapa sisi walimu wengi ndio tunapoteza nguvu zetu! Kuwasomea wanafunzi tukizani tunawafundisha! Hiyo haitoshi!), AONE (hapa ndipo wenzetu wanapotuacha na ndio wanatilia mkazo -ICT inaingia hapa unaweza tumia ICT kutengeneza animations ukaziweka kwenye CD au ukachukua video kuelezea concept ya "reproduction" badala ya kulazimisha kuwasomea), na KUTENDA (hapa pia wenzetu nchi zingine wanatupiga bao! Hatufanyi hivyo kwa visingizio kibao eti hakuna mahabara nk wakati waweza tumia ICT ama vitu vinavyopatikana kwenye mazingira yako na wanafunzi wakafanya na kuelewa somo! Mfano tuna vyura wengi kwenye mazingira yetu na kwenye baadhi ya mitihani ya kidato cha nne wanafunzi wanatakiwa kufanya practicals za kupasua vyura lakini ni mara ngapi walimu wa biology wanafanya practical hizo kwa wanafunzi wao ili kuwaelewa concepts kwa vitendo? Ila tunasingizia hatuna vifaa wakati tuna mapanya tena mapanya buku mitaani bila kuacha machura yanayotupigia kelele usiku). Kwa kifupi nilichozungumza sio kitu kigeni ila ni utamaduni wetu wa kutotumia fursa kama walimu na wadau wa elimu. Teknolojia niliyozungumza ambayo yaweza saidia "in-service teachers" vyuo vingi wanatumia kule University of UP Daudi Danda unajua mambo online teaching ya illuminate! Sasa kwa jinsi gani teknolojia hiyo inaweza kutusaidia kuwapa maarifa na ujuzi walimu wetu kwa gharama nafuu! Maana sio rahisi kuleta walimu wote kwenye chuo kama DUCE na kuwapa mbinu za kisasa bila ya kutumia teknolojia!
Mdau: Geofrey Kalumuna


Saturday, October 26, 2013

Tanzania 10 - Msumbiji 0 - Hakika Timu ya Taifa ya Wanawake walio chini ya miaka 20 watatupeleka Canada kwenye kombe la dunia!

Hongera Timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 kwa ushindi mnono mlioupata leo kwenye uwanja wa taifa.
Mchezo wa leo ni harakati za Timu yetu kuwania kuingia fainali za wanawake zitakazofanyika nchini Canada mwakani kupitia kanda ya Afrika. Timu yetu imepata ushindi wa mabao 10 kwa 0!
Hakika Timu hii imetutoa kimasomaso licha ya wadau wa michezo nchini kuwa bize na uchaguzi wa bodi ya ligi na ule uchaguzi wa shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF).
Lakini blogu hii inaungana na wadau wa michezo nchini hususan kandanda kuipongeza Timu yetu ya wanawake kwa ushindi mkubwa walioupata.
Tunaomba wale wote walio bize na uchaguzi wahakikishe wakishachaguliwa wanatilia mkazo uanzishwaji wa ligi ya wanawake nchini Tanzania ili tuweze kupata wachezaji bora watakaoliwakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa.
Picha: landboybeibe

Thursday, October 24, 2013

Hongera Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na DUCE kwa kujenga kituo maalum "Teachers Professional Center"

 
 


Hongera serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kujenga kituo maalum katika chuo kikuu kishiriki cha DUCE kiitwacho "Teachers Professional Center". Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Gharib Bilal alikuwa mgeni rasmi katika halfa hiyo ya uzinduzi iliyofanyika Jumatano ya tarehe 23 mwezi wa kumi mwaka 2013.

 

Aidha kama mdau nilipata fursa ya kutoa mada mbele ya Makamu wa Rais Mh Gharib Bilal jinsi gani kituo cha "Teacher Professional Center" kinachomilikiwa na DUCE kinavyoweza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuchangia ubora wa Elimu nchini na hasa kuweza kuwapa maarifa na ujuzi walimu (in-service teachers) kupitia Teknolojia ya kisasa ili kuongeza maarifa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini na kuongeza ufaulu. 

 

Uzinduzi wa kituo hiki unaenda pamoja na kauli mbiu ya "Big Results Now" yaani "Matokeo Makubwa Sasa" katika sekta ya elimu nchini Tanzania.

 

Blogu hii inapenda kuipongeza serikali ya Tanzania chini ya Mh Rais Jakaya Kikwete kwa ujenzi wa kituo hiki maalum kitakacho chochea kasi ya elimu nchini na hasa kitakachokuwa kikitumika kutoa mafunzo kwa walimu walio makazini kupitia Teknolojia ya kisasa. Aidha blogu hii inakipongeza chuo kikuu kishiriki cha Elimu DUCE kwa kuweza kutekeleza ujenzi wa kituo hiki. Vile vile blogu hii inawapongeza wadau na wafanyakazi wa DUCE pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika kusimamia ujenzi wa kituo hiki.

 

Pia blogu hii inatoa pongezi na shukrani za pekee kwa Benki ya Dunia (World Bank) kupitia mpango mahsusi uitwao "Science Technology and Higher Education Program (STHEP) " uliofanikisha miradi mingi nchini kwenye sekta ya elimu juu ukiwemo mradi huu wa wa ujenzi wa  "Teacher Professional Center" ndani ya chuo kikuu kishiriki cha DUCE.

 

Blogu hii inaomba kituo hiki kitunzwe na pia kitumike kikamilifu ili kukizi lengo la kituo chenyewe pamoja na kufikia malengo ya BIG RESULTS NOW! Pamoja tutafika!
 

 







 



 


Friday, October 18, 2013

Hongera YANGA kwa kuonana na Mstahiki Meya wa Ilala ya kuomba nyongeza ya eneo la kujenga uwanja

Hongera sana klabu ya YANGA kwa kuwa na wazo la uwanja wa kisasa ambao michoro ya awali ishachorwa na wataalamu. Pili blogu hii ina upongeza uongozi wa klabu ya YANGA kwa kuonana na Mshahiki Meya wa Manispaa ya Ilala na kutuma maombi ya kuongeza eneo la kiwanja. Hakika juhudi hizi zinastahili kuungwa mkono na wadau wote wa michezo hususan mpira wa miguu aka kandanda AMA kabumbu. Kwa mujibu wa mtandao wa YANGA Meya wa Manisapaa ya Ilala jijini Dar es salaam mstahiki Jerry Slaa leo amepokea maombi ya klabu ya Young Africans kuhusu kuomba eneo la ziada kwa ajili ya kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa uwanja wa kisasa eneo la jangwani.
Juhudi hizi sio ndogo na zinapaswa kuendelezwa. Wapo watu wanafikiri hii ni ndoto la hasha bali inawezekana kwa Klabu kama YANGA kujenga uwanja wa kisasa. YANGA ina wadau wengi sana ndani na nje ya nchi. 
Kinachohitajika ni kwa YANGA kuunda kamati ya ujenzi itakayowashirikisha wadau wa YANGA wakiwemo wataalamu mbalimbali wa ujenzi, wataalamu wa masoko, wataalamu wa ardhi na miundombinu, makocha, wachezaji wa zamani, wafanyabiashara, wanasiasa bila kusahau wakeleketwa YANGA wakiwemo na wanachama na baadhi ya wajumbe toka kwenye uongozi wa YANGA. Muhimu kamati iwe na watu makini na wanaoaminika ili moja ya jukumu ni kuandaa mpango mkakati na pia kuusimamia mpango huo. Mpango huo uonyeshe roadmap ya kupata fedha na na namna pesa itakavyotumika.Klabu nyingine zinapaswa kuiga mtizamo wa YANGA ili Tanzania ipige hatua kwenye maendeleo ya soka.
Kwa habari zaidi bofya hapa.

Wednesday, October 16, 2013

Hongera blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania"

Hongera blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania" ambayo lengo lake kuu ni kuwasaidia wafugaji nchini Tanzania kupata elimu bora ya kisasa ya ufugaji ili waweze kupata matokeo mazuri na kuwasaidia kupata kipato kwa kupunguza hasara ambazo zinaweza kutokea kutokana na magonjwa mbalimbali.
 
Blogu ya "tuijengetanzania" inaipongeza blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania" kwa kuanzisha blogu inayowasaidia wafugaji nchini ili kuwasaidia katika kupambana na changamoto za ufugaji kama vile magonjwa ili kuweza kuwafanya wafugaji kupata faida kubwa.
 
Wadau wa ufugaji na hasa wafugaji wadogo wadogo nchini Tanzania wanaombwa kutembelea blogu ya "sekta ya mifugo Tanzania" ili kuweza kupata taarifa na maarifa juu ya ufugaji. Taarifa na maarifa watakayopata yatawafanya waepuke magonjwa na kuweza kujua dalili, kinga na matibabu ya magonjwa ya wanyama wafungwao na kupata faida kubwa.
 
 
 
 

Tuesday, October 15, 2013

Hongera serikali ya Tanzania kwa kuanzisha Tume ya TEHAMA “ICT” nchini

Hongera serikali ya Tanzania kwa kuanzisha Tume ya TEHAMA “ICT” nchini Tanzania. Hakika hatua hii ya serikali ni ya kuungwa mkono. Wadau wa TEHAMA nchini tumefurahi na kufarijika sana baada ya kusikia serikali ipo kwenye mchakato wa kuanzisha tume ya TEHAMA. Tume hii itaratibu, itasimamia na kuendeleza shughuli zote ya TEHAMA nchini. Sekta hii ya TEHAMA inakuwa kwa kasi sana duniani na hapa nchini. Sekta hii pia inaingia kwenye kila nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Hivyo ili Tanzania iwe na mafanikio kupitia sekta hii, Tume ya kuratibu TEHAMA ni ya umuhimu sana.
Kwa uchache, TEHAMA ina chagamoto zake kama vile uwepo suala la usalama wa taarifa za watu mbalimbali (e-security), haki ya faragha (e-privacy),  pamoja na haki ya wanachi kupata taarifa (freedom of information). Mambo haya kwa kweli yana umuhimu wake lakini yanakinzana. Nchi mbalimbali bado zinachangamoto ya kuweka mstari kati ya haya mambo matatu.
Hivyo basi pamoja na mambo mengine Tume hii tunatarajia itakuja na mfumo ama uwezo wa kulinganisha masuala haya matatu ili yasilete athari nchini.
Pia ni wakati muafaka kwa serikali kupitia tume hii kuanzisha sera mbalimbali za TEHAMA kama vile sera ya mitandao ya kijamii (social media policy), sera ya mkonga wa internet (broadband internet policy) pamoja na kupitia tena sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 (ICT policy of 2003). Sera hii imekaa kwa muda mrefu na inahitaji mapitio  “review”.
Kuna mambo mengi sana ambayo tume hii ina kazi kubwa ya kufanya. Lingine ni kuhamasisha na kutoa kipaumbele sehemu za vijijini kuwa na TEHAMA na huduma za internet na data. Njia mojawapo ni kwa tume kuweka “incentive” kwa makampuni ama watu wataowekeza vijijiji ili taifa letu liweze kupiga kasi inayostahili. Incentive hii inaweza kuwa kwenye kodi.
Hakika kuna mambo mengi ya kufanya, hivyo kama wadau tunaipongeza sana serikali kwa kuwa na wazo hili la kuanzisha tume ya TEHAMA nchini. Hakika tupo pamoja na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha TEHAMA inakuza uchumi na kuleta ustawi nchini.
Picha: sundayshomari.com
prisca_tena_fee8f
Afisa Habari Mwandamizi toka Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia Bi. Prisca Ulomi(kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu Uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, wakati wa Mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO)

Mh. Ummy Mwalimu atumia siku ya kimataifa ya mtoto wa kike  jijini Tanga kuzindua Mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga kupitia TAWODE

Siku ya tarehe 11 oktoba mwaka huu ilikuwa siku ya kimataifa ya Mtoto wa Kike. Mh. Ummy Mwalimu Naibu waziri wa maendeleo ya wanawake, jinsia na watoto alitumia siku hiyo  jijini Tanga kuzindua Mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga chini ya Taasisi ya Tanga Women Development Initiative (TAWODE).
 
Mgeni rasmi alikuwa Mhe Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga. Kupitia mradi huu Mh. Ummy  ametekeleza kwa vitendo dhamira yake kama kiongozi - aliyechaguliwa na wanawake wa mkoa wa Tanga katika kuchangia na kuboresha maisha ya wanawake wa mkoa wa Tanga.

Mradi huu  utakaotekelezwa katika Wilaya za Pangani, Muheza, Mkinga, Lushoto na Tanga Mjini, umelenga kuchochea uwezo na ubora wa wasichana wenye umri wa miaka 10-24 kutambua weledi na umuhimu wao kwa maendeleo yao na ya jamii zao. Kupitia Mradi huu Mh. Ummy na wenzake wamedhamiria kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wasichana waliopo katika shule za Serikali za Msingi na Sekondari, kuboresha hali ya afya ya uzazi, kupunguza mimba za mapema, ndoa za utotoni na maambukizi ya virusi vya ukimwi. Aidha wamepanga kuwafikia moja kwa moja wasichana 16,000 na zaidi ya 100,000 kupitia njia mbalimbali ikiwemo mabango, Radio jingles (Mwambao FM 106.0), matamasha ya wasichana nk. Aidha Wasichana 1,000 waliopo shuleni na wanaoishi katika mazingira magumu wataingizwa katika Mfuko wa Bima ya afya ili kuweza kupata huduma za afya bure. Ni imani ya Mh. Ummy kuwa jitihada hizi zitachochea maendeleo ya wanaTanga kwa jumla. 

 
Hakika blogu hii imefurahishwa sana na Juhudi azifanyazo Mh. Ummy na wenzake. Blogu hii inamwomba Mh. Ummy azidi kuongeza Juhudi hizi ndani ya mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Blogu hii pia bado inatambua mchango wa Mh. Ummy nchini Tanzania katika kusimamia masuala ya wanawake na watoto.
 
Blogu hii inamwomba Mh. Ummy kupitia wizara yake kuweka sheria kali zinazowalinda watoto mfano sheria zinazokataza watu wenye umri mkubwa kufanya ngono na vitendo vya kingono na watoto wadogo chini ya miaka 16 ama 18. Sheria hizi zipo kwa wenzetu na ni kali ambazo zinawalinda watoto hasa wa kike na watu wajulikanao kama "sugar dad". Hakika zipo sheria nyingi ambazo kupitia wizara husika wanaweza kuziingiza kwenye system